Kura za kusaka waua Albino: Kielelezo cha polisi kushindwa kazi


Alloyce Komba's picture

Na Alloyce Komba - Imechapwa 18 March 2009

Printer-friendly version
IGP Said Mwema

NAMFAHAMU binafsi Inspekta Jenerali wa Polisi nchini (IGP), Said Mwema tangu nikiwa ripota wa habari za matukio ya kihalifu. Wakati huo, yeye alikuwa Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa [RCO] wa Dar es Salaam, chini ya RPC Alfred Gewe.

Mwema ni kachero mkubwa wa Polisi aliyekuwa anazifanyia kazi taarifa za vyombo vya habari kuhusu uhalifu na wakati mwingine akieleza mbinu za kukabiliana na wahalifu husika kama alivyowahi kunieleza walivyokabiliana na vitendo vya uporaji watu jioni na asubuhi mapema maeneo ya ufukwe wa Feri, Jangwani darajani kwa watu watokao Kariakoo, Fire, Magomeni na Muhimbili.

Mwema, kachero mtulivu na msikivu lakini mfuatiliaji makini, aliwaita askari sita walio chini yake na kuwapangia kazi mbele yangu akiwaelekeza namna ya kufanya huku nao wakichangia mawazo yao.

Baada ya kuongoza operesheni mbili kubwa maeneo ya ufukweni Feri na Jangwani darajani palipokuwa na adha kubwa ya vibaya waporaji watu nyakati za usiku na asubuhi mapema ambayo nilimlalamikia binafsi, na kuniita baada ya siku chache kuniarifu kukamatwa kwa vijana wapatao 40, nikazidisha kiwango cha kumheshimu.

Alishirikiana na makachero wachache tu kukamata vibaka hao wakiwa na aina tofauti ya silaha kama vile visu, mapanga, nondo na nyembe. Walikamata pia misokoto mingi ya bangi.

Mbali na kuzidisha heshima kwake, waliendelea kuwa rafiki zangu akiwa na RPC Gewe, makachero waliofanana katika umakini hususan ufuatiliaji wa taarifa za kihalifu hata kama wamezipata kwa mwendawazimu au mtoto mdogo ombaomba wa mitaani.

Niligundua pia kwamba siri ya mafanikio ya Kamanda Mwema ilikuwa ni jinsi alivyokuwa akishirikisha askari anaofanya nao kazi hata kama ni wa vyeo vya chini.

Utamkuta anaita kwa mfano: “Aisee, Michael (ambaye ni koplo) hebu nisaidie tumkamate vipi huyu jamaa leo hii kwa sababu anasumbua sana wananchi pale Manzese Uzuri. Au tumwache kwanza ajisahau kidogo lakini tukichunga nyendo zake zisilete madhara makubwa?..Ila nataka wewe tu ufanye kazi hii na asijue mtu mwingine!..”

Baadaye kachero Mwema alipelekwa mkoani Mbeya kuwa RPC. Aliimudu kazi yake na hiyo pengine ilimsaidia kuteuliwa kuingia Interpol.

Ipo sasa tofauti kubwa ya kiutendaji akiwa IGP. Jeshi la Polisi linashindwa kupanga mikakati ya kupambana na mauaji ya wenye ulemavu wa ngozi (albino) yaliyoenea mikoa mbalimbali nchini kutokana na imani za kishirikina kwamba watapata utajiri, cheo au mafanikio mengine.

Kwanza, Polisi haijafanya uchunguzi au utafiti makini kujua chanzo cha mauaji haya. Pili, haijafanya uchunguzi au utafiti wa kujua ukubwa wa tatizo, ikiwemo ni maeneo gani hasa ya nchi. Tatu, haijafanya sensa yenye takwimu yakinifu ya kujua idadi ya albino nchini, na nne, ni hatua gani imezifanya za kusaka wauaji, yaani mbinu za kipelelezi.

Alichokifanya Vicky Mtetema, mwandishi wa Shirika la Utangazaji la Uingereza [BBC] kujifanya anataka utajiri kupitia waganga fulani wa jadi katika moja ya mikoa ya ziwa na akaelekezwa na mmojawao akatafute viungo vya albino, ni utafiti huu ninaohoji kama Polisi walifanya.

Hadi leo watu wanauliza kwanini Polisi ilishindwa kufanya ukachero kama huo? Kila mmoja anaweza kuwa na jibu lake. Lakini taarifa ziliopo zinadai kwamba Polisi na vyombo vingine vya usalama havikufurahia kazi ya Vicky.

Nakubali kuwa Jeshi la Polisi linashirikisha wananchi katika kazi yake hasa hivi sasa kwa mbinu ya polsi jamii. Lakini linapaswa kudhibiti uhalifu kwa kukamata wahusika na ushahidi wa kutosha wa kuwatia hatiani. Huo ndio wajibu wake wa msingi.

Rais Jakaya Kikwete na Waziri Mkuu Mizengo Pinda ambao hupata ushauri kutoka kwa wakuu wa majeshi ya ulinzi na usalama, wameamua kuongoza vita dhidi ya maharamia hawa. Tayari utaratibu wa wananchi kupiga kura ya siri ya kutaja wahusika umeanza nchini.

Ni kura ya hatari sana inayoingiza waliomo na wasiokuwemo. Watu hutumia chuki walizonazo na baadhi ya wenzao kuwataja.

Mtu yeyote anaweza kutajwa ingawa kitakachoangaliwa ni idadi ya kura. Na haya ndio matokeo yanayosubiriwa na Polisi wa Tanzania. Ndipo wataingia mitaani kusaka na kukamata watu waliotajwa katika kura hii.

Kwamba leo, Polisi, inayotakiwa kutumia mikakati ya kisayansi katika kutekeleza jukumu lake la kulinda usalama wa raia na mali zao, linaridhia kutumika kwa mkakati wa kienyeji mno na wa hatari katika kutekeleza jukumu hilo, ni jambo la kusikitisha.

Nimeangalia kipindi cha ucheshi cha Star TV Jumamosi na kushuhudia mfano wa hatari ya kura hii. Mtu mmoja alipita mitaa ya kijiji anachoishi na kushawishi wanakijiji wenzake wamtaje mtu aitwaye Kafuru.

Anasema Kafuru amekuwa adui yake mkubwa na ndiye sababu kubwa ya kila matatizo anayoyapata maishani mwake. Alihonga wanakijiji na wapo wengi walimkubalia. Hatimaye walimpigia kura nyingi Kafuru na walipokuja viongiozi wa Wilaya, jina la Kafuru likaibuka miongoni mwa yaliyotajwa sana. Kafuru akashikwa palepale na kufungwa pingu.

Kura ya siri ya kutaja wahalifu ni sawa na kutupa mshale gizani. Huna hakika utampata nani. Kura hii ni kielelezo cha Jeshi la Polisi kushindwa kazi.

0
No votes yet