Kushuka kwa Elimu: Nani wa kulaumiwa?


Thomas Lyimo's picture

Na Thomas Lyimo - Imechapwa 03 March 2010

Printer-friendly version

UKOSEFU wa mitaala inayokidhi mahitaji ya elimu ya kisasa inayoendana na maendeleo ya sayansi na teknolojia, ni miongoni mwa matatizo makubwa yanayozorotesha maendeleo ya elimu nchini.

Mitaala inayotumika kufundishia Tanzania haiwezeshi watoto kupata uwezo katika kufikiri bali zaidi hufundishwa kukariri.

Kwa namna hiyo, watoto wanakosa ufahamu wa mambo mengi na matokeo yake wanamaliza elimu ya msingi bila ya kupata maarifa ambayo ndiyo msingi mkubwa wa mtu kusoma.

Tatizo jingine ni serikali kutojenga mazingira yanayowezesha walimu hasa wa shule za msingi, kufundisha kwa ufanisi. Walimu wengi wamechanganyikiwa kwa kukosa nyenzo muhimu za kufundishia.

Maslahi yao hayatazamwi ipasavyo kiasi cha kukutwa wakihangaika katika kufuatilia. Muda mwingi ambao walipaswa kuutumia kupanga mpango wa kufundisha na kukaa darasani hupotea.

Katika shule nyingi, walimu hawana nyumba za kuishi, tatizo linalolazimisha waishi kwenye nyumba za kupanga ambazo ziko nje ya maeneo wanapofundisha.

Ingawa serikali imeruhusu walimu wajiendeleze, hata wale wachache wanaojitolea kujiendeleza wananyimwa fursa na wakuu wao wa kazi. Wanaendelea kufundisha kwa mazoea wakati mifumo ya ufundishaji inabadilika kulingana na wakati.

Mlolongo huo wa matatizo katika sekta ya elimu, unaashiria kuwa vyombo husika katika kuimarisha elimu nchini havijatiza wajibu wao vizuri.

Ni kwa vipi basi walimu wasioenziwa watalipatia taifa wataalamu wa fani mbalimbali? Haiwezekani.

Walimu hawawezi kujenga wanafunzi kwa kiwango cha kuwawezesha kukabiliana na changamoto mpya na nzito za kufikia maendeleo yanayozingatia sayansi na teknolojia.

Katika shule za msingi kwa mfano, unatarajia watoto wafundishwe namna ya kujenga mawazo ya kutenda na kuzalisha vitu badala ya kufundishwa zaidi kukariri. Huko ni kufundishwa ukasuku.

Mifumo endelevu kama hiyo ya ufundishaji inabidi kuendelezwa pale watoto wanapoingia ngazi ya sekondari.

Matarajio ni kwamba kwa watoto waliotoka shule za msingi watakuwa wameshakua akili na kumudu kudadisi kila kitu badala ya kuwa wasikilizaji tu wa wanachofundishwa.

Vijana wanakosa uwezo wa kufikiri mambo kwa kina, pamoja na kuwa wamemaliza elimu ya chuo kikuu.

Hawawezi kutumia fursa elimu waliyopata kujiletea maendeleo au kubadilisha mazingira mabaya kwa ajili ya mabadiliko ya kweli katika jamii.

Kijana aliyekosa mbinu za kitaalamu za kumfikirisha kuhusu matatizo yanayokabili jamii alipo, hapati ujasiri wa kutatua matatizo yanayosumbua watu.

Hivyo ni vikwazo vya nchi kupiga hatua ya maendeleo iwe ya kiuchumi kuanzia ngazi ya familia hadi taifa, au katika kuimarisha huduma za kijamii: elimu, afya, maji, miundombinu na mazingira.

Haishangazi basi kuendelea kushuhudia viwango duni vya kufaulu mitihani ya kitaifa kwa watoto katika ngazi zote. Matokeo ya mitihani ya kidato cha nne ya mwaka 2009, ni uthibitisho wa hoja hii.

Katika shule ya Rashidi Kawawa, yenye wanafunzi 102; waliopata daraja la nne ni 60 tu; waliobaki 42 wamefeli. Ina maana hata kwa kile kidogo serikali ilichowekeza kwa ajili yao, hakikuzaa matunda.

Nani wa kulaumiwa? Wizara ya Elimu au wazazi? Kila mtu katika taifa ana mchango.

Serikali imeshindwa kutatua matatizo ya walimu hasa maslahi yao na kuwajengea mazingira mazuri ya kikazi. Haijaongeza walimu wenye sifa.

Serikali imeshindwa kutawala utunzi na matumizi ya vitabu na haijasikiliza wadau wa elimu kwa kiwango cha kutosha kufanya uamuzi. Kuna utitiri wa vitabu madukani, je wanafunzi waamini vipi?

0
No votes yet