Kuna mtihani wa kuua siasa feki


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 07 December 2011

Printer-friendly version
Tafakuri

DUNIANI sasa kuna vita dhidi ya bidhaa bandia (feki). Hapa nchini Tume ya Ushindani wa Biashara (FCC) imekuwa na jukumu la kuteketeza bidhaa feki kwa kushirikiana na Shirika la Viwango Tanzania (TBS).

Bidhaa feki ni uhalifu. Ni kutengeneza bidhaa inayofanana na nyingine, kwa nia moja tu, kujipata faida kubwa kwa kuigiza kitu ambacho kina jina kubwa na hivyo kulaghai wateja kuwa inawauzia kitu halisi kumbe ni feki.

Mambo ya kuigiza hayapo kwenye bidhaa tu. Wapo watu wa aina kwa aina ambao huiga wengine kila siku iendayo kwa Mola. Wapo wanaoigiza sauti za wengine, miondoko, mavazi na hata wapo wanaoiga mfumo wa maisha binafsi wa watu wengine.

Katika siasa ndiyo kabisa usiseme, kuigana ni kama jadi; watu wanaiga wengine hadi unashindwa kujua hivi halisi ni yupi.

Tangu kuanza kwa mchakato wa katiba mpya nchini tumeshuhudia juhudi za dhati kwa baadhi ya watu kujaribu kutoa mawazo yao juu ya kile wanachokitaka, lakini katika harakati hizo pia wapo wengine feki.

Kwa mfano, wakati wananchi walipoanza kutoa maoni juu ya muswada wa sheria ya katiba mpya, katika ukumbi wa Karimjee, Dar es Salaam ilikuwa zaidi ya kueleza ubandia wa mambo.

Siku ya kwanza wananchi walipofurika katika ukumbi huo na kuwapo kwa hamasa kubwa, kesho yake kada mmoja wa CCM alifanya ghilba mbaya kwa kuwaalika chipukizi wake. Akawazoa kwa magari kutoka kwao mapema alfajiri ili kujaza ukumbi wa Karimjee.

Wananchi wengine walipofika saa mbili, walikuta ukumbi umejaa pomoni, lakini waliokuwako walikuwa chipukizi wa CCM waliokusanywa kwenye mashina kwa malipo.

Tukio hili halikuwa ulaghai wa kisiasa tu, bali pia ilikuwa  njia ya kujaribu kuwapiku CHADEMA ambao jana yake wanachama wake wengi walihudhuria kongamano hilo na kushiriki kutoa hoja katika kuboresha muswada huo.

Kwa hiyo, alichofanya kada yule wa CCM ilikuwa kujaza wakereketwa wake kwenye ukumbi ule ili nao wawe wengi. Lakini wingi wa kuiga kama wa jana yake kwa CHADEMA, haikuwa kujenga hoja ila kujaza watu ili wenye hoja wakose fursa na ikibidi kuzomea kama watazungumza.

Mfumo huu wa kuendeleza ufeki tumeushuhudia tena wiki iliyopita. Wabunge wa CHADEMA baada ya kususia kushiriki mjadala wa muswada wa sheria ya katiba mpya wa mwaka 2011 bungeni, walikutana jijini Dar es Salaam kushiriki vikao vya juu vya chama chao. Walitoka na maamuzi mengi, lakini moja ni kuunda kamati ya watu wachache ambayo ingetafuta uwezekano wa kuonana na Rais Jakaya Kikwete ili kuwasilisha hisia, hoja na kilio chao juu ya sheria hiyo ya kurekebisha katiba.

Baada tu ya CHADEMA kuazimia kukutana na Rais, Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC) siyo tu iliunga mkono hoja ya CHADEMA, bali pia ilitaka Rais Kikwete akutane na vyama vyote vyenye wabunge! Mara habari zikasambaa kwamba Chama cha Wananchi (CUF) ambao kimsingi ni sehemu ya serikali, nao wakaomba kukutana na Rais kama CHADEMA.

Ingawa hakuna mtu mwenye hati miliki ya mawazo, kitendo cha CUF kuibuka kipindi CHADEMA walichotaka kuonana na Rais na hoja ikiwa ni ile ile, hisia za ufeki ziliibuka. Kwamba hapa nani anamuiga mwenzake na kwa nini?

Hisia za ufeki zilizidi sana kwa sababu kuu mbili; mosi, CUF kupitia wabunge wao walishiriki kikamilifu katika mchakato wote wa kupitishwa kwa sheria hiyo; wabunge wake walijadili muswada huo, na pia walipata fursa ya kuwadhihaki wabunge wa CHADEMA waliosusa mjadala huo. Na hata katika kupitisha kifungu kwa kifungu hakuna mbunge wa CUF aliyekataa.

Kwa maneno mengine, hakuna chochote ambacho CUF walikuwa nacho hawakukisema ndani ya bunge, hivyo kuibuka nje ya bunge kufuata mkakati wa CHADEMA ni dhana ile ile ya kututengenezea bidhaa feki.

Pili, CUF na CCM wameunda serikali ya umoja wa kitaifa Zanzibar; wana nafasi ya Makamu wa Rais, Maalim Seif Shariff Hamad; wana mawaziri kadhaa, lakini pia wana nafasi za wawakilishi wa kuteuliwa na Rais wa Zanzibar.

Kwa mujibu wa Waziri wa Sheria na Katiba, Celina Kombani, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ambako CUF wanawakilishwa, walishiriki vilivyo katika matayarisho ya muswada huo. Kwa maneno mengine muswada huo ni sehemu ya kazi ya mikono ya CUF.

Kwa kuwa, walishiriki katika hatua zote za kuupitisha ni jambo la kushangaza kuwaona sasa wakiingia katika siasa za kuiga ili kuwa sawa na CHADEMA. Kwa mfumo huu wanatengeneza siasa feki ambazo hakika hazitawajenga.

Ufeki ni hoja moja, lakini hoja ya pili katika mkakati huu wa kujenga siasa feki, ni kwa Rais Kikwete mwenyewe, inawezekana kuwa CCM kwa kupitia NEC au kwa kuwashawishi marafiki wao CUF wameamua kutumia gia ya kuiga ya CHADEMA kwa nia moja tu, kuvunja mkakati wa CHADEMA katika suala zima la sheria ya kuandika katiba mpya ambayo inaweka utaratibu wa kuundwa kwa tume ya kuratibu nchakato wa kukusanya maoni ya wananchi katika upatikanaji wa katiba mpya.

Kwa kuwa taifa hili sasa linasujudu sana siasa za ghilba na feki, ukweli unabaki kuwa, hata kama CCM imecheza mchezo wa kuigiza ili kuivuruga CHADEMA katika hili, bado Rais ambaye ni mwenyekiti wa CCM amebebeshwa mzigo mabegani mwake kufanyia kazi waliyokubaliana na CHADEMA. Kikubwa, kufanya marekebisho ya sheria hiyo.

Inawezekana, fursa ya kukubali kuwaona CHADEMA haraka haraka ilikuwa njia ya kuwatuliza na kuonyesha kuwa serikali ni sikivu na iko tayari kwa majadiliano, kwa maana hiyo itafanyia kazi mapendekezo yaliyowasilishwa; lakini kama fursa hiyo ilikuwa aina nyingine ya kuendesha siasa feki, ni hakika sura ya Rais ipo hadharani ikisubiri kila aina ya hasira na kelele za makundi mbalimbali ya kijamii juu ya kuandikwa kwa katiba mpya.

Kibaya zaidi, ambacho kinaweza kutokea ni pale vyama vya siasa na wanaharakati wengine watakapohamasisha uasi wa umma dhidi ya mchakato huu. Hili litafanyika iwapo haya mazungumzo yaliyotokea kati ya Rais na CHADEMA hayatakuwa na tija na ikaonekana kuwa ni aina nyingine ya siasa feki.

Kwa vyovyote itakavyokuwa mwenye wajibu wa kuvunja utamaduni wa siasa feki katika mchakato wa katiba mpya ni Rais Kikwete. Kama alikuwa hajui, ukweli ni kwamba ameukubali mzigo huu, bila masharti yoyote na umma unasubiri atekeleze makubaliano, na kwa kufanya hivyo atakuwa ametoa mchango wake kukomesha siasa feki, vinginevyo amefungua lango la kushambuliwa na serikali yake katika mchakato mzima wa katiba mpya.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: