Kuna ukame wa viongozi waandilifu


Joseph Mihangwa's picture

Na Joseph Mihangwa - Imechapwa 28 April 2009

Printer-friendly version

SOMENI kitabu cha mwandishi Ibn al-Marzuban. Kinaitwa "Superiority of Dogs over those who wear clothes" – Mbwa walipozidi binadamu kwa akili.

Ndani ya kitabu kuna shairi liitwalo “The Passing of Men of Responsibility,” – Kutoweka kwa watu wenye wajibu na uadilifu. Anaandika:

“Hawapo tena watu waadilifu
katika dunia hii
Wale wanaotoa pishi zao
kwa wema wakati wa ukame,
Wamekwisha, hakuna aliyebakia;

Ni mjinga asiyeliona hilo,
kwamba hawapo tena,
Hawapo tena wenye
uadilifu na busara,
Isipokuwa fulani na fulani,
watasema, “na jina lake ni nani?”


Ibn al-Mazurban anamlinganisha mbwa na kizazi cha sasa cha kisiasa kisicho na shukrani, akisema:

Mmeiga sifa duni kuliko za mbwa,
Mbwa hutoa msaada na ulinzi,
Ni mwaminifu anayeheshimu kile unachomtaka afanye,
Hulinda ujirani wote bila ubaguzi.

Hutoa kwa hiari sio kushurutishwa
wala kwa rushwa;

Hukuponya hasira yako na
kukuondolea huzuni na fadhaa,
Ungekuwa kama yeye,
usingekuwa kaa la moto
moyoni mwangu.

Mwandishi analia. Anaona mgogoro wa kiutawala unanukia. Mgogoro huu unaweza kuelezewa kwa ufupi kama ifuatavyo: Uwajibikaji umekwisha na viongozi wanatumikia matakwa yao bila hofu ya kuulizwa.

Si hayo tu. Siasa imebinafsishwa. Uhuru wa habari umebanwa. Asasi za kiraia zimedhibitiwa na eerikali imejenga tabia ya “kuteleza.”

Tabaka la watawala huzidi kujiweka mbali na wananchi kwa kiburi cha pesa, isipokuwa unapokaribia uchaguzi. Limetekwa nyara na mitaji ya kimataifa; haliwezi kudumu kwa njia ya utawala bora bali kwa mizengwe na ubabaishaji.

Demokrasia ni serikali kwa njia ya majadiliano kati ya watu walio sawa na huru kwa uwazi, bila hofu wala upendeleo na kwa kuheshimiana.

Demokrasia ni zaidi ya kushinda uchaguzi kwa kishindo; bali ni nguvu ambayo uongozi wa nchi unawajibika kwake.

Lakini leo hii uhasama wa kisiasa umekithiri. Ibn al-Mazurban anaona muda mwingi unapotea kwa malumbano, kujihami na kwa maandalizi ya mbinu chafu za kushinda chaguzi kuingia au kubakia madarakani badala ya kushughulikia mipango ya maendeleo.

Viongozi walioko madarakani hawapo tayari kukaa na wapinzani kuzungumzia mambo ya manufaa kwa taifa, kisiasa, kijamii na kiuchumi. Wamewasahau wananchi. Wameweka mbele siasa za matumbo. Wamesahau kwamba ubora wa serikali hupimwa kwa ubora wa vyama vya upinzani makini na vyenye nguvu.

Wamepungukiwa hisia, msisimko na mguso wa kitaifa unaozaa uzalendo na ushujaa. Shauku ya wengi siyo tena kujenga jamii iliyo bora; bali mashindano ya panya katika kutafuta mali kana kwamba utajiri ndiyo mwisho wa yote katika maisha.

Uongozi unapita mikononi mwa wasomi wachoyo ambao si tu kwamba hawayaelewi matatizo halisi ya watu, bali pia hawataki kuyaelewa. Wako wapi viongozi bora?

Kutumikia kumegeuka kuwa kutumikiwa. Uongozi kwa mifano umegeuka kuwa uongozi kwa mizengwe na kuteleza. Ushiriki katika siasa umebanwa kwa manufaa ya siasa za vyama na kwa njia hii wananchi wanakosa mamlaka ndani ya nchi yao.

Tumepumbazika kwa kuiga tamaduni za wengine na kutafsiri maendeleo kumaanisha mashirika ya ndege, majengo marefu, mahoteli makubwa, mabenki, miziki ya kiuzinzi, uvaaji unaoacha mwili uchi na kuongea lugha za kigeni.

Kupenda kazi, nidhamu, usawa mbele ya sheria, fursa sawa kwa wote katika shuguhuli za kiuchumi, mambo yaliyochangia maendeleo ya kiteknolojia, kijeshi, kiuchimi na kisiasa hayatiliwi maanani.

Kimejengeka kiburi cha madaraka na kujiamini kupita kiasi. Wanaotahadharisha juu ya maovu katika jamii wanaitwa majina mabaya: wapinzani, wavivu wa kufikiri, wadhanifu au wasiolitakia taifa maendeleo, kumbe hicho ni kinyume chake.

Kwa wale mashujaa bandia, wanaodhani kwamba wanaweza kuchezea akili ya watu wetu milele kwa matakwa yao ya kichoyo, waelewe kwamba ushindi kwa njia ya mizengwe si ushindi; na kwamba uzandiki huzaa uzandiki.

Demokrasia itashamiri vipi wakati watu wanahangaika kwa njaa, wanatembea peku ili mradi tu wengine wachache wamiliki magari ya kifahari na mahekalu?

Ili serikali ipate uhalali wa kutawala, inapaswa kutekeleza mambo yafuatayo: Kupanua maendeleo ya kiuchumi; kujenga umoja wa kitaifa na kuongeza uwezo wa serikali katika kukabiliana na mabadiliko ya kijamii.

Tanzania inaweza kuepuka kuingia hali anayoilezea Ibn al-Mazurban. Hiyo ni kwa kukataa kuua demokrasia msalabani kwa jina la “Siasa za Vyama na Ubinafsi,” kulindana na hata kubinafsishwa kwa serikali na kikundi kidogo chenye nguvu ya fedha.

Bali taifa laweza kujikuta katika maelezo ya Ibn al-Mazurban Uhalali iwapo fedha itaachwa inunue siasa na siasa inunue fedha kiasi cha uongozi na uchumi kuwa mikononi mwa kikundi kidogo cha matajiri.

Kumetokea nini leo, kwamba nafasi za chama ni jambo la kufa na kupona kwa wakuu wa wilaya na mikoa, mawaziri na vigogo wengine? Ni uchu wa madaraka ya kisiasa; lengo ni kununua utajiri na si kutumikia umma.

Hapa hakuna kitakachokwenda mbele; maadili na malengo ya taifa yatapotea. Mwisho wa yote kutajengeka unafiki, uzandiki na ubabaishaji.

Kukosekana kwa tabia ya kukosoa na kukosolewa kutazaa kiburi, kunata, ukatili, uhaba wa uvumilivu; na hapo ndipo ngoma Italia sana, ambapo mwisho wake ni kupasuka.

Wale wanaojiona hawawezi kukosolewa watajihesabu kama miungu wadogo. Mwisho wa yote, maisha yatageuka ya kuabudu mashujaa wa ovyo. Ni ugonjwa mbaya unaoweza kuua demokrasia.

Katika kitabu chake, Tujisahihishe, Mwalimu Julius K. Nyerere anabainisha wazi kuwa ni vizuri tunapojadili masuala yanayoigusa jamii nzima kujifunza kusikiliza hoja zinazotolewa na wenzetu na kuzijibu kwa kuzikubali au kuzikataa bila kujali zimeletwa na marafiki zetu au wasio marafiki zetu.

Leo, mambo ni tofauti. Kuna hoja za chama tawala na hoja za wapinzani. Kuna sababu gani kukataa mchana kweupe tuhuma za ufisadi nchini zilizo wazi, kwa sababu tu zimetolewa na wapinzani?

Wanasiasa wasitangulize maslahi yao binafsi na ya vyama vyao; muhimu ni maslahi ya taifa kwanza na watu wake; vyama vya siasa baadaye. Tunaongozwa na Katiba ya nchi ambayo iko juu ya Katiba za vyama na juu sheria zingine zote.

Na kwa nini tuendelee kufumbia macho makosa ya wakubwa kwa sababu tu wamejificha kwenye mbawa za chama? Au tunataka kuingia katika ainisho la Ibn al-Mazurban? Tukatae hilo.

0
No votes yet