Kusajili simu ni uhalifu mpya


Ndimara Tegambwage's picture

Na Ndimara Tegambwage - Imechapwa 30 June 2010

Printer-friendly version
Uchambuzi

MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ilipotangaza, kwa niaba ya serikali, kwamba kila mwenye simu ya mkononi sharti aisajili, nilihoji mantiki ya hatua hiyo na kuhitimisha kuwa tunakokwenda ni kubaya.

Ni bahati mbaya kuwa wanaojua umuhimu wa simu hizo hawakusimama nami kupinga hatua ya serikali. Walikaa kimya. TCRA ikaendelea kuhimiza na mwisho wa usajili unapaswa kuwa leo – 30 Juni 2010.

Hoja kuu ya watawala katika biashara ya usajili ni “kukabiliana na uhalifu.” Serikali inadai – pamoja na wale wanaoungana nayo katika kufikiri; au kwa mkumbo tu – kwamba simu za mkononi “zinatumiwa vibaya.”

Kuna fikra kwamba simu hizi zinatumiwa na baadhi ya wananchi (watu) kupanga na wakati mwingine kufanya uhalifu. Hivyo sharti zisajiliwe.

Kwamba kila simu ikiandikishwa, itakuwa rahisi kujua nani aliwasiliana na yupi, juu ya nini na kama ni uhalifu, wahusika watafuatiliwa, kukamatwa na kuchukuliwa hatua.

Kwanza, hatua ya kuhimiza watu kusajili simu, tena bila maelezo sahihi na yanayotosheleza, imesaidia kutangaza biashara ya wanaouza simu za mkononi. Hapa serikali, kupitia TCRA, imekuwa “meneja masoko” wa makampuni yanayouza simu za mkononi.

Siyo rahisi kwa sasa kujua nani alipatana kazi hii na analipwa kiasi gani; au basi ni kiwewe kinachotokana na kutoelewa umuhimu wa mawasiliano na haki ya mtu binafsi kuwa na faragha ya mawasiliano yake na mwenzake.Kwa hiyo, kwa kelele za kauli na vipenga, baadhi ya wananchi wamefikiri kuwa, iwapo hawatanunua simu na kuzisajili leo au kesho, basi hawataweza kumiliki simu milele na milele.

Ushahidi wa hilo ni misururu ya wananchi kwenye vituo vya kusajili simu. Ushahidi mwingine ni hatua ya makampuni ya simu kutangaza mwisho wa usajili kana kwamba ndio mwisho wa dunia.

Ushahidi mwingine ni ule wa makampuni ya simu kuanzisha bahati nasibu za kusajili simu – kujenga kiwewe na harara kwa msaada wa serikali.

Lakini ukweli ni kwamba simu hazileti uhalifu wala hazienezi uhalifu. Kuna wahalifu wengi – mamia kwa mamia, hata maelfu kwa maelfu – ambao hawana simu na hawajawahi kufikiria kuzinunua.

Kuna wengi waliofungwa kwa uhalifu mkuu – mauaji, wizi wa kutumia silaha, ujambazi aina aina – bila kuhusisha simu ya mkononi wala ya mezani. Kuhusisha simu na uhalifu na kutumia hoja hiyo kuhalalisha usajili, ni hatua ya juu mno ya mkengeuko.

Labda tukae tukirudia kuwa uhalifu ni sehemu ya tasnia ya jinai kama zilizvyo tasnia nyingine katika jamii. Uhalifu huendana na kukua kwa fikra za kuukabili. Historia imeliweka wazi hilo.

Kwa kuwa mhalifu ni adui, watu wameunda milango imara na kufuli. Wenye uwezo wamejenga magrili kupambana na uvamizi nyumbani; huku wengine wamenunua silaha za kuwalinda nyumbani na wawapo safarini.

Kukua kwa uhalifu kumeandamana na kukua katika taaluma ya sheria; kujua kulenga hoja mwanana na kuzingatia ushahidi usiotiliwa shaka.

Ni wizi wa fedha na vitu vingine vya thamani, pamoja na upotevu wa aina mbalimbali unaokomaza fikra katika udhibiti na kusababisha kuwepo juhudi za kuelimisha wahasibu na wakaguzi.

Ni kushamiri na hata kukomaa kwa uhalifu kunakokomaza mbongo za mahakimu na majaji; wakizingatia hoja nzito za waendesha mashitaka ili kuadhibu uhalifi.

Lakini pia ni mazingira hayo ambayo yanafanya elimu ya sheria kukua hadi kuwa na maprofesa waliobobea katika eneo la elimu ya jinai na hata kupata maana na tafsiri kadha wa kadhaa za jinai.

Kwa hiyo, huwezi kupambana na uhalifu kwa kusajili simu za mkononi. Hiki ni kisingizio kisichokuwa na mashiko; lakini pia kimekuwa njia nyingine ya kuchochea biashara ya simu za mkononi.

Kusajili simu kwa shabaha ya kupambana na uhalifu ni kukiri kushindwa kutumia mbongo za waliosomea taaluma ya sheria na nyingine katika kukabiliana na tasnia ya jinai.

Kusajili simu, ikiwa njia ya kukabiliana na jinai, ni kudhihirisha kushindwa kwa wanaohusika na kujisalimisha kwa wahalifu na uhalifu. Ilitarajiwa kila mbinu mpya ya uhalifu ilipojitokeza, basi pawepo fikra mpya za kuikabili na siyo kuingilia mawasiliano ya wananchi.

Kuingilia mawasiliano ya watu pia ni kuvunja haki za binadamu. Hapa tunaona nia ya serikali ya kutaka makampuni ya simu za mkononi kuwa zinaipa taarifa zinazopitia kwenye mitandao yao.

Huu nao ni uhalifu utakaotendwa na serikali na makampuni ya simu. Utakuwa unatendwa na watu wanaopaswa kuelewa, kuthamini na kulinda haki za kila mtu katika mawasiliano binafsi na faragha yake.

Makampuni ya simu yatakaposhiriki uhalifu huu, yatakuwa yamekosa hadhi ya kuhudumia wateja wake na yatakuwa yamegeuka sehemu muhimu ya watawala watakaokuwa wakivunja haki za binadamu.

Leo ndiyo ilipangwa kuwa siku ya mwisho kusajili simu. Kinachojitokeza ni kwamba serikali inataka kuharibu bomba la mawasiliano – simu.

Twende taratibu tukijiuliza: Wahalifu watarajiwa wakitumia wenzao kupeleka ujumbe iweje?

Tuwasajili waliotumwa? Nani atawasajili na wapi?

Iweje, pale wahalifu watarajiwa watakapotumia miluzi iliyomo katika ishara maalum wanazoelewa wao kwa wao? Tusajili miluzi? Vipi na wapi?

Kuna watakaotumia kope na ishara mbalimbali. Yuko wapi mtaalam wa kusajili ishara na alama za wahalifu watarajiwa?

Kusajili chombo au njia au mkondo wa mawasiliano hakusaidii kupambana na uhalifu. Kwa nini tusikubali kwamba watawala wanazidi kuwaelemea raia na kwa woga walionao, wanataka kujua wanasema nini na wanafikiri nini?

Woga huu unatokana na watawala kushindwa kupata majibu kwa maswali wanayoulizwa. Wanaogopa hata uvumi na umbeya. Wanakimbia kejeli. Lakini hasa wanaziba mifereji ya taarifa ambazo zingewafikia bila kujua zinakotoka.

Wanataka kujua nani kasema nini? Ili wamfuate. Ili wamkamate. Ili wamvunjevunje. Ili wazime fikra zake. Hasa wanataka kuzima “uasi” ndani ya fikra na kauli zake kabla hazijazaa mbegu. Huu nao ni uhalifu.

0
No votes yet