Kusila, Barongo watuhumiwa


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 25 January 2011

Printer-friendly version

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Dodoma, William Kusila na Katibu wake, Kapteni John Barongo wanatuhumiwa kutumia magari ya chama hicho kwa kazi binafsi.

Hata hivyo, viongozi hao wa CCM wamekana tuhuma hizo wakisema kuwa gari moja linatumika kumchukua mwenyekiti na kumrudisha nyumbani na jingine lilitolewa bure kwa shughuli za kitaifa.

Magari yanayolalamikiwa kutumiwa kibinafsi ni ya Toyota Land Cruiser – moja lenye namba T 643 BJB na jingine namba za usajili T 390 BSL.

Tuhuma ambazo MwanaHALISI imepata zinasema Kusila anatumia gari la chama kwa shughuli za nyumbani ikiwemo kubeba mazao.

Kwa upande wa Kapteni Barongo, tuhuma hizo zinasema amelikodisha gari kwa Sh. 9 milioni kwa ajili ya shughuli za mitihani ya darasa la saba ya mwaka jana.

Magari yote hayo yalitolewa Agosti mwaka jana kwa ajili ya shughuli za uchaguzi mkuu.

Lakini, Kusila alipoulizwa, amekiri kutumia gari la chama kwa shughuli zake na kulilaza nyumbani kwake kwa kuwa anaishi mbali na mjini. Alitaja masafa ya kilometa 44 anakoishi kutoka mjini Dodoma.

Alisema, “Nikiwa natoka nyumbani kwangu huja na kijana wangu dereva na kupakia mazao yangu kwa ajili ya kuyaleta sokoni. Je, unataka nifanye nini wakati mimi ni mkulima?”

Alipoulizwa kama hana ugomvi na katibu wake kuhusu gari hilo, Kusila alisema hana tatizo lolote na Barongo, akisema alimruhusu kulala na gari analolitumia.

Kuhusu gari jingine linalodaiwa kuwa limekodishwa kwa malipo, Barongo aliiambia MwanaHALISI kwa njia ya simu juzi Jumatatu kwamba gari gari hilo liliazimwa kwa Mkurugenzi wa Halmashauri kwa ajili ya shughuli za mitihani.

Alisema chama kilitoa kibali kwa maandishi baada ya kupokea maombi ya mkurugenzi kuomba msaada wa gari ili kufanikisha shughuli za kitaifa zilizokuwepo. Alisema mashirika mbalimbali yaliombwa kutoa msaada kama huo.

Alipoulizwa kama alikodisha gari hilo na kupokea malipo ya Sh. 9 milioni, Kapteni Barongo alisema hakuna gari lililokodishwa bali anachokijua yeye ni kuwa ”gari liliazimwa.”

”Magari haya yalikuwa mawili tuliyopata mwaka jana. Moja liliharibika likabaki moja. Hili zima tulilitoa baada ya kuazimwa na Mkurugenzi wa Manispaa kusaidia shughuli za mitihani,” alisema.

Alisema maombi ya magari yalitolewa kwa mashirika mbalimbali mkoani kwa barua. Tulijibu barua kukubali na tukawapa na dereva. Tumefanya hivi kwa barua ambayo ipo,” alisema.

Alisema, ”ninachojua mimi ni kuazima gari na kibali tulitoa gari walitumie kwa shughuli za mitihani. Hakuna malipo.”

Tuhuma zilipokuja, ilielezwa kwamba makao makuu ya CCM yalisambaza magari aina ya Toyota Land Cruiser katika ofisi zake za mikoa na wilaya kwa ajili ya kusaidia kufanya kazi za uchaguzi mkuu na baadaye magari hayo kutarajiwa kutumiwa na viongozi wa chama katika shughuli za chama.

“Magari hayo yalifikishwa ofisini Agosti mwaka jana, mpaka sasa yamekuwa yakilala nyumbani kwa mwenyekiti Kusila, nje kidogo ya mji wa Dodoma, bila kujua kama kulikuwa na makubaliano na katibu wake Barongo,” kilisema chanzo cha habari hizo.

Magari hayo yamekuwa yakilala nyumbani kwa viongozi hao na kufanya kazi za nyumbani na amekuwa mkali pale linapohitajika kufanya shughuli za chama.

Chanzo hicho kinasema Kusila amekuwa akitumia madereva wawili tofauti, mmoja anajulikana kwa jina moja la Seif, ambaye alikuwa dereva wake wakati akiwa mbunge.

Dereva huyo hulipwa posho ambayo angepaswa kulipwa dereva aliyeajiriwa na chama.

Chanzo  hicho kilisema mtu mwingine anayetumika kuendesha gari hilo ni mfanyakazi wake wa nyumbani anayelitumia kusombea mazao kutoka kijijni.

Taarifa kutoka ofisi hiyo zinasema Kapteni Barongo alikodisha gari hilo kwa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma kusambaza na kukusanya mitihani ya darasa la saba iliyofanyika Septemba 6 na 7 mwaka jana.

Inadaiwa Kapteni Barongo alilichukua kwa kuandika barua kuwa limetolewa bure kusaidia shughuli za mitihani, lakini maelezo ya ndani yalidai gari hilo lilikodiwa na kulipwa fedha kama magari mengine yaliyokodiwa.

Mtoa habari alisema mara baada ya kumalizika shughuli za mitihani, chama kililipwa Sh. 9 milioni kama malipo ya kukodi gari hilo pamoja na matengenezo yake.

Mara baada ya kumalizika shughuli za mitihani, dereva huyo mwajiriwa wa CCM, alitakiwa kukabidhi gari ofisini makao makuu ili mwenyekiti wake Kusila aendelee kulitumia.

Wakati kampeni zikiendelea, habari kutoka Manispaa ya Dodoma zilivuma kuwa gari hilo pamoja na magari mengine, yalilipwa fedha za kukodiwa, zikiwamo fedha za matengenezo hali iliyowatia shaka viongozi wengine wa juu wa CCM Mkoa.

Uhakika wa gari hilo kulipwa fedha za kukodiwa na matengenezo ulijidhihirisha pale Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Dodoma ilipoanza kufuatilia gari hilo na mengine ili kujua ni kiasi gani kila gari lililipiwa kama kodi na matengenezo.

TAKUKURU ndiyo iliyokuwa ya kwanza kufichua siri ya gari hilo kukodiwa na kulipiwa malipo ya kodi na matengenezo baada ya ofisa wake kufika ofisi za CCM Mkoa zaidi ya mara mbili kutaka wapatiwe barua na risiti zilizoonyesha malipo hayo.

Mpango wa kulipwa malipo hewa unaonekana kufanywa na Ofisa Elimu anayetajwa kuwa ni mke wa Kapteni Barongo. TAKUKURU inafuatilia kujua kama malipo yaliyofanywa kwa magari hayo ni halali.

Naibu Mkurugenzi wa TAKUKURU mkoani Dodoma, Sosthenes Kibwengo, bila kutaja kama gari la CCM mkoa lilihusika katika shughuli za mitihani ya darasa la saba, alikiri kuwa taasisi hiyo inayafanyia uchunguzi magari zaidi ya 10.

“Taasisi yetu imelifanyia kazi suala hilo, ni kweli kwamba maofisa wetu wapo katika uchunguzi wa magari yaliyotumiwa na manispaa katika shughuli za mitihani ya darasa la saba… lakini siwezi kukwambia ni nini tumepata,” alisema Kbwengo.

Kibwengo anasema wao watapeleka taarifa ya uchunguzi wao TAKUKURU makao makuu mara uchunguzi utakapokamilika.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: