Kumfunga Maranda bila wezi wa Kagoda ni bure


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 25 May 2011

Printer-friendly version
Rajabu Maranda akielekea gerezani

 WIKI hii mavuno ya kwanza ya haki kwa wezi wa fedha za Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) Katika Benki Kuu (BoT) yameanza kujitokeza. Lakini hisia za watu zimeonyesha wengi kutokufurahishwa na kiwango cha adhabu.

Washitakiwa wawili ndugu, Farijala Hussen na binamu yake Rajabu Maranda sasa wamethibitika ni wezi wa fedha za EPA, na wametiwa hatiani kwa kujipatia Sh. 1.8 bilioni. Wamehukumiwa kwenda jela jumla ya miaka 21, lakini watatumikia miaka mitano tu kwa kuwa makosa hayo yanakwenda sambamba katika kuyatumikia jela.

Mbali na kifungo hicho, Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu iliyokuwa inasikiliza kesi hiyo imewataka kurejesha fedha hizo watakapotoka jela na wakishindwa kufanya hivyo, wafilisiwe mali zao.

Jambo kubwa hapa ni kwamba mmoja wa wezi ni Maranda ambaye ni kada wa muda mrefu wa CCM na ni Mweka Hazina wa CCM mkoani Kigoma. Mavuno haya ni ya kwanza katika kesi 13 za EPA zilizopo mahakamani.

Suala la EPA limekuwa tete kwa muda mrefu tangu lilipolipuliwa na Katibu Mkuu wa CHADEMA, wakati huo akiwa mbunge wa Karatu, Willibrod Slaa, lakini serikali kwa kiburi tu ikajaza pamba masikioni.

Kwa habari mbaya, baada ya kuona kuna shinikizo la wafadhali, serikali ikiwa imekwisha kujichanganya juu ya ukweli wa EPA, iliamua kufanya ukaguzi wa akaunti hiyo BoT na kubaini kuwa fedha zilizochotwa ni Sh. 133 bilioni. Makampuni yaliyotajwa kujinufaisha na wizi huo ni pamoja na ya kina Maranda walioanza kutumikia kifungo jela.

Kinachosikitisha ni kwamba, kwa makusudi serikali hadi leo inakwepa kwa nguvu na hila kuwashughulikia wote waliohusika na EPA.

Kampuni iliyoasisi mpango huu haramu wa kuiba fedha za umma, Kagoda Agriculture Limited, wahusika wake hawajakamatwa na wala hakuna taarifa zozote kama katika Sh. 40 bilioni ilizochota yaani asilimia 30 ya fedha zote, walirejesha au la.

Kumekuwa na madai kwamba walioandamwa kwenye EPA ni dagaa tu, lakini vigogo kama Kagoda hawaguswi ingawa wanadaiwa wao ndio hasa waliokuwa mstari wa mbele kuasisi mpango huo haramu.

Ni kweli kesi moja kati ya 13 za EPA imehukumiwa, lakini kwa mawazo ya wengi, kulingana na kosa lenyewe na kwa kuzingatia nchi sasa ilivyochafuka kwa ufisadi, hasa wa kujichulia mali ya umma kana kwamba hakuna sheria, wala mwenye wajibu wa kilinda, adhabu kubwa zaidi ilitarajiwa kwa wahusika.

Inawezekana kwamba wanaotoa maoni ya kuwa akina Maranda wamepewa adhabu ndogo kwa kuangalia miaka mitano hawajui jela na hawajawahi kuonja makali ya kunyang’anywa uhuru wao kwa kutupwa jela.

Hata hivyo, hisia za watu  juu ya udogo wa adhabu si za kupuuza kwa kuwa katika mazingira ya kurasimishwa kwa ufisadi katika ofisi za umma ni lazima adhabu kali zingetolewa kuwasilisha ujumbe mmoja kwa wananchi wote, kwamba taifa hili sasa lina kile kinachoitwa kutokuvumilia kwa hali yoyote vitendo vya rushwa.

Baba wa Taifa, aliwahi kusema kwamba ni lazima serikali iwatishe wala rushwa. Mwalimu alisema walitunga sheria ya kutokumpa hakimu mwanya wa kuamua atoe adhabu gani kwa mlarushwa, ilikuwa ni kifungo na viboko juu, alipigwa viboko 12 wakati anaingia jela na 12 wakati anatoka akamuonyeshe mkewe.

Kwa kutafakari msimamo wa Mwalimu ambaye katu hakuvumilia rushwa, ukitazama hali ya mambo inavyokwenda sasa ndani ya serikali na hasa kwenye chama tawala, ni kama vile kuna kusita kwingi katika kupambana na maovu haya. Kuna maneno mengi kuliko matendo halisi.

Ni kweli hukumu hii ya kwanza ya EPA ni kielelezo cha kuthubutu kwa serikali kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wahusika wa sakata hili, lakini kielelezo hiki kinapwaya pale watu wanapotazama kwa mapana athari za kuacha baadhi ya watuhumiwa nje ya mchakato wa kisheria, hivyo kujenga hitimisho kwamba wapo watenda uhalifu wanaoguswa na wapo wanaotembea huru huku mabegani mwao wakiwa wamebeba rundo la tuhuma za ufisadi.

Pamoja na kuelemewa na tuhuma hizi, wanaachwa wanaranda mitaani, wanakumbatiwa katika vikao vya maamuzi vya chama, na kikubwa zaidi wametetewa kwa muda mrefu hadi chama tawala kilipojikuta kikipoteza umaarufu wake kwa kasi ya ajabu kama matokeo ya uchaguzi mkuu yalivyothibitisha kwamba chama hicho ni lazima kifanye maamuzi magumu vinginevyo kinaondosheka madarakani.

Kwa hukumu ya wiki hii dhidi ya Maranda na Farijala, serikali na hata chama tawala ikiunganishwa na harakati zake za kujivua gamba, wanaweza kutamba kwamba sasa hawana msalie Mtume na rushwa, lakini chereko chereko hizo zinazima kama moto wa karatasi kwa sababu, katika vita hivi kuna sura ya ubaguzi.

Ubaguzi huu ni wa kutazama yupi ashitakiwe na yupi aachwe. Ni dhambi mbaya. Ubaguzi haujawahi kushinda, ndiyo maana kwa miaka yote hii tangu mwaka 2008 moto wa EPA ulipolipuka serikali haijawahi kuwa na sura ya kuaminika mbele ya umma kuhusu vita dhidi ya ufisadi.

Kwa maana hii serikali isije kujisifu kwa hukumu hii ya miaka mitano jela kwa watu waliokwapua Sh. bilioni 1.8 kwa sababu bado adhabu hii haijionyeshi kuwa tishio kwa wala rushwa na mafisadi ambao kuna kila ushahidi kuwa wamesheheni serikalini na kwenye chama tawala.

Serikali pia haina sababu ya kushangilia kwa kuwa bado imeendelea kukumbatia mapapa wa ufisadi ambao waliasisi mpango huu haramu. Kwa bahati mbaya zaidi hata vyombo vya dola hasa vya usalama ama vimekataa kuusaidia umma kujenga imani na serikali katika vita hivi kwa kushindwa kuchukua hatua za kuwafichua mafisadi wote, au wanakula na mafisadi kiasi cha kuwa walinzi wa mafisadi badala ya wananchi.

Kwa hiyo, hukumu hii, pale ambako ilitarajiwa iwe kielelezo cha ushindi kwa serikali katika vita hivi, imegeuka kuwa kichekesho kwa kuwa miaka mitano ya kukaa jela, wezi hawa wataishia tu kukaa jela si zaidi ya miaka mitatu, kwa maana hiyo hivi punde tu watatoka na kuendelea kutanua mitaani wakiwa huru kama watu wengine.

Kuna mwanasiasa mmoja alitoa maoni yake mara baada ya kusikia hukumu ya akina Maranda na kusema “ingekuwa China hawa ama ingekuwa ni kifo au kifungo cha maisha”.

Ieleweke kwamba kadri Kagoda itakavyolindwa, hata wafungwe akina Maranda wangapi, bado vita dhidi ya ufisadi haitakuwa na mafanikio yoyote kiasi cha kutisha mafisadi na umma kusadiki kuwa serikali inachukia ufisadi.

0
Your rating: None Average: 5 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: