Kura yako ni haki, ukombozi wako


Ndimara Tegambwage's picture

Na Ndimara Tegambwage - Imechapwa 27 October 2010

Printer-friendly version
Uchambuzi

HAKUNA utata. Hakuna visingizio. Kila kura ina umuhimu. Asiyepiga kura tayari “amepiga kura” ya kuchagua asiyempenda. Asiyefaa. Asiyeweza. Amka!

Mwone huyu. Ametoa macho. Mkali mithili ya pilipili ya kiangazi. Anang’aka: “Mimi ni kabwela bwana! Kura yangu siyo muhimu.”

Acha mzaha! Nani kakudanganya? Wewe ndiye unafukuzana na kunguru. Mnanyang’anyana mifupa ya samaki – yale mabaki baada ya viwanda kunyofoa minofu ya kuuza Ulaya. Mapanki.

Umetoka kuwa bwana, umekuwa mtwana. Ziwa lako lakini huwezi kula samaki. Minofu ya samaki wanakula wazungu – Ulaya. Wewe ule mapanki, mwaka hadi mwaka; ndani ya nchi yako.

Hapana. Kura yako ina thamani. Itaweza kuamua nani asimamie ziwa; ili upate samaki; ili upate kitoweo; ili urejeshe hadhi yako, ili utoke utumwani.

Kumbuka! Wewe ndiye mkazi wa mwambao wa Ziwa Viktoria. Wewe ndiye mkazi wa visiwa vya ziwani. Unakula harufu ya samaki; wazungu wanakula minofu. Unakula mapanki; wao wanayasaga kwa chakula cha nyau.

Mwone huyu. Uso umekunjika kama nane. Ni joto, baridi, njaa na magonjwa. Hajui umoja, amani na utulivu; nyimbo za wenyewe hizo. Yuko vitani – mchana na usiku. Halafu unasikia anasema hatapiga kura.

Amka! Nenda kituoni. Umewasikiliza wagombea wote. Usijiingize kwenye vineno kuwa “ni walewale.” Ni kweli, nyoka aliwaponza wote watambaao; lakini si kila anayetambaa anauma, ana sumu, anaua.

Usijali urefu wa foleni ya wapigakura. Wote hao ni wapiganaji. Mbona wao na wewe mmesubiri kwa miaka mingi ya kuumia? Shiriki kutoa uamuzi: nani akutawale.

Watoto wamemaliza gwaride. Ni mjini Kigoma. Lilikuwa gwaride la saa mbili au zaidi – la kuzima Mwenge. Jua limewakuta uwanjani. Limewawakia hadi linaanza kuwaaga. Wanaonyesha ujasiri na uzalendo.

Lakini posho waliyoahidiwa haitoki. Vifaranga hao wanaandamana hadi kwa mkuu wa wilaya. Naye anauliza: Mnataka nini? Nao wanajibu: Tunataka posho zetu! Naye anasema: Mtalipwa!

Watoto wadogo. Wacheza gwaride. Wanaonja utovu wa uadilifu wa watawala wao. Mpaka vifaranga waandamane ndipo waahidiwe malipo. Kura yako yaweza kusitisha utovu wa uadilifu.

Ulizaliwa Katesh, Sechet, Basotu Basodesh. Unaamriwa kuhama kupisha kilimo cha ngano. Unatupwa nje ya eneo lako. Ni serikali. Wanalima. Wanachoka au wanashindwa. Wanagawa ardhi na kuondoka.

Hawakumbuki kuwa walikung’oa kama gugu. Hawataki kuelewa kuwa umehangaika miaka yote. Kila unapokwenda wanakwambia “rudi kwenu.” Unakuwa mkimbizi ndani ya nchi yako.

Acha mzaha. Piga foleni. Kura yako italeta mabadiliko. Itafuta machozi, jasho na damu iliyochuruzika kutoka mikwaruzo na miti yenye miiba ambamo ulikuwa unakurupushwa – wewe na mifugo yako.

Kura yako ina uzito mkubwa. Ni wewe uliyeishi Loliondo. Ni wewe uliyelinda mbuga na wanyama. Nawe huli nyamapori. Yako ni nyama ya mbuzi, kondoo na ng’ombe. Ungekuwa unakula nyamapori, wanyama wasingekuwepo.

Lakini amekuja “mwekezwaji.” Anatoka Arabuni. Unaamriwa: Toka! Umejiuliza, utoke uende wapi? Mifugo yako imeswagwa na kupotelea porini na nyumba yako imeunguzwa hadi jivu. Unyama.

Kura yako yaweza kuleta mabadiliko. Ndiyo mwamuzi wa nani atakusikiliza, atakujali. Kakae foleni utumbukize kura sandukuni.

Wewe ni mkazi wa Mbamba Bay. Unamwambia rais wa nchi yako kuwa ndani ya nchi yake hakuna huduma, na zile chache zinazopatikana, ni ghali sana. Sasa unataka kuwa unapata huduma zako kutoka Malawi.

Unalia na kusaga meno. Unajuta kwa nini ulizaliwa ulipo – ndani ya nchi yako. Halafu unasema ni jua kali huwezi kusimama foleni kupiga kura?

Kura yako yaweza kuleta uongozi unaojali; hata kama ni kuweka uhusiano mwema kati ya eneo lako na nchi jirani. Kapige kura uondoe manyanyaso.

Mbamba Bay wanataka kuwa Malawi. Mtwara wanataka wawe Msumbiji. Mtukula wanataka kuwa Uganda. Karagwe wanataka wawe Rwanda. Ni mwendo wa kukata tamaa ambao unaweza kuuzima kwa kutumia kura yako.

Kwa miaka mitano sasa au zaidi, unafanya kazi kwenye mgodi wa mkaa wa mawe, bila malipo au kwa “kishika roho” tu. Kwa nini? Waliojipa mgodi hawana fedha za kulipa na wanaona aibu kuuendesha baada ya kutajwa kwenye ufisadi.

Halafu unasema mvua inanyesha huwezi kusimama foleni kupiga kura? Mbona kura yako ni mwamuzi atakayeweka waadilifu madarakani; wanaojali na wenye uchungu na wafanyakazi.

Tulia hapo ulipo. Jaribu kukumbuka Wimbo wa Taifa. Imba kimoyomoyo: “Tanzania, Tanzania, nakupenda kwa moyo wote, nchi yangu Tanzania …”

Inatosha. Angalia kulia kwako. Angalia kushoto. Tupa macho mbele. Geuka nyuma. Unaona nini? Kibanda chako kilichokaa kwa upweke. Wenye nyumba husema mabanda ya aina hii ni “mbavu za mbwa.”

Nenda ukaone au sikiliza simulizi za kweli. Mijini wamejenga mahekalu. Nyumba moja inalingana na shule ya sekondari ya vidato vinne na mikondo miwili-miwili. Humo wanakaa baba, mama, mtoto mmoja na mbwa mkubwa mweusi!

Rudisha macho yako kwenye banda lako. Jaribu kuimba Wimbo wa Taifa. Maneno hayatoki. Ukifanikiwa utaishia kwenye “Tanzania, Tanzania…” Yale ya “…nakupenda kwa moyo wote,” yanakuwa mazito kutamka.

Machozi yanakulengalenga machoni. Hakuna wa kukuliwaza. Ni wewe na familia yako. Ni hali hiyohiyo kwa miaka 50 ya uhuru wa “Tanganyika nakupenda.” Hukupata fursa. Hukuwezeshwa.

Je, unaweza kusema huendi kupiga kura kwa kuwa ni jua kali? Kura yako haitakuwa peke yake. Haitakuwa na upweke wa banda lako. Itakuwa na kura nyingine zinazokataa maisha ya namna hiyo. Amka!

Tume ya Taifa ya Uchaguzi ina kazi moja. Kuweka taratibu, kanuni na kuandaa uchaguzi mkuu kila baada ya miaka mitano au uchaguzi mdogo (marudio).

Ni tume iliyoteuliwa na rais. Rais huyo huwa anagombea kipindi cha pili cha miaka mitano katika uchaguzi ulioandaliwa na Tume yake.

Sasa angalia kazi ya Tume. Kwa miaka mitano haijaweka sahihi orodha za wapigakura. Kuna wanaolalamika kuwa majina yao yamekutwa kwenye vituo viwili.

Kuna waliohamishwa kutoka vituo vyao hadi vituo vingine tena vya mbali. Kuna wanaopaswa kusafiri mwendo wa kilometa 10 kujiandikisha na kurudi (kilomita 20). Vivyo hivyo wakati wa kupiga kura.

Ni makusudi? Ili wananchi wachoke na kuacha kupiga kura? Ni uzembe? Ni kutojali? Hawatoki hawa hadi umeamua. Hakuna cha jua, mvua au umbali. Kapige kura.

Kura yako yaweza kufanya mengi makubwa. Yaweza kuleta mabadiliko. Kapige kura.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: