Kubenea asema, Sitta mwongo


Fred Okoth's picture

Na Fred Okoth - Imechapwa 26 October 2011

Printer-friendly version
Waziri wa Afrika Mashariki, Samwel John  Sitta

MKURUGENZI mtendaji wa gazeti la MwanaHALISI, Saed Kubenea, amekana tuhuma kwamba gazeti lake “limenunuliwa na watuhumiwa wa ufisadi nchini.”

Waziri wa Afrika Mashariki, Samwel John Sitta, amedai kuwa Kubenea na gazeti lake wamenunuliwa na watuhumiwa wa ufisadi kutokana na kumshambulia yeye na “wapiganaji wenzake” katika vita dhidi ya ufisadi.

“Mafisadi wanatumia magazeti yao na magazeti mengine kunishambulia. Huko nyuma walikuwa wanatumia magazeti ya Tanzania Daima na Tazama Tanzania. Lakini sasa, wamemnunua hata huyu kijana wetu, Kubenea na gazeti lake la MwanaHALISI…” alisema Sitta.

Tuhuma hizo nzito ziliibuliwa juzi Jumatatu wakati Sitta akihojiwa katika kipindi cha “Dakika 45” kinachorushwa na kituo cha televisheni cha ITV.

Spika huyo wa zamani wa Bunge alidai gazeti hilo lilianza vizuri, lakini sasa limeanza kuyumba baada ya kutumiwa kupambana na wanaopinga ufisadi.

Hatua ya Sitta kuituhumu MwanaHALISI imekuja miezi sita baada ya gazeti kuripoti ushiriki wa kiongozi huyo kwenye uanzishwaji wa Chama cha Jamii (CCJ).

Katika toleo lake la 18 Mei 2011, gazeti liliripoti juu ya Sitta kuwa nyuma ya ujio wa CCJ. Lilinukuu Fred Mpendazoe, mbunge wa zamani wa Kishapu (CCM), ambaye ni miongoni mwa waanzishili wa chama hicho na aliyekuwa swahiba mkubwa wa Sitta.

Wengine ambao Mpendazoe aliwataja kuwa ama washiriki au waanzilishi wa CCJ, ni Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk. Harrison Mwakyembe, katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, katibu msaidizi wa CCM wilayani Moshi Mjini, Daniel ole Porokwa na kada wa chama hicho, Paul Makonda.

Akiongea na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake, Kubenea amesema tuhuma za Sitta “zinastahili kjibiwa kwa uzito unaostahili kwa vile ni uongo na upuuzi mtupu ambao umelega kuharibu sifa za gazeti, wamiliki na waandishi wake.”

“Kuna watu wanaotuchukia na kila siku tunaongeza maadui wapya kutokana na kazi tunaoifanya. Miongoni mwa maadui wetu wa sasa, tunaona yumo Samwel John Sitta aliyechukizwa na hatua ya gazeti letu kufichua ushiriki wake kwenye CCJ. Ndiyo maana ameamua kukaa chini, kutunga tuhuma na kuziporomosha,” ameeleza Kubenea.

Amesema, “Natambua mchango wa Sitta katika mapambano dhidi ya ufisadi, hasa alipokuwa Spika wa Bunge la Muungano. Lakini tatizo kubwa linalomkabili mwanasiasa huyo, ni kule kutaka kuandikwa anavyotaka na siyo alivyo…”

Kubenea amesema, “Hatujawahi, hata mara moja, kuandika habari, makala au kitu chochote chenye mwelekeo wa kushambulia Sitta binafsi. Kazi tuliyoifanya ni kuripoti kilichopo. Labda kama hilo ndilo kosa letu.”

“Tulitarajia angetupongeza kwa kutimiza wajibu wetu kwa kuwaambia Watanzania ukweli, badala ya kutushambulia na kutulaani. Tulidhani angetumia makala na habari tulizochapisha kujikosoa, kwa kuwa yeye ni binadamu kama wengine. Hatukutarajia kutumia fursa aliyopewa kutushambulia,” ameeleza Kubenea.

Akiongea katika kipindi hicho, Sitta alikiri kufuatwa na watu mbalimbali kujiunga na vyama vyao. Bali aligoma kuzungumzia bayana ushiriki wake kwenye CCJ. Alisema CCM kinahitaji mageuzi makubwa kabla hakijakutwa na kiama.

Inadaiwa Sitta alikuwa miongoni mwa waanzishili wa CCJ. Mkakati ulikuwa ni kuondoka ndani ya CCM kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010. Baadaye yeye na kundi lake walipanga kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ili kuongeza nguvu ya kuiondoa CCM.

Kuna taarifa kwamba Sitta ndiye alikuwa akilipia pango la ofisi. Ndiye alikuwa anatoa fenicha za ofisi na ndiye alikuwa analipa mishahara ya katibu mkuu wa CCJ, Renatus Muabhi na mwenyekiti wake, Richard Kiyabo.

Hii si mara ya kwanza Sitta kutoa kauli ambazo baadaye zimeonekana kumponza na wakati mwingine kumvunjia heshima.

Kwa mfano, Januari 2008, alibeza madai na vielelezo vilivyotolewa bungeni na Dk. Slaa kuhusu tuhuma za ukwapuaji wa mabilioni ya shilingi ndani ya Benki Kuu ya taifa (BoT), ikiwamo wizi uliofanywa na kampuni ya Kagoda Agriculture Ltd., iliyokwapua zaidi ya Sh. 60 bilioni.

Dk. Slaa ambaye wakati huo alikuwa mbunge wa Karatu, aliwasilisha vielelezo hivyo kujenga hoja ya kutaka Bunge liunde kamati ya kukagua hesabu za BoT.

Akipinga hoja ya Dk. Slaa, Sitta alisema, “Vielelezo vya Dk. Slaa ni vipeperushi vya mitandao.” Alidai hakuna wizi uliofanyika ndani ya BoT na kwamba Dk. Slaa alikuwa anatafuta umaarufu wa kisiasa.

Mfano mwingine ni pale Sitta alipoamuru kufungwa kwa mjadala wa kampuni ya kufua umeme ya Richmond bungeni kwa kuwa “serikali imetekeleza maazimo 21 kati ya 23 yaliyotolewa na bunge.”

Lakini baadaye alinukuliwa akisema, uamuzi wake wa kufunga mjadala huo, ulitokana na “tishio la kuvuliwa uanachama wa CCM.”

0
Your rating: None Average: 2 (2 votes)
Soma zaidi kuhusu: