Kuna amani Tanzania?


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 08 July 2008

Printer-friendly version
Kalamu ya Jabir

ANA lundo la nyaraka. Kila ukiangalia barua alizonazo, hupati jibu kwa haraka. Ni lundo kubwa kiasi cha kukushangaza na kujiuliza 'imekuaje huyu Mtanzania.' Hivi amemkosea nani?

Ni Johari Salum Msuya, bibi anayehangaikia haki yake kwa miaka 16 sasa. Hajakosea kitu, bali katika kufuatilia tatizo linalomsibu kwa muda wote huo, amejenga maadui wengi kuliko marafiki.

Matokeo yake shauri lake linapigwa danadana na maofisa wa umma, kisha linabaki palepale penye mkwamo?

Bibi Johari ni mama anaishi kwa ufukara mkubwa ndani ya mitaa ya Kinondoni, Dar es Salaam, baada ya kuporwa nyumba aliyokuwa amepewa na serikali miaka kadhaa iliyopita.

Nyumba hii alipewa baada ya mmiliki wake wa awali, kufariki dunia na kukosa mrithi wa kumiliki. Ni baada ya kuthibitika haikuwa na mrithi kwa kuwa muda wa kufungua madai ulipita bila ya kujitokeza mrithi wake. Mwisho ikakabidhiwa kwa Kabidhi Wasii Mkuu ambaye alimkabidhi Bi, Johari.

Nyumba hiyo ipo Kitalu 31A, mtaa wa Karafuu, Kinondoni Dar es Salaam. Ni jiji hili ambalo lina Mkuu wa Mkoa, mkuu wa wilaya na meya wa Manispaa.

Ungetarajia mtiririko huu wa viongozi wa umma wangeshirikiana vizuri na maofisa wa kwenye wizara na idara za serikali, uwe ni msaada kwa bibi huyu.

Asilani abadani. Si mtendaji wa mtaa anayeifahamu vilivyo historia ya nyumba hiyo pamoja na hali halisi ya Bibi Johari, si maofisa wa wizara na idara zilizohusika na tatizo lake, wala Ofisi ya Rais, iliyotatua utata.

Fikiria unafunua mafaili yaliyosheheni nyaraka, halafu unakuta ofisi moja ya umma imetoa barua 30 zenye matamko yanayotofautiana kuhusu mgogoro wa nyumba hiyo.

Lakini baadhi ya maofisa wa ofisi ya Kabidhi Mkuu wa serikali, wameonyesha ufisadi mkubwa kwa kushirikiana na maofisa wa Idara ya Mahakama, Polisi na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Kikubwa kinachoonekana katika suala hili, ni kupindisha kanuni na taratibu za utumishi na hata sheria za nchi.

Ofisi ya Waziri Mkuu imefikiwa na Bibi Johari kuombwa kusaidia kupatikana kwa ufumbuzi, lakini hakufanikiwa kumpata waziri mkuu.

Watumishi wenye akili iliyotulia, wasingetarajiwa kumnyima mama huyu kuonana na waziri mkuu. Angalau basi, wangemsaidia kutatua tatizo lake. Hawakufanya hivyo!

Wamemnyima fursa aliyoomba ya kukutana na waziri mkuu na wameshindwa pia kumsaidia.

Haya yalianza mwaka 1992 pale Mahakama ilipotoa tamko rasmi kuwa nyumba hiyo haina mrithi na kwa hivyo inapaswa kuwa chini ya dhamana ya Kabidhi Wasii Mkuu wa Serikali.

Na ndivyo ilivyokuwa. Barua nyingi zinathibitisha ukweli huo. Bibi Johari aliiomba nyumba hii baada ya kuthibitisha kuwa mmiliki wake wa awali, Juma Tasbihi Kipofu, hakukwa na mrithi.

Mtu anayetajwa kama Patason Kasembe, aliyekuwa akimsaidia Mzee Juma wakati wa uzeeni muda mfupi kabla ya kufa kwake, naye alifariki dunia.

Anayetajwa kama Shewere, Mkuu wa Kanda wa eneo iliyopo nyumba, anasema baada ya Kasembe kufariki, walitokea wavamizi wakaingia.

Anasema waliwahi kutolewa kwa amri ya mahakama, lakini amri hiyo haikupatikana wakati wa kufuatiliwa na hao waliosemekana kuwa walivamia hawakutoa amri iliyosema nyumba haina mrithi.

Ofisi ya Mkuu wa Wilaya Kinondoni ilijitahidi sana kuhangaikia amri hiyo, lakini haikufanikiwa kuipata na hivyo, E. Nyambibo, Afisa Tawala Wilaya, anasema katika barua yake ya 16 Novemba 1992, yenye Kumb. A. 10/I/57 kwamba 'suala hilo limekuwa gumu kulishughulikia.'

Nyambibo alikuwa amemwandikia Kabidhi Wasii Mkuu wa Serikali akitaka msaada kwa kuwa anafahamu kuwa katika ofisi hiyo suala hilo linafahamika vizuri.

Hii ni kutokana na kuwahi kufikishwa na Jaji Mweisumo, alipokuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani.

Jaji Mweisumo alikuwa Naibu waziri katika wizara hiyo katika miaka ya mwanzo ya tisini. Wakati huo, Waziri wa Mambo ya Ndani alikuwa Augustine Mrema.

Katika barua yake kwa Kabidhi Wasii Mkuu, 22 Septemba 1992, Jaji Mweisumo alimtaka asaidie taratibu za kuwezesha nyumba hiyo kuuziwa Bibi Johari ambaye amekuwa akiishi wa shida kwa kukosa nyumba.

Barua hiyo ilinakiliwa kwa Waziri Mkuu ambaye alipata kuandika barua yenye kumb. PM/2/M.50/13 ya tarehe 6 Oktoba 1992.

Kabidhi Wasii Mkuu alipata kuandika barua akifahamisha kuwa amegundua kulikuwa na mrithi aliyehalilishwa na Mahakama ya Mwanzo Kinondoni mwaka 1986, baada ya kujitokeza kuwa aliuziwa nyumba hiyo na aliyekuwa mrithi halali.

Leceus Kisumo ndiye mtu anayetingisha taasisi za serikali akidai aliuziwa nyumba hiyo. Baada ya mbinu zake kufanikiwa, ofisi ya Kabidhi Wasii Mkuu iliungana naye na kutoa barua ya kuthibitisha kwamba nyumba hiyo imepata mwenyewe.

Kwa bahati nzuri, taarifa za barua hii zilimfika Bibi Johari kwa kuwa zilipelekwa kwa Katibu Mkuu na Ofisi ya Waziri Mkuu.

Kumbe Kabidhi Wasii Mkuu alisahau – kwa hakika wala siyo kuwa alisahau ila ndivyo anavyoumbuka mpanga maovu - kwamba zipo kumbukumbu kadhaa zinazoonyesha kuwa Mahakama ya Kindononi imekanusha kuwahi kutoa idhini ya kurithiwa kwa nyumba hiyo.

Hakimu Mfawidhi wa Kinondoni alibadilishana na Kabidhi Wasii Mkuu taarifa ya kukanusha kurithiwa nyumba hiyo kupitia barua zenye kumbukumbu PCK/KND/CR/5/71 ya 8 Oktoba 1998; ADG/PA/AG/97/31 ya 7 Februari 2003 na PCK/KND/CR/5 ya 19 Februari 2003.

Bibi Johari aliandika barua kwa Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu akimfahamisha alichokiita, 'upotoshaji mkubwa uliofanywa na Ofisi ya Kabidhi Wasii Mkuu' akikumbusha matamko hayo ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya wilaya ya Kinondoni.

Anashangaa: Kabidhi Wasii Mkuu anajaribu kuieleza Ofisi ya Waziri Mkuu kuwa wakati ofisi ya Kabidhi wasii inapangisha nyumba hiyo kwa kodi ya 2,000/- kwa mwezi 18 Januari 1993 tayari nyumba hiyohiyo na wakati huohuo imeshapata msimamizi wa mirathi.

Anasema mrithi aliteuliwa na Mahakama ya Mwanzo Kinondoni 10 Februari 1986. 'Jambo hili linashangaza na halina ukweli na linaacha maswali mengi,' anasema Johari kwa masikitiko.

Anasema, 'Je, Serikali kupitia ofisi ya Kabidhi Wasii ilinikabidhi nyumba iliyokuwa tayari na msimamizi wa mirathi?'

Ndipo akataja kumbukumbu za barua hizo tatu zinazokanusha kuwepo msimamizi wa mirathi.

Suala la Bibi Johari linakirihisha kwa namna lilivyoshughulikiwa na kwa sasa ni kama vile hakuna msaada anaopata, maana alitimuliwa kwenye nyumba hiyo kwa hati bandia ya Mahakama.

Wakati anatimuliwa vitu vyake vya thamani ya Sh. 9 milioni vimechukuliwa na mtu aliyedanganya Mahakama. Sasa Johari analala ugenini akiwa na mtoto wake wa kiume mwenye ulemavu asiyeweza kujisaidia kwa chochote.

Kwa sasa analalamikia watu kadhaa waliomzushia mgogoro hata kumfukuza katika nyumba.

Miongoni mwao ni, Kabidhi Wasii Mkuu wa serikali, aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Philip Marmo, ambaye alimfuata wakati akiongoza wizara hiyo na uongozi wa jeshi la polisi wilaya, mkoa na taifa kwa kushindwa kumlinda dhidi ya madhalimu wa mali zake.

Matumaini yake pekee sasa yamebaki kwa mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Abbas Kandoro, ambaye anasifika kwa kusikiliza matatizo ya wananchi. Je, atamsaidia?

0
No votes yet