Kumbe JK angeweza kuzuia mgomo? 


M. M. Mwanakijiji's picture

Na M. M. Mwanakijiji - Imechapwa 14 March 2012

Printer-friendly version

MGOMO wa madaktari uliokuwa umeanza ngwe yake ya pili umemalizwa baada ya mazungumzo ya saa chache kati yao na Rais Jakaya Kikwete Ikulu jijini Dar es Salaam Ijumaa iliyopita.

Mazungumzo hayo yalisababisha madaktari kukutana siku ya Jumamosi na kutoa tamko la kusitisha mgomo wao, huku wakituma ujumbe mkali kwa serikali.

Kusitishwa kwa mgomo kumetokana na hatua ya Rais Kikwete kuahirisha kukutana na wazee wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani wa Dar es Salaam na badala yake akakutana na uongozi wa madaktari.

Kwa baadhi ya watu wanaona uamuzi wa Rais kuingilia kati ni wa kupongezwa na unaonesha alivyo na ushawishi. Hakuna aliyewahi kwenda Ikulu kuzungumza naye akarudi bila “kulainika!”

Hivyo, bila shaka ni rahisi sana kuamini kuwa mgomo wa madaktari ungeweza kuzuiwa kuanza kama Rais Kikwete angeamua kuingilia kati na kuwasikiliza madaktari mapema.

Mgomo wa juzi ni matokeo ya mgomo wa awali uliodumu kwa wiki mbili hivi hadi wanaharakati walipoanza kuingia mitaani ndipo hatimaye Waziri Mkuu Mizengo Pinda akaona hana jinsi isipokuwa kuwabembeleza madaktari warudi kazini.

Walirudi kazini kwa masharti kwamba mambo fulani yawe yameonekana kutekelezwa ndani ya wiki tatu, vinginevyo wangeendeleza mgomo. Kimsingi ule wa kwanza uliahirishwa tu ili kuipa serikali nafasi.

Sasa mgomo ulipoanza ngwe ya pili wengine tulitarajia labda Kikwete angeingilia kati lakini hatukuwa na matumaini sana kwani kama hakuzuia mwanzoni ni kipi kingemsukuma kuingilia kati safari hii.

Na kweli. Karibu siku tatu zilikuwa zimeyoyoma ndipo akiwa amepata mwanga fulani akaamua kukaa na madaktari na kweli baada ya saa chache akafanikiwa kusitisha mgomo ili apate nafasi ya kushughulikia matatizo mengine.

Lakini kwanini Rais Kikwete hakuzuia mgomo huo kuanza? Hili linaweza kuwa miongoni mwa maswali magumu kuyapatia majibu.

Kama Rais aliweza kuingilia kati mgomo wa pili tena siku ya tatu ni kwanini hakuweza kuingilia kati mgomo wa kwanza siku ya kwanza?  

Majibu mbalimbali yanaweza kutolewa. Moja, Rais Kikwete alikuwa na safari ya kwenda Davos nchini Uswisi kuhudhuria mkutano na nchi tajiri na hivyo asingeweza kushughulikia mgomo huu. Mgomo ulipoanza na mkutano wa Davos nao ulikuwa unaanza.

Hata hivyo, jawabu hili si zuri sana kwani jirani zetu Kenya hawakumpeleka rais wao Davos bali aliyekwenda huko ni Raila Odinga ambaye ni Waziri Mkuu.

Nigeria walimpeleka waziri wao wa fedha. 

Je, chini ya tishio la mgomo Rais Kikwete angeweza kukaa chini na madaktari na badala yake kumtuma makamu wa rais au waziri mkuu ili kuhakikisha kuwa mgomo hautokei?

Pili, Kikwete aliwategemea wasaidizi wake kumaliza tatizo la mgomo lakini walimuangusha. Hili nalo laweza kuwa ni jibu zuri, lakini pia lina matatizo.

Hivi ni kwa mara ngapi tunaweza kuwalalamikia “wasaidizi” wake? Ikumbukwe kuwa sehemu kubwa ya mgomo imetokana na kulalamikwa kwa wasaidizi hao – kwenye hili ni waziri wa afya, naibu wake, katibu mkuu na mganga mkuu.

Sasa ni kwa vipi watu ambao wanahusishwa na mgomo wenyewe kuangaliwa kama watakaoweza kuutafutia suluhu? Na wale wanaoitwa “wasaidizi” si walikuwepo hata kabla ya mgomo?

Hadi madaktari wanaamua kutangaza mgomo maana yake ni kuwa juhudi zote za kupitia wasaidizi zilikuwa zimeshindikana? Kama tayari wasaidizi wameshashindwa ni kwa vipi tunawaangalia wao? 

Tatu, waziri mkuu Pinda angeweza kumaliza mgomo na hivyo haikumhitaji rais kubaki nchini kufanya kazi hiyo. Ni wazi sasa tunajua kuwa waziri mkuu hakuweza kuumaliza mgomo. 

Kuanzia tishio lake la kuwafukuza kazi madaktari na baadaye ahadi yake kuwa Rais angeweza kuwashughulikia mawaziri.

Kwa kweli Pinda hakuwa mtu sahihi kuuzuia kuanza au kuendelea kwa mgomo kwa sababu moja kubwa – hana uwezo wa kumwajibisha waziri yeyote au kumfukuza kazi kiongozi anayeteuliwa na Rais!

Hili limeonesha mojawapo ya udhaifu mkubwa wa Katiba iliyopo. Waziri mkuu wa Tanzania haundi baraza la mawaziri – yaani hateui hata mtu mmoja kuwa waziri au naibu na hivyo hawezi kumwajibisha waziri au naibu waziri hata mmoja.

Jambo lolote la kinidhamu iwe utendaji au vinginevyo ni lazima alipeleke kwa rais. Na hivyo ndivyo alivyofanya kwenye suala la David Jairo na hata kwenye suala la Waziri Hadji Mponda na naibu wake, Dk. Lucy Nkya.

Sasa kama hakuwa na hana uwezo wa kumwajibisha waziri yeyote ni kwa vipi ilitarajiwa angeweza kuwaridhisha madaktari ambao kubwa la malalamiko yao ilikuwa ni utendaji wa wateuliwa wa rais?

Wapo wanaoweza kusema siyo kila kitu kinamhitaji rais kila wakati; kama mawaziri na viongozi wengine wangefanya kazi zao wala mgomo usingeenda mbali hivyo.

Hii yawezekana kuwa ni kweli lakini ni ukweli nusu. Kuna vitu ambavyo ni rais pekee anayeweza kuvifanya – kwa lugha ya kigeni inaitwa “presidential prerogatives” – katika hili la mgomo, ni rais pekee ambaye angeweza kulimaliza kutokana na msingi halisi wa madai yenyewe.

Niliandika hili huko nyuma na kumsihi Rais Kikwete kuingilia kati kwa sababu niliamini kuwa madai ya madaktari ni mazito mno kiasi kwamba siyo waziri mkuu au mtu mwingine anayeweza kuyamaliza. Leo imethibitika.

Lakini wapo wanaosema Rais hawezi kufanya kazi kwa mashinikizo. Hili ni mojawapo ya hoja zisizo na mashiko kabisa. Kama kwenye demokrasia wananchi hawawezi kuishinikiza serikali yao – hata kwa migomo na maandamano kama hoja za kawaida zimeshindwa – ni wapi sasa itafanyika hivyo?

Wananchi wanapochagua viongozi hawanyang’anywi haki yao ya kuishinikiza serikali; serikali isiyopewa mashinikizo itawatala watu ipendavyo! Rais au kiongozi yeyote akitaka aepuke kushinikizwa ni lazima awe wa kwanza katika kushughulikia malalamiko ya wananchi, si kuyaatamia hadi yatotoe migomo!

Ndugu zangu tukumbuke kuwa kilichositishwa ni mgomo wenyewe, lakini vyanzo vya ule mgomo bado vipo.

kilichoondolewa ni moshi tu, lakini siyo makaa ya moto. Kwa mtu aliyesoma tamko la madaktari tunaweza kuona ujumbe mkali kabisa kwa serikali na ni matumaini yangu ujumbe huo umefika.

Ni matumaini yangu – na labda ya Watanzania wengine – kuwa Rais Kikwete hatokaa tena pembeni wakati wananchi waliompigia kura na kumuajiri wanaangamia. 

Ndiyo maana bado najiuliza: Kwa nini Rais Kikwete hakuingilia mgomo huu mapema kabla ya kuanza na kuhakikisha hauanzi; na kwanini ulipoanza hakutumia muda wake mfupi kukutana na madaktari kujaribu kuumaliza?

Binafsi sina jibu la swali hili. Inawezekana wengine wanalo!

mwanakijiji@jamiiforums.com
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: