Kujiuzulu hakutoshi


editor's picture

Na editor - Imechapwa 22 April 2008

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

WAZIRI wa Miundombinu, Andrew Chenge amejiuzulu. Inajulikana kilichomsukuma hadi kuchukua hatua hiyo, ni tuhuma za kujilimbikizia utajiri kwa njia zisizofaa.

Chenge amefanya uamuzi wa maana ingawa amechelewa. Alitarajiwa kujiuzulu mara tu alipotangazwa kama mmoja wa viongozi 11 waandamizi serikalini na wafanyabiashara watafuna nchi.

Kama pale hapakuwa mahali bora pa kujiuzulu, basi angefanya hivyo pale alipobaini kwamba anachunguzwa na makachero wa Uingereza kuhusiana na kupokea mlungula kwa lengo la kufanikisha ununuzi wa rada mwaka 2002.

Angalau angejiuzulu baada ya kuwasili nchini akitokea ziarani China. Katika uwanja wa ndege wa Mwalimu JK Nyerere, Dar es Salaam, umma ulikusanyika ukitaka kufahamu kutoka kwake amepataje utajiri unaotajwa kuwa nao.

Hakujali yote hayo, alisubiri mpaka wateuzi wake wa Ikulu wamwamuru. Ndipo akautema uwaziri. Tunampongeza kwa kuamua.

Hatua yake ya kujiuzulu ni mfululizo wa matokeo ya harakati za kupinga ufisadi miongoni mwa viongozi wa serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Ni harakati hizihizi zilizowaondoa Februari mwaka huu, Edward Lowassa, aliyekuwa Waziri Mkuu, Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi na mtangulizi wake katika wizara hiyo, Dk. Ibrahim Msabaha.

Hawa walijiuzulu baada ya kushiriki, ama kunyamazia kufanikisha mkataba wa kufufua umeme wa dharula kati ya serikali na kampuni ya Richmond.

Hakika, wapo mafisadi wengi waliotajwa katika orodha hiyo ambao hawajaondoka. Wapo wengine ambao hawajatajwa, lakini wanahusika katika kutafuta nchi.

Wote hao, tunawataka waondoke haraka katika utumishi wa umma bila kujali madaraka yao.

Lakini lipo tatizo jingine. Kwamba waliojiuzulu uwaziri, wanaendelea kubaki na ubunge na nafasi nyingine za uongozi katika chama. Baadhi yao wanaendelea kuwa wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM.

Bunge na NEC ya chama tawala, ni taasisi nyeti na zenye uwakilishi mpana. Hizi si taasisi zisizopaswa kukaliwa na watu wachafu. Ni vema huko nako wakang'atuka.

Aliyemo humo anatumikia umma vilevile. Haiingii akilini kiongozi kujiuzulu uwaziri akabaki mbunge au akaendelea kuwa mjumbe wa NEC. Hilo haliwezekani.

Tunakubaliana na wito wa wananchi wa Bariadi Magharibi, kutaka Chenge aachie ubunge wao. Tunataka pia kuona akina Lowassa, Karamagi, Dk. Msabaha na wengineo waliokosa uwaziri, lakini wamebaki na wabunge au nafasi nyingine za utumishi wa umma wakijiuzulu.

Kuendelea kutumikia taasisi zinazotoa maamuzi yanayogusa maslahi ya Watanzania na taifa, hakujengi utamaduni wa kuridhia matakwa ya umma na yale ya wakati.

Kwa mfano, Chenge, Lowassa na Karamagi, ni wajumbe wa NEC ya CCM. Unaacha uwaziri katika serikali, lakini unaendelea kubaki mjumbe wa NEC ya chama kilekile kinachoendesha serikali.

Tunasema wazi kujiuzulu hakutoshi. Umma unasubiri hatua zaidi kuchukuliwa kwa wale wenye tuhuma za moja kwa moja za kuifisidi nchi. Hatutaki ubaguzi katika kushughulikia watuhumiwa. Taifa hili halina aliye juu ya sheria.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: