Kumbe kustaafu ni mchezo wa kuigiza tu


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 23 February 2011

Printer-friendly version
Kalamu ya Jabir

YUSSUF Omar Chunda, mtangazaji wa zamani wa redio, anakumbuka alivyoandaliwa sherehe nzito na wafanyakazi wa Sauti ya Tanzania Zanzibar (STZ) alipostaafu utumishi wa serikali mwishoni mwa mwaka jana.

Hadi leo anaitizama picha aliyopigwa akipokea televisheni ambayo ilikuwa moja ya zawadi alizopewa na wafanyakazi wa STZ wakati wakimuaga na kumtakia kheri na fanaka katika maisha mapya.

Wakati sherehe ikirindima, Chunda ambaye pia ni mpenzi mkubwa wa mpira wa miguu aliyewahi kuwa mmoja wa viongozi wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) tangu enzi kikiitwa IFOZA – Idara ya Futiboli Zanzibar, alikuwa ameshapokea hundi ya fedha za mafao ya kumaliza kutumikia serikali.

Katika uteuzi mpya alioufanya Dk. Ali Mohamed Shein wiki iliyopita kuzihusu wizara tatu, aliigusa pia Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, jina la Chunda lilitajwa kama mkurugenzi mpya wa Idara ya Habari Zanzibar (Maelezo).

Kumbe siku hizi kustaafu ni mchezo wa kuigiza. Wale wanaorudishwa hawalaumiki. Tatizo ni anayewateua. Baadhi ya wastaafu wana wajukuu ambao wanahitaji kazi sasa baada ya kumaliza masomo. Watazipataje wakati babu na bibi zao wanang’ang’anizwa kubaki serikalini?

Mstaafu mwingine aliyerudishwa baada ya kutimiza umri wa kutumikia serikali ni Sufiani Khamis Juma, mhandisi wa mitambo aliyeteuliwa Mkurugenzi wa Televisheni ya Zanzibar (TVZ).

Huyu naye alistaafu na kupokea mafao baada ya kutumikia serikali kwa mujibu wa sheria.

Alipostaafu alitafuta kazi na kubahatika kuajiriwa Chuo Kikuu cha Mzumbe, mkoani Morogoro. Kinyume na matarajio yake, alipigiwa simu na Ikulu ya Zanzibar na kutakiwa kupokea uteuzi huo.

Zipo taarifa kwamba alipigiwa simu na Dk. Shein mwenyewe na kushawishiwa arudi na kushika nafasi mpya katika kituo ambacho alikitumikia kwa sehemu kubwa ya maisha yake kama fundi mkuu na aliwahi kuwa mkurugenzi wake.

Sufiani anarudishwa serikalini na kukabidhiwa kituo ambacho baada ya kuanzishwa kama kituo cha kwanza cha televisheni ya rangi Afrika Mashariki na kutamba kwa hazina ya waandishi hodari na mitambo ya kisasa, siku hizi ni majengo yanayotumika kuchekesha.

Wakati kituo cha Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC1) chini ya Serikali ya Muungano kilichoanzishwa miaka ya mwisho ya 1990 kikianzia na Televisheni ya Taifa (TvT) sasa kinavuma kwa kwenda na wakati kiurushaji matangazo yake kupitia mfumo wa digitali, siku hizi kuangalia TVZ ni kama karaha.

Mitambo yake imechakaa, waandishi wake mahiri wamekata tamaa, na wapiga picha wake wengi wajuzi wamehamia kwenye vituo vingine. Siku hizi kupitia TVZ ni jambo la kawaida kujikuta unaletewa kitu tofauti na kile ambacho mtangazaji alikutayarisha kukiona. Itachukua miaka kadhaa kabla ya kugeuza mfumo wa utangazaji kuwa wa digitali.

Hiki ni kituo ambacho kimepata wakurugenzi wanne na mawaziri kadhaa ndani ya miaka 20 lakini kadiri siku zinavyokwenda, kinazidi kushuka hadhi kihabari. Wala wafanyakazi wake hawalaumiki. Kwa kweli wanajitahidi kuwapatia wananchi kile wanachomudu kukitoa kwani hawapati msaada wa maana kwa serikali.

Kwanza bado wakuu wa serikali hawajataka kukiachia kifanye kazi kitaalamu. Inawezekana hawatoi maelekezo kwa kila kitu, lakini kwa sababu ya mfumo wa kukidhibiti katika utendaji wake kujengeka, wahariri wake na waandishi wanaepuka lawama na kwa hivyo wanachokifanya ni lazima kiwe kinachofurahisha Chama Cha Mapinduzi (CCM) na viongozi wake.

TVZ kama ilivyo Sauti ya Tanzania Zanzibar inasifika Zanzibar na duniani kote kwa kuipendelea CCM wakati wa uchaguzi mkuu, licha ya maelekezo ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) na wafadhili kukihimiza kutoa nafasi sawa kwa vyama vyote vya siasa kwa kuwa ni kituo kinachoendeshwa kwa kodi za wananchi.

Kinachosemwa na kiongozi wa chini wa CCM kitapewa nafasi zaidi TVZ kuliko tukio lililomhusisha katibu mkuu wa wizara au linaloonyesha shida za kimaisha zinazokabili wananchi. Mara kadhaa TVZ imeshindwa kutoa taarifa ambazo waandishi wake wamezishuhudia sambamba na waandishi wa vyombo vingine vya habari.

Mawaziri waliopita wa habari, akiwemo Ali Juma Shamhuna aliyesimamia sekta ya habari ya serikali wakati ikiwa chini ya Ofisi ya Waziri Kiongozi, walikitumia kituo hicho kwa maslahi yao na chama chao huku wakidharau umuhimu wa kuimarisha maslahi wafanyakazi.

Kutokana na dharau ya viongozi kwa wafanyakazi, TVZ imejikuta ikipoteza vipaji vya kiuandishi, utayarishaji vipindi, utangazaji na upigaji picha wakiwemo wale walioacha majina walipoondoka TVZ.

Kwa mfano, Marin Hassan Marin ambaye sasa anatamba akiwa TBC1, alikuwa injini muhimu alipokuwa TVZ alikohamishiwa baada ya kulazimishwa kuondoka STZ kwa sababu za kisiasa, alianzisha vipindi kadhaa ambavyo sasa havipo au vinachechemea katika utokaji wake.

Nitaje kipindi cha Mawio alipokuwa STZ na TVZ Doctor alipokuwa TVZ. Mawio ni kipindi  cha mkusanyiko wa habari na matukio. Hiki sasa kinarekodiwa mchana kweupe kwa ajili ya kutoka asubuhi ya siku inayofuata. Ni kinyume kabisa na asili yake pale kilipoanzishwa na Marine. Alikuwa akiwezesha taarifa motomoto kutoka huku baadhi yake zikipatiwa ufafanuzi wa papo kwa papo na viongozi wahusika waliokuwa wakipigiwa simu kuelezea msimamo wao kuhusu jambo fulani.

Hata sasa, TVZ hawana muundo wa utumishi unaohalalisha viwango vyao vya mishahara na madaraja ya kikazi. Bado TVZ inategemea habari za kupewa ndani ya serikali na CCM kuliko zile ambazo waandishi wake wanazihangaikia. Kwa hakika, waandishi wake, kama walivyo wa STZ, hata wakipeleka habari, zinalazimika kusubiri kwanza zile zilizotoka kwa wakubwa.

Ninalenga kubainisha kuwa TVZ inahitaji mapinduzi ya kweli ili kuridhisha wananchi kama kweli ni kituo cha serikali yao. Inahitaji kiongozi madhubuti mwenye ubavu wa kumkabili rais, achilia mbali waziri, ili kukiwezesha kutosheleza matumaini ya wananchi.

Katika wakati wake, Chunda aliyeishi STZ kwa miaka mingi, STZ haikujijenga kama kituo cha umma kweli. Ameiacha hivyo huku wafanyakazi wake wakiwa taabani kimaslahi na kitaaluma. Hivi amestaafu, wafanyakazi wa STZ wanajilipia masomo ya kitaaluma wakati ni waajiriwa wa kudumu. Walipoomba kusaidiwa, waliambiwa, “Idara haina pesa za kusomesha wafanyakazi.”

Angalau STZ imepata mkurugenzi anayeaminika. Rafii Haji Makame ni msomi na mjuzi wa fani. Amekuwa katika Tume ya Utangazaji Zanzibar na anajulikana alivyo mchapa kazi na mpenda wafanyakazi. Anaweza kuleta mapinduzi yanayotakiwa na wakati; vinginevyo STZ itabaki kusikilizwa tu wakati wa matangazo ya vifo kama ilivyozoeleka kwa miaka mingi sasa.

Taasisi zote hizi mbili hazina vitendea kazi vya kisasa. Hazina usafiri wa uhakika, zaidi ya gari chache wanazotumia wakurugenzi. Kuzibadilisha kunahitaji viongozi wakali na wanaofuatilia majukumu kwa kuwa bado ndani ya serikali kuna viongozi waandamizi hawajaamini kama Zanzibar inafuata imebadilika.

Na hayo ndiyo changamoto kubwa zinazomkabili Abdilahi Jihad Hassan, waziri mpya wa habari, utamaduni, utalii na michezo kutoka Chama cha Wananchi (CUF).

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: