Kufeli huku ni kushindwa sera za CCM


M. M. Mwanakijiji's picture

Na M. M. Mwanakijiji - Imechapwa 15 February 2012

Printer-friendly version
Jamvi la Weledi

KARIBU nusu ya wanafunzi waliofanya mtihani wa kumaliza kidato cha nne mwaka jana wamefeli. Matokeo yameonyesha kuwa ni asilimia 53.59 tu ya wanafunzi waliofanya mtihani wa Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) ndio waliofaulu katika viwango mbalimbali.

Takwimu hizo pia zinaonyesha jambo jingine: Kati ya wale waliofaulu wavulana ni wengi zaidi kuliko wasichana.

Je, kufeli huku kuna maana gani? Jibu liko wazi: Sera ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuhusu elimu pamoja na kutumia mamilioni ya shilingi, imeshindwa.

Kumekuwepo na miradi mingi ya kila namna ya kuboresha elimu kuanzia elimu ya msingi na ya sekondari na hata elimu ya juu. Mipango hiyo mingi imekuwa ikiendana na mpango wa kupunguza umaskini na kukuza uchumi nchini (MKUKUTA) huku mipango hiyo ikijaribu kwa kiasi kikubwa kuendana na malengo ya maendeleo ya Milenia.

Kutokana na mipango hiyo yote na sera mbalimbali za elimu wanafunzi wengi zaidi wameingia shuleni (tukichukulia ongezeko la watu vile vile) na shule nyingi zimejengwa.

Hakuna shaka hata kidogo kuwa mipango yote hiyo imefeli na wakati wa kulikubali hilo umefika. Haitoshi tena kutafuta visingizio vya kujaribu kuelezea kwanini tumefelisha watoto wengi hivi.

Ingekuwa ni matokeo ya kidato cha nne tu ndio mabaya basi tungesema kuna tatizo kwenye elimu ya sekondari, lakini tumeona mambo haya haya kwenye elimu ya msingi na tumeyaona kwenye matokeo ya mitihani ya uhasibu na boharia na mitihani mingine.

Hata kwenye vyuo bado tuna wanafunzi wengi wanaofeli kwenye ngazi mbalimbali za elimu.

Hili lote linathibitisha kile ambacho wengine tumeshaanza kukiona na kukikubali kuwa ni kweli kwamba sera ya elimu ya Chama cha Mapinduzi na miundombinu inayotokana na sera hiyo imeshindwa!

Imeshindwa kuinua elimu, imeshindwa kuboresha elimu, na imeshindwa kutupatia wahitimu wenye weledi mkubwa katika masomo mbalimbali, kwani hawa ndio wanakuja kuwa wataalamu wa baadaye.

Hata wale wanaofaulu yawezekana kabisa wanafaulu katika mitihani lakini wakipewa nafasi ya kujieleza au kuelezea mambo mbalimbali wanapata shida sana. Tumeliona hili kwa baadhi ya wanafunzi wa vyuo vikuu wanapozungumza au kuhojiwa na nirahisi kuona jinsi ambavyo wanahangaika na ufundi wa kujieleza. Siyo kwamba hawafahamu bali hawajaandaliwa kuwa wenye umahiri katika kujieleza na kuchambua mambo. Ni wachache wa hawa ambao wamekubuhu wakichanganya na vipaji vyao ndio wanang’ara kwelikweli.

Tatizo ni nini?

Sitajaribu kwa makala hii fupi kujibu swali hili kwani ninaamini ni utafiti wa kisayansi unaweza kutuonyesha liliko tatizo. Ninachoweza kufanya hata hivyo, ni kujaribu kuuliza maswali ambayo naamini kwa kiasi chake yanaweza kuchochea watafiti wetu kututafutia majibu.

Kwenye siasa ninaamini ni kujidanganya kufikiria kuwa CCM inaweza kuja na sera ambazo zitaboresha elimu. Kuangalia CCM au serikali inayotokana nayo kutafuta majibu ya tatizo la elimu ni kujidanganya. Wakati umefika kuanza kuangalia nje ya CCM na serikali yake kutafuta majibu.

Mazingira ya elimu yakoje?

Ukisikia na kusoma habari za ufujaji mkubwa wa fedha za umma na matumizi ya wizi ya baadhi ya taasisi zetu ni vigumu kuelewa kwanini bado kuna shule hata moja Tanzania ambayo watoto wake wanakaa chini. Hata kwenye shule ambazo wanafunzi hawakai chini bado mazingira ya elimu hayafai kwa kutolea elimu (the environment is not conducive for education to take place). Maana yake ni kuwa elimu siyo tu kile kinachofundishwa – kitu ambacho kimekuwa ni msisitizo wa utawala wa sasa – bali hata mahali na mazingira ambapo elimu hutolewa.

Hivi mtoto ambaye anapofika shule kitu cha kwanza ni kutafuta tofali la kukalia au kutafuta mahali pazuri ili asipigwe na baridi ataweza vipi kujifunza vizuri? Hivi mtoto ambaye anafika shule akiwa na njaa anaweza vipi kujali kinachotokea darasani? Hivi mtoto ambaye anapojitahidi kusoma kuna watu mafataki wanamsarandia anaweza vipi kutuliza akili kusoma? Hivi, mwalimu ambaye hajalipwa madeni yake anaweza vipi kukaa darasani kufundisha huku nyumba yake inavuja? (kama anayo hiyo nyumba!).

Wanaofundisha ni kina nani?

Mojawapo ya maswali yangu ya ugomvi ni hili la wanaofundisha kwenye hizi shule ni kina nani? Nchini Marekani karibu walimu wote wanaofundisha sekondari (Junior High na High School) ni walimu wenye shahada ya elimu (B.A/BS Ed). Katika sera ya CCM ya kuongeza walimu tukabadilisha hadi kuwa na kile kinachoitwa “walimu wa voda faster” yaani watu waliopewa mafunzo ya ualimu ya haraka haraka ili wakafundishe kwenye shule za kata – kwani walipoamua kujenga shule nyingi za kata hawakuwa na walimu wa kutosha!  Sera mbovu zilizoshindwa!

Sasa, tunaweza kuwa na sera yenye kuhakikisha kuwa siyo tu kwenye elimu ya sekondari tunakuwa na walimu wenye shahada lakini hadi kwenye elimu ya msingi? Itakuwaje kama hadi kwenye shule za awali za chekechea tunakuwa na walimu wenye shahada siyo tu wale wenye kufundisha kusoma na kuandika kwa vile na wao wanajua kusoma na kuandika?  Je, walimu hawa wa sasa wanapewa mafunzo kiasi gani kuinua uwezo wao? Je, kuna utaratibu gani wa kupatiwa kozi fupi fupi za kuwaboresha na kuwajaribu  walimu hawa? Je, walimu nao wanaweza kupewa leseni za kufundisha – siyo shahada au stashahada tu. Je, tunaweza kuweka utaratibu kuwa kila mwaka kila mwalimu ni lazima ajaribiwe kuonekana yuko bado na uwezo wa kufundisha kwa kujua mambo ya sasa na hivyo kuendelea kuwa na leseni yake? Yaani kuwa na utaratibu kama ulioko kwa madaktari na wanasheria?

Kuna baadhi ya watu wameona matokeo haya ni kama kitu cha kuchekesha. Wengine wameona ni matokeo ya udini na wengine wamebakia kukicheka kizazi cha “bongo flava”. Waliniudhi baadhi ya watangazaji ambao walilijadili hili kama kitu cha kuchekesha kupiga muziki wa Bruno Mars wa “Today I don’t feel like doing anything” wakidhani ni jambo la kuchekesha. Ndugu zangu, suala la elimu sasa ni janga la kitaifa, si mchezo, si utani! Ni janga linalotokana na kujaribu na kufeli vibaya, kutekeleza sera zilizoshindwa za CCM. Matokeo haya mabaya hayajaletwa na shetani, mapepo au vidudumtu; ni matokeo ya sera mbovu!

Cha kushangaza bado watu wanaangalia kwenye CCM kutafuta majibu! Watu hawa hawa ambao watoto wao na wadogo zao wamefanya vibaya ndio hawa hawa utawaona wamevaa magwanda ya kijani na nyeusi wakishangilia “nambari wani eeeh, nambari wani CCM!” Yaani hawahusishi kabisa matokeo mabaya ya elimu ya watoto wao na utawala ulioko madarakani!

Tuna kazi! Ati tunacheka!

mwanakijiji@jamiiforums.com
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: