Kumbe watu tunao, sasa tatizo nini?


Ezekiel Kamwaga's picture

Na Ezekiel Kamwaga - Imechapwa 18 May 2011

Printer-friendly version
Waraka wa Wiki

NILIJISIKIA faraja kubwa wiki iliyopita wakati nilipoona picha ya wawakilishi wa Tanzania katika Mkutano wa Umoja wa Mataifa nchini Uturuki uliozungumzia Maendeleo ya Nchi Masikini.

Kuna picha moja nilimuona Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal, aliyemwakilisha Rais Jakaya Kikwete kwenye mkutano huo na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka wakibadilishana mawazo.

Dk. Bilal ni msomi aliyebobea katika fani ya nishati ya nyuklia. Profesa Tibaijuka amebobea katika uchumi wa kilimo, na baada ya kufanya kazi Umoja wa Mataifa (UN) kwa kipindi kirefu, ana ufahamu mkubwa kuhusu masuala ya makazi na umasikini.

Faraja yangu haikutokana tu na ukweli kwamba viongozi hao wawili wamesoma hadi kufikia kiwango cha juu lakini zaidi ni ule mjumuiko wa uzoefu na weledi ambao watu hao wawili wanatengeneza kwa pamoja katika maisha yao ya kikazi.

Hatujapata taarifa rasmi kuwa ni kipi hasa nchi yetu imenufaika kutoka katika mkutano huo ingawa lililo wazi ni kuwa hakuna anayeweza kusema Tanzania haikuwakilishwa vizuri katika mkutano huo. Watu wa kusimama na kuzungumza walikuwapo na ninajua wote hao wawili wanaheshimika.

Ukizingatia kwamba nusu ya wajumbe zaidi ya 800 wa mkutano ule walikuwa tayari wanamfahamu Tibaijuka, hiyo ilikuwa ni faida kwa Tanzania kwa vile lengo la mkutano huo lilikuwa ni kuzisaidia nchi masikini kupambana na umasikini.

Afghanistan walikwenda kwenye mkutano ule lakini waliongozwa na rais wao Hamid Karzai na maswahiba zake. Jirani zetu, Kenya na Uganda nao walikwenda kwenye mkutano ule lakini kwa maana ya kombinesheni, wangefurahi kama wangewakilishwa na Tibaijuka na Bilal.

Na hili wala halijatokea Istanbul peke yake.

Dk. Salim Ahmed Salim ndiye aliyeteuliwa na UN kuwa msuluhishi katika mgogoro wa Darfur, nchini Sudan. Benjamin Mkapa alipitishwa kusimamia kura ya maoni kuamua iwapo Sudan Kusini ijitawale au la.

Omar Nundu, ambaye sasa ni Waziri wa Miundombinu, alikuwa Rais wa Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (ICAO) kabla ya kustaafu. Nafasi hiyo ni sawa na kuwa Rais wa FIFA kwa jamii ya soka. Ni nafasi kubwa katika sekta ya usafiri wa anga.

Kama tukianza kutaja majina ya Watanzania ambao wakiwa nje ya nchi wamefanya makubwa na wana heshima kubwa, orodha itakuwa ndefu na sitapata wasaa wa kujadili kile nitakacho.

Pamoja na heshima yote hiyo ambayo Watanzania wameileta, nchi yetu kila kukicha inaonekana hainufaiki na kundi hili la wajuzi waliopo nchini. Na wakati mwingine, huwa ni huzuni tupu.

Wakati Dk. Salim akitumwa kusuluhisha migogoro mbalimbali duniani na akiwa Katibu Mkuu wa uliokuwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU), hali ya kisiasa katika visiwa vya Zanzibar anakotoka ilikuwa mbaya, mbaya sana.

Na Mkapa mwenyewe wakati akiwa rais, ndipo yalipotokea yale mauaji ya Zanzibar ya 26-27 Januari, 2001. Nje ya Tanzania ni msuluhishi anayeheshimika, ndani ya nchi mauaji ya kisiasa yanatokea wakati yeye akiwa Amiri Jeshi Mkuu!

Wakati Nundu akiaminika duniani na kupewa madaraka makubwa, Shirika la Ndege la hajaonesha cheche hasa za kiutendaji katika kushughulikia matatizo ya mashirika ya umma yanayotoa huduma nyeti kama hili la ndege (ATCL) na ya reli (TAZARA) na (TRC) ambayo yanasubiri mipango endelevu.

Nilikuwa najiuliza: Hivi waziri Nundu alikuwa akiongea nini na viongozi wenzake wawakilishi kutoka Kenya na Ethiopia wakati walipokuwa wakijadiliana kuhusu sekta ya mawasiliano ya ardhini na angani katika nchi zao? Alichangia nini katika medani ya kimataifa iwapo nyumbani hali inasikitisha?

Mifano mingine bado ipo.

Dk. Bilal yu hai na kila mtu anajua weledi wake kwenye masuala ya nyuklia. Hata hivyo, tayari tumeambiwa kuwa wakati nchi yetu bado haijaweka sheria maalumu itakayotawala uchimbaji wa madini ya uraniamu nchini –kichagizo muhimu katika masuala ya nyuklia, tayari baadhi ya makampuni ya kimataifa yameanza shughuli za kutafuta madini hayo nchini.

Kuna msemo wa Kiswahili usemao Nabii Hakubaliki Kwao ambao unaweza kutumiwa na baadhi ya watu kulieleza vizuri hili. Lakini, mbona Marekani, India, China, Singapore, Botswana, Brazil wanawaheshimu wataalamu wazawa na wanawatumia? Hili la nabii hakubaliki kwao haliwezi kukubalika Tanzania tu wakati kwingineko likikataliwa na kudharauliwa.

Katika miongoni mwa maandishi maarufu ya Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, lipo lile analosema kwamba, “Ili nchi iendelee, inahitaji mambo manne – Watu, Ardhi, Siasa Safi na Uongozi Bora.

Dk. Salim anaamini kuwa Mwalimu angehitaji kuongeza jambo la tano – Nyenzo – ili kuendelea kwa maana bila ya nyenzo, watu hawataitumia vizuri ardhi. Ninaamini Mwalimu hakutakiwa kuzungumzia nyenzo kwa sababu watu waliowezeshwa wanaweza kabisa kuibua nyenzo muhimu za kufanyia kazi.

Ndiyo maana kuna kipindi wanajeshi wa jeshi la ulinzi la wananchi wa Tanzania waliokuwa kiwanda cha Nyumbu walifanikiwa kutengeneza gari. Kama watu waliweza kutengeneza gari, kuna nyenzo gani ya uzalishaji ingeshindikana kubuniwa?

Ukitaka kusikitika jiulize watu wa Nyumbu wanafanya nini sasa? Hamna kitu. Na bado tunaagiza matrekta ya kulimia kutoka nje ya nchi wakati kuna viwanda vya matrekta hapa nchini vya kuweza kutengeneza matrekta nyumbani.

Kuna mahali nchi yetu inakosea katika namna ya kuwatumia wataalamu wetu na kuutumia utaalamu tulionao kupitia wenzetu hawa. Labda niambiwe hatuna wataalamu wa maana bali wa maneno matupu. Na huo wenyewe utakuwa ni usaliti kwa Taifa.

Ama watu hawatumiwi ipasavyo au wataalamu wetu ni watu wanaozungumza kile wasichokiamini na wanaamini kile wasichokizungumza.

Bado nipo gizani. Kwa nini tuko hapa na utajiri wote huu wa vipaji vya watu?

0718 81 48 75, www.ezekielkamwaga.com
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: