Kuepuka akina Mba, tufuate Sabermetrics


Ezekiel Kamwaga's picture

Na Ezekiel Kamwaga - Imechapwa 01 December 2010

Printer-friendly version

SABERMETRICS ni jina geni katika ulimwengu wa michezo. Limekuwa likitumika zaidi nchini Marekani kuanzia miaka hii ya 2000.

Kwa kifupi, Sabermetrics huzungumzia zaidi takwimu za mambo yanayofanyika ndani ya uwanja kuliko yale ya nje ya uwanja. Kwa mfano, mtu unaweza kuzungumzia kuhusu idadi ya pasi, wingi wa mipira ya kurusha na umbali ambao wachezaji wamekimbia uwanjani.

Sabermetrics haizungumzi kuhusu idadi ya watu walioingia viwanjani kutazama mpira. Haizungumzii pia namna askari wanavyolinda uwanja. Ni mambo ya ndani ya uwanja tu.

Dhana hii ya Sabermetrics inaelezwa vizuri katika kitabu kipya cha Michael Lewis kiitwacho Moneyball. Kitabu hicho kinaeleza namna timu isiyo na uwezo kifedha inavyoweza kusajili wachezaji wazuri na kushindana na zile tajiri.

Kwa kutumia sayansi ya Sabermetrics, klabu husajili wachezaji wasiofahamika na wasio na gharama kubwa lakini wenye uwezo mkubwa wa kutekeleza majukumu yao.

Kwa maana hiyo, kwa kutumia sayansi hii klabu zinasajili wachezaji kwa kutazama takwimu muhimu za wachezaji ikiwamo mchango wao kwenye timu inaposhambuliwa na kushambulia.

Hii ndiyo maana Chelsea ilimsajili Claude Makelele kutoka Real Madrid kwa gharama nafuu lakini akaja kuwa nguzo muhimu ya klabu hiyo wakati wa Jose Mourinho.

Inaonekana sayansi hii bado haijafika Tanzania. Makocha na kamati za usajili nchini bado zinasajili wachezaji kwa njia ya “macho”. Kwamba kwa vile kocha ‘A’ alikuwa mcheza mpira mzuri zamani, basi ana uwezo wa kuona mchezaji mzuri mahali na kumsajili.

Hii ni njia ya kizamani sana ya kusajili wachezaji. Na ndiyo maana klabu zetu kubwa bado zinasajili wachezaji magarasa kila mwaka, tena kwa bei ghali.

Miaka miwili iliyopita, kwa mfano, Yanga ilimsajili mshambuliaji raia wa Cameroon, Robert Jama Mba, kwa gharama kubwa lakini akaishia kuwa kituko kwani mchezaji huyo hakufanya lolote.

Mara nyingi, suala la kusajili mchezaji hufanywa na mtu mmoja au kwa kumwona mchezaji katika mechi moja tu. Mfano mzuri ni usajili wa Simba uliofanyika hivi karibuni wa mshambuliaji wa Zanzibar Heroes, Ali Shiboli.

Hadi mwezi mmoja uliopita, hakuna hata kiongozi mmoja wa Simba au Yanga aliyezungumza kuhusu Shiboli. Baada ya kumwona kwenye mechi za kirafiki hivi karibuni tu, sasa Shiboli ameonekana lulu.

Kesho akijiunga na Simba na akianza kufanya vibaya, watu wataanza kulaumu. Badala ya kuangalia tatizo liko wapi, akina Godfrey Nyange “Kaburu” wataanza kumtafuta ‘Shiboli’ mwingine msimu ujao.

Wenzetu walioendelea kisoka wanafanya mambo makubwa matatu katika miaka hii wakati wanapotaka kusajili wachezani au mchezaji.

Kwanza wanasajili wachezaji wenye umri mdogo kwa lengo la kuja kuwapiga bei wanapokuwa wamekomaa na kukua kimchezo.

Hivi ndivyo Alex Ferguson alivyofanya kwa Cristiano Ronaldo na Arsene Wenger alivyofanya kwa akina Nicolas Anelka, Thierry Henry na Patrick Vieira. Unasajili mchezaji unamtengeneza, anasaidia timu yako na unamuuza kabla kiwango chake hakijaporomoka.

Njia ya pili ni kutengeneza wachezaji kama wanavyofanya Barcelona. Kwa kutumia kituo chao cha kukuza watoto kisoka cha La Masia, Barca ina uhakika wa kutengeneza vipaji vya miaka kumi ijayo.

Njia ya tatu ndiyo hii ya sasa ya kutumia Sabermetrics. Unamfuatilia mchezaji kwa muda mrefu ili ujue tabia yake, staili yake ya kucheza, mchango wake kwa timu na uwezo wake kwa ujumla.

Kwa mfano, Makelele alikuwa haonekani umuhimu wake kwa Real Madrid kwa vile kila mtu alikuwa akimzungumzia Zinedine Zidane, Luis Figo na Fernando Morientes.

Lakini kila mara takwimu zilikuwa zikionyesha kuwa Madrid ilikuwa ikishinda mara nyingi zaidi wakati Makelele anapocheza. Yeye ndiye aliyekuwa akikimbia zaidi, akikaba zaidi na akipora mipira zaidi kuliko mchezaji mwingine yeyote wa klabu hiyo.

Kwa hiyo, Chelsea ilikuwa ikitafuta mnyang’anya mipira na mkabaji katikati ya uwanja. Takwimu zikaonyesha hakuna zaidi ya Makelele, ikamchukua.

Lakini ilifanya utafiti kwanza. Utafiti pia ndiyo, kwa mfano, ungeweza kuisaidia Simba kujua mengi zaidi kuhusu Shiboli. Nani anamtengenezea nafasi? Staili ya ufundishaji ya Stewart Hall anayemfundisha Zanzibar Heroes inaendana na ya Patrick Phiri?

Hili ni muhimu kwa sababu kila mchezaji ana aina ya mchezo inayomsaidia kuliko nyingine. Kwa mfano, staili ya ufundishaji ya Rafael Benitez inamfaa zaidi Fernando Torres kuliko ile ya Roy Hodgson.

Kwa hiyo, Torres huyohuyo ambaye anaweza kuonekana mzuri akifundishwa na Benitez, anaweza kuonekana bomu chini ya Hodgson.

Inawezekana staili ya Phiri isiendane na ile ya Hall lakini makocha wazuri huwa tayari kubadili mfumo waliozoea ili kumfaidisha mchezaji muhimu. Swali ni kwamba, je Phiri yuko tayari kubadili mfumo uliompa ubingwa mwaka jana kwa ajili ya Shiboli?

Haya ndiyo mambo ambayo wenzetu huyafikiria kwanza kabla ya kufanya usajili wa wachezaji. Timu zetu huwa zinatumia siku moja tu ya mechi kusajili mchezaji.

Matokeo yake, timu za Tanzania zinaendelea kusajili wachezaji walioanza kuchoka kutoka nje ya nchi bila ya kujifunza kutokana na makosa ya zamani.

Makocha wa kigeni wanaokuja kufanya kazi nchini nao wamechangia sana katika hili. Wanasajili wachezaji wanaowajua wao na matokeo yake wanakuja kuonekana bomu baada ya muda mchache.

Ushauri wangu wa bure kwa klabu zetu ni kujitahidi kufuata mifumo ya kisasa wa kusajili wachezaji. Ikiwezekana ziajiri hata watafuta vipaji kwa ajili ya kuwatafutia wachezaji.

Kama Shiboli ameonekana baada ya mechi mbili tu, ina maana kuna vipaji vingi vilivyopo nchini ambavyo bado havijazinduliwa. Cha msingi ni kuvisaka hivyo vipaji kisayansi.

0
No votes yet