Kumbe Pinda naye ana usanii


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 24 February 2010

Printer-friendly version
Tafakuri
WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda

WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Tabora mwishoni mwa wiki, alitoa kauli yenye utata alipokuwa kwenye jimbo la Igunga, ambalo mbunge wake ni Rostam Aziz.

Pinda aliwataka wananchi wa jimbo hilo wasimuhukumu Rostam kwa ‘maneno ya bungeni’ badala yake wamuhukumu katika uchaguzi mkuu ujao kwa kazi alizowafanyia kama mbunge.

Pinda alikuwa akirejea maendeleo ambayo yamepatikana katika jimbo la Igunga, Rostam akiwa mbunge wake. Itakumbukwa kwamba Rostam aliingia bungeni tangu mwaka 1994 kwenye uchaguzi mdogo wa jimbo hilo.

Tangu wakati huo, ameshinda uchaguzi mara nne, yaani 1994, 1995, 2000 na 2005. Kwa vigezo vyote ni mbunge mkongwe katika siasa za Tanzania.

Ni kweli kabisa Rostam huenda ametekeleza kwa nguvu zake zote ilani ya CCM ya uchaguzi; yawezekana amesaidia jamii yake kutoka katika ngazi ya umasikini sana hadi hali yenye nafuu; pia yawezekana kuwa kwa macho ya Pinda, alimradi maendeleo yamepatikana, basi mtu asijadiliwe kwa mambo mengine yoyote.

Huu ni msimamo wa Pinda na kwa kweli kuna kila sababu ya kumuhukumu kwa huo. Lakini kauli ya Pinda inatoa picha moja nzuri au mbaya kuhusu Bunge, kwamba ni mahali watu wanafikia kwa ajili ya kulumbana, hakuna tija, ni kitovu cha magomvi na misuguano isiyokwisha.

Kwa kauli ya Pinda kwamba ‘maneno ya bungeni’ si hoja ya kumpima Rostam ni sawa na kusema kwamba mikutano 20 ya Bunge kila miaka mitano ni upotevu wa rasilimali za wananchi bure; ni kushiriki vikao vya kusigana lakini ambavyo havina tija.

Kwa upeo wangu naamini kwa yakini kabisa kwamba Pinda amepotoka, tena sana.

Nitafafanua. Kwanza Pinda katoa majibu ya jumla jumla kuhusu maneno ya bungeni wakati alipaswa kujua kwamba ndiyo yalimfikisha kwenye nafasi aliyonayo; kwa maneno mengine bila maneno ya Richmond, Pinda leo hii asingekuwa waziri mkuu.

Kwa muda mrefu sasa kumekuwa na juhudi za makusudi kutoka kwa watu hasa wenye nyadhifa serikalini na kwenye chama tawala, kukejeli na kubeza sakata la Richmond kana kwamba lilipikwa; kwamba yaliyotokea si lolote wala chochote.

Ni jambo la bahati mbaya kwamba watawala wetu wanataka kutulazimisha kukubaliana na mfumo hatari sana wa kukwepa wajibu; kwamba watu watende maovu lakini wanaachwa tu walivyo, hakuna wa kumchukulia hatua. Wapo juu ya sheria!

Tujikumbushe kitu kimoja hapa. Msuguano ambao unadaiwa au maneno anayosema Pinda ni hayo hayo yaliyompa uwaziri mkuu; kwamba kuna watu walishindwa kuwajibika vilivyo katika dhamana walizokuwa wamekabidhiwa, ama kwa sababu ya pupa au kushindwa kupima mambo sawasawa wakajikuta wanaruhusu nchi kutapeliwa na kampuni hewa ya Richmond.

Baada ya mambo kuchemka vilivyo, ikagundulika kwamba kulikuwa na uzembe wa hali ya juu, nasisitiza, uzembe wa hali ya juu katika mchakato mzima wa mkataba wa kufua umeme wa migawati 100 ambao ulitolewa kwa kampuni ya Richmon Development LLC. Huu ni uzembe, huku ni kushindwa kuwajibika na kwa kweli ni kulisababishia taifa hasara.

Pinda ni lazima afahamu kwamba Richmond ilisababisha hasara kubwa kwa taifa hili; kwanza kuna fedha za walipa kodi walipewa ili kusafirisha mitambo; kuna kushindwa kutekeleza mradi kwa wakati na hivyo kuleta adha kubwa ya ukosefu wa umeme. Hasara ya kukoseka kwa umeme huku nchi ikiendesha mgawo wa nishati hiyo ni hasara kubwa sana ya kiuchumi ambayo haijafidiwa hadi leo.

Wapo watu waliofunga ofisi zao, vipato vyao vikapotea, wapo walioshindwa kulipia mikopo yao na kuishia kufilisika, wapo walioshindwa hata kutimiza wajibu wao kwa familia zao; kwa kifupi madhara ya Richmond yakichambuliwa vilivyo na kuwekwa hadharani, umma unaweza kuandamana na kuasi.

Kadhalika, Pinda anafahamu vilivyo kuna sakata la wizi wa fedha katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), anafahamu vilivyo wahusika wakuu, mojawapo ni Kampuni ya Kagoda Agriculture Limited. Pinda anajua nani anatuhumiwa kuwa mmiliki wa kampuni hii.

Baadhi ya watuhumiwa wa EPA wako kortini, lakini si Kagoda, Pinda anafahamu haijafanywa lolote, ni bahati mbaya kwamba serikali kama si mfumo mzima wa chama tawala na serikali yake, wanalinda wahusika wa Kagoda wasifikishwe mahakamani. Pinda anajua tuhuma za wizi wa Sh bilioni 40 si maneno maneno tu bungeni, ni uporaji mkubwa na mbaya kwa taifa!

Lakini kama sote tukikubali kwamba Richmond ilisababisha watu kuwajibika, kwa maana ya mtangulizi wa Pinda, Edward Lowassa, na mawaziri wengine wawili, Dk. Ibrahim Msabaha na Nazir Karamagi; ni dhahiri kwamba ilikuwa tatizo.

Serikali ilikubali baraza la mawaziri livunjike kwa sababu ya Richmond. Pinda alikuwa serikalini wakati huo, yaani Februari 2008 na sasa angali serikalini, anafahamu vilivyo ukweli huu.

Kwa kutambua ukweli huu umma hadi sasa haujaweza kujua ni wapi watu waliowajika kwa sababu ya Richmond wanapata ujasiri wa kusimama na kutaka wasafishwe, wanapata wapi jeuri ya kutaka kuwabomoa wale ambao waliendesha uchunguzi dhidi yao na kuweka kila kitu hadharani? Wapi wanapata nguvu hizi?

Kwa kauli ya Pinda naweza kusema naye si mmoja ya nguzo ambazo watu hawa walioanguka kwa sababu ya Richmond wanapata egemeo la kuendesha mapambano kiasi cha kuifikisha nchi katika wakati mgumu kama sasa, yaani kulifanya Bunge lionekane kama kituko kwa wananchi waliokuwa wamelijengea heshima na kuliheshimu?

Binafsi naamini Pinda ameteleza Igunga, tena utelezi huu ni mbaya zaidi kwake kwa kuwa huyu ni mtu ambaye amekuwa akisimama kwenye mstari wa uadilifu, kuchukia kwa maneno na pengine kwa vitendo tabia ya kufuja mali ya umma.

Lakini jaribio lake la kutaka kusema kwamba kelele au maneno ya pale bungeni hayana maana ila wananchi wampime mbunge wao kwa kuwa tu amehamasisha maendeleo jimboni ni kauli za bahati mbaya kutoka kwenye kinywa cha mtu wa nafasi kama yake.

Ni kwa maana hiyo sasa umma unaweza kupambanua kwamba serikali kwa ujumla wake ilikuwa na mkakati wa kusafisa wote waliohusika kwenye Richmond.

Nikikipanua wigo zaidi, serikali yetu inaonyesha kuwa haijali wala kusumbuliwa na kelele za kutaka uwajibikaji kwa wale wote walioshindwa kufuata mstari wa maadili. Kauli ya Pinda inasumbua na inakasirisha, haifanani na mtu ambaye anachukia machafu na uroho wa kuifilisi nchi. Pinda umekuwaje tena?

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: