Kunadi mafisadi: JK kamdhalilisha Pinda


Mwandishi Maalum's picture

Na Mwandishi Maalum - Imechapwa 06 October 2010

Printer-friendly version
Gumzo

MGOMBEA urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jakaya Kikwete ameendelea kuwanadi wanasiasa wanaotuhumiwa kwa ufisadi.

Orodha yao ni ndefu lakini nitaje wale walionadiwa na kuombewa kura na Kikwete. Hao ni Basil Mramba, Edward Lowassa, Andrew Chenge na Rostam Aziz.

Hali kadhalika alipanda jukwaani na Frederick Mwakalebela, mmoja wa watuhumiwa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) katika kesi ya rushwa ya fedha za uchaguzi.

Hatua hii ya Kikwete ina sura nyingi, na mimi kama mwanachama halali wa CCM nalazimika tena kuijadili kama nilivyowahi kueleza msimamo wangu ndani ya chama, lakini ukapuuzwa na Kikwete mwenyewe kwa kuuita fitna.

Kuna mmoja wa wagombea ubunge wa CCM katika jimbo moja mkoani Mwanza ambaye amenieleza kuwa kama angeweza angeomba Kikwete asifike jimboni mwake kumwombea kura kwa sababu, zitapungua badala ya kuongezeka.

Hii ni kwa sababu, watu wengi katika jimbo lake wana chuki kali dhidi ya ufisadi waliofanyiwa na chama cha ushirika cha Nyanza na sasa badala ya serikali kuwachukulia hatua mafisadi hao, Kikwete ameahidi kutoa fedha na kuidhamini Nyanza eti ili isifilisike.

Anasema hatua ya Kikwete imeudhi wengi, kwa sababu fedha hizo pia zitaliwa na mafisadi na deni litabaki palepale. Anasema watu wengi wanamwona Kikwete kuwa na ushirika na mafisadi mahali popote walipo.

Msimamo huu wa Kikwete na ukaidi wa kutosikia maoni ya watu wa kawaida, unakiweka chama, serikali na TAKUKURU mahali pagumu na kwenye shaka kubwa na zaidi sana, unaliweka bunge rehani.

Kutafuta kura kwa gharama ya kutelekeza imani, misingi na uadilifu wa chama kutaigharimu hata serikali atakayoiunda hapo baadaye endapo atachaguliwa tena kushika madaraka.

Watu wema wanasema, hata kama serikali ya Kikwete ina mazongezonge ya rushwa na ufisadi, kama mgombea wa chama kinachojinadi na kudai kupambana na rushwa, alipaswa afanye angalau “usanii” wa kuuchukia ufisadi hadharani, hata kama ana ushirika nao nyuma ya pazia.

Mbona miezi ya mwanzo pale Lowassa alipojiuzulu, alikuwa anaogopa kuonekana naye hadharani na kulazimika kujificha na kwenda kwake usiku?

Ingeathiri nini kama angeamua kutokwenda Monduli, Rombo, Bariadi na Igunga? Sidhani kama ni lengo la Kikwete wala CCM kuchukua majimbo yote nchini?

Kwanza, haiwezekani, na pili hata kama ingewezekana, si afya kwa mustakabali wa taifa letu. CCM dhaifu kama tuliyo nayo, inahitaji vyama vya upinzani ili iweze kuongoza taifa hili.

Sikio la kufa halisikii dawa; kuna gharama kubwa tutalazimika kulipa kwa sababu ya ukaidi wa mgombea wetu kukumbatia mafisadi.

Tuombe Mungu, adhabu hiyo itolewe na mafisadi wenyewe kwa chama, badala ya wananchi kutoa adhabu hiyo ambayo itawaumiza hata wana CCM waaminifu.

Bunge lililomaliza muda wake, pamoja na udhaifu hapa na pale, liliweka rekodi ya aina yake pale lilipoweza kujadili na kupitisha maamuzi mazito yaliyolenga kuwaadhibu watuhumiwa wa ufisadi.

Hata kama baadaye lilistuka na kubadili mkondo chini ya uongozi wa Spika Samwel Sitta, lakini lilikuwa tayari limewaonyesha watu kuwa likiamua linaweza kufanya kazi yake sawasawa.

Mizengo Pinda aliyeshika wadhifa wa waziri mkuu baada ya Lowasa, kwa hekima kubwa aliweza kukaa katikati, bila kuhalalisha ufisadi lakini pia bila kuacha serikali ibebe msalaba wa ufisadi.

Watu wengi wanamwona Pinda kama mkombozi wa Kikwete japo wana shaka kama Kikwete analichukulia hilo kwa uzito unaostahili. Watu wana shaka kwa sababu hatua aliyoichukua Kikwete kumnadi na kumsifia Lowassa inatia giza katika uhusiano wa Kikwete na Pinda.

Kikwete alimtuma Pinda kwenda New York kumwakilisha katika mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Huku nyuma akapanda jukwaani na kumnadi Lowassa na kumsifia kama mchapa kazi na msafi.

Akawasihi watu wasahau yaliyopita na kuganga yajayo. Hizi si kauli nzuri kutolewa na mkuu kwa waziri mkuu aliyefukuzwa.

Kauli hizi zinadhalilisha kiti cha rais na Kikwete mwenyewe mbele ya Lowassa kwa sababu wote wawili walikuwa na uwezo wa kuzuia Lowassa asiondoke lakini, mmoja kama si wote wawili, alimgeuka mwenzake kwa sababu wanazozijua.

Maadam sasa tuna waziri mkuu mwingine, si vema kwa Kikwete kumsifia aliyepita kiasi hicho. Mwanandoa yeyote anafanya makosa kumsifia mtalaka wake mbele ya mkewe wa sasa.

Lisemwalo lipo, kama halipo laja. Kwa Kikwete kusema Lowassa alionewa, watu wanapata nafasi ya kuthibitisha uvumi ambao umekuwa unaenezwa na wapambe wa Lowassa kuwa atarejeshwa madarakani endapo Kikwete atachaguliwa tena kwa kipindi cha pili.

Wapambe hawa wanaenda mbali zaidi na kusema, baada ya Kikwete kumaliza muda wake, anayefuata ni Lowassa. Hii ina maana Pinda anapasha kiti moto ili mwenye miliki ya kiti hicho aje kukuta bado kina joto.

Hata kwa kitendo cha Kikwete kumsifia Lowassa kuwa mchapakazi na anamwamini kwa mengi, ni sawa na kumpiga kofi Pinda ambaye amekuwa akiongoza shughuli za serikali bungeni huku akilazimika kutetea uozo ambao yeye hakuhusika kuutenda.

Serikali hii ya Kikwete na Pinda inayojinadi kupambana na ufisadi kwa kupanda jukwaani kuwanadi mafisadi, ni mzigo mzito zaidi kwa Pinda ambaye ni mtu mnyenyekevu anayelazimika kutumiwa bila kutumika.

Pinda anadhalilishwa bila kudhalilika; ni msafi anayetumika katika chombo kichafu bila kuwa na uwezo wa kukisafisha.

Kunadi watuhumiwa wa ufisadi na kuwaombea kura ni kulidhalilisha bunge lililojadili na hatimaye kupitisha maazimio kadhaa ya kushughulikia ufisadi nchini.

Kikwete ambaye katika mazungumzo ya faragha hupenda kudai kuwa analiheshimu sana bunge na kamwe hawezi kuingilia mamlaka yake, kwa kitendo hiki amelifedhehesha bunge.

Ni yeye aliyekubali Lowassa ajiuzulu; ni yeye aliyekubali barua ya Chenge kujiuzulu kutokana na kashfa ya rushwa ya ununuzi wa rada. Ni yeye aliyemwondoa Mramba katika baraza la mawaziri na bila shaka kuridhia hatua za kumlaza rumande na kumpeleka mahakamani.

Sasa ni yeye Kikwete yuleyule anawashika mikono na kuiinua juu akiwaombea kura. Tabia hii ya kudhalilisha vyombo vya dola na vile vya utoaji haki, inaondoa heshima na utukufu wa dola zima na kuifanya serikali iwe kijiwe cha mafisadi.

Haishangazi sasa kuwa Bunge letu linaloundwa na wabunge wengi wa CCM, limejaa idadi kubwa ya wafanyabiashara ambao wanahangaika kulinda mali zao na familia zao dhidi ya hatua za kisheria zinazoweza kuchukuliwa dhidi yao. Tusikubali Kikwete kutufikisha huko.

Mwandishi wa makala hii, amejitambulisha kuwa msomaji wa MwanaHALISI na mwanachama wa CCM.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: