Kumbe CCM ni chui wa karatasi?


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 01 September 2010

Printer-friendly version
Tafakuri

KWANZA alianza Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Pius Msekwa, Julai mwaka huu, Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ilipomuomba na kupendekeza Katibu Mkuu wake, Dk. Willibrod Slaa, agombee urais.

Msekwa alilalamika kuwa wanakwenda kuwasilisha malalamiko yao Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwamba wakati kampeni za urais kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 hazijaanza, Dk. Slaa alishaanza kampeni.

Nini ilikuwa kisa cha malalamiko ya CCM? Eti Dk. Slaa alikuwa anatembelea maeneo mbalimbali nchini, huku akihutubia maelfu ya wananchi.

Kwa Mzee Msekwa, CHADEMA walikuwa wameanza kampeni mapema. Baadaye NEC ilitoa kauli ikivitaka vyama kuzingatia taratibu na sheria, ingawa kimsingi NEC inawajibika katika ulingo wa kisiasa pale tu kampeni rasmi zinapoanza.

Wakati Mzee Msekwa akilalamikia CHADEMA, alikuwa amevaa pengine miwani ya mbao iliyomzuia kuona kwamba mgombea wao, Rais Jakaya Kikwete, alikuwa ameitisha mikutano inayofanana na ya Dk. Slaa mkoani Dodoma na Dar es Salaam.

Wakati huo pia walisahau kwamba tayari walishamwaga mitaani fulana nyingi zenye picha ya mgombea wao huyo. Kulikuwa na khanga na mabango ya namna hiyo.
Vyote hivyo – fulana, khanga na mabango – vilikuwa vinahamasisha mgombea wao awe na mvuto kwa wapiga kura.

Hiyo kwa Mzee Msekwa haikuwa kampeni wala si suala la kuhojiwa kokote, wao wana haki ya kuendesha siasa watakavyo, lakini si vyama vingine, vikifanya hivyo ni sawa na uhaini.

Haikubaliki!

Hofu ileile ya Mzee Msekwa, juzi Jumapili ikaonyeshwa tena na Mwenyekiti wa Kamati ya kampeni ya mgombea urais wa CCM, Abdulrahman Kinana, ambaye alikutana na waandishi wa habari na kutuhumu CHADEMA kuwa wamevunja maadili ya uchaguzi ambayo vyama vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi vilikubaliana kuyafuata na kuyatii.

Kinana anayedaiwa alisafiri kutoka Kigoma kuja Dar es Salaam kufanya mkutano huo kujibu mapigo ya CHADEMA ambayo yalitolewa Jumamosi iliyopita wakati wa uzinduzi wa kampeni zake kitaifa, alisema CHADEMA kilitumia mkutano huo kueneza uongo, na kuwakashifu viongozi waandamizi wa CCM.

Kinana hakuishia hapo na hofu yake tu, kwani pia alienda mbali zaidi kwa kusema kwamba watalalamikia rafu zilizochezwa na CHADEMA kwa NEC kwa kuwa wanaamini haikuwa hahali kwa makada wa CHADEMA kutumia jukwaa lao kuwaandama makada wa CCM.

Kwa bahati nzuri mkutano wa CHADEMA kama ulivyokuwa wa Chama cha Wananchi (CUF) siku iliyotangulia, na CCM, yote ya uzinduzi iliyofanyika jijini Dar es Salaam lakini kwa siku tofauti, ilionyeshwa moja kwa moja na kituo cha Televisheni cha Taifa (TBC1).

Kwa maana hiyo, watu wengi waliofika viwanja vya Jangwani na wale waliobaki majumbani waliweza kufuatilia kwenye luninga zao juu ya kile kilichojiri.
Hadi sasa imekuwa ni vigumu mno kusema hiyo kashfa inayosemwa na Kinana na kama ambavyo juzi, Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba, naye aliibuka kuzungumzia ni nini hasa?

Swali gumu na ambalo inabidi liwekwe sawa na makada hawa ni hili, hivi mtu akisema fulani na fulani ndio waasisi wa EPA anakuwa ametenda kosa gani kama ana ushahidi wa kuthibitisha hayo?

Na kwa nini taharuki yote hii, leo mkutano wa waandishi wa habari ufanywe na Kinana, kesho ufanywe na Makamba, lakini wote wakizungumzia jambo hilo hilo moja? Nini kimetokea kwa chama kikubwa kama CCM? Taharuki ya nini?

Tuingie kwa undani zaidi katika sakata hili, nani asiyejua kwamba suala la sakata la EPA yaani ile kashfa ya kukwapuliwa kwa zaidi ya Sh. 133 bilioni kutoka Akaunti ya Madeni ya Nje ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) iliasisiwa mahususi kuisaidia CCM?

Je, Mabere Marando, mwanasheria na wakili mahiri na mwanasiasa muasisi wa vyama vingi nchini, aweza kuitwa baba wa mageuzi, si ni wakili wa baadhi ya washitakiwa wa EPA? Je, Kinana na Makamba hawajui kwamba ana ushahidi wa nyaraka kuhusu kashfa hiyo?

Kama wanajua, ni vema basi CCM wakatulia na wasimchokonoe pweza, lakini kama hawajui, basi wasiishie kwenda kushitaki Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) tu. Bora waende mahakamani ili ukweli ujulikane kwa kuwa haki hupatikana mahakamani na si NEC.

Kwa muda mrefu kumekuwa na juhudi zinazofanywa ama na watawala au wale waliokaribu na watawala ambao wananufaika na mfumo wa kulindana uliopo kuona kwamba sakata la EPA linafikia mwisho bila vigogo hawa walioliasisi wakiguswa.

Ni kwa maana hiyo kauli za akina Kinana na Makamba kwamba eti kuna kashfa iliyotamkwa Jangwani Jumamosi ni utani mbaya unaostahili kupuuzwa hadi hapo mapapa wa kampuni ya kifisadi ya Kagoda Agriculture Limited iliyothibitishwa kuchota Sh. 40 bilioni katika kashfa ya EPA watakapoonja mkono wa sheria.

Lakini la msingi zaidi ni kuhoji mbinu hizi za akina Kinana na Makamba za kutaka watu wanyamaze kuhusu kashfa zilizoifilisi nchi zinalenga kumkomboa nani?

Tunajiuliza swali hili kwa sababu kilichozungumzwa Jangwani kinahusu ukombozi wa rasilimali za umma, ili zifanye kazi ya kuwaondoa kwenye umasikini wananchi wote.

Ni vema Kinana na Mkamba pamoja na wenzao wakaelewa kuwa unaweza kudanganya watu kwa kitambo lakini hakika huwezi kuwadanganya watu wote wakati wote.

Ni kwa maana hiyo maswali magumu kama ya EPA yakapewa majibu stahili yanayofanana na kashfa hiyo, lakini kilio cha kuwaita waandishi wa habari na kujaribu kurubuni umma ili uwe na huruma na vitendo vya wizi vinavyofanywa mchana kweupe na wale walioaminiwa na kukabidhiwa ofisi za umma, hakitavusha taifa.

Juhudi za kina Makamba na Kinana zinasaidia zaidi umma kuamini kwamba ukubwa wa CCM si lolote. Kumbe ni chama dhaifu na kinachotegemea huruma ili kifunike maovu yake.

Mbinu hizi zimeshindwa ndiyo maana kinatakiwa sasa kujiondoa hapo na kujitokeza hadharani kujibu tuhuma zake, kwamba ni kwa jinsi gani kilinufaika na EPA, vinginevyo hii ni kansa itakayoitafuna milele.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: