KUTEKWA ULIMBOKA: Tume huru kutoka jeshi lisilo huru!


Kondo Tutindaga's picture

Na Kondo Tutindaga - Imechapwa 04 July 2012

Printer-friendly version
Uchambuzi

TUKIO la kutekwa na kuteswa kwa kiongozi wa Jumuiya ya Madaktari, Dk. Steven Ulimboka litatuvua nguo kama taifa.

Daktari huyo amekuwa katika mvutano wa muda mrefu na serikali katika harakati za kutetea hali bora za kazi na maslahi ya madaktari.

Kwa nyakati kadhaa amekutana na viongozi wa kitaifa wa sasa na wa zamani. Na siyo siri kuwa, kiongozi yeyote wa serikali mwenye udhaifu katika hoja na nafsi isiyojiamini, atapata tabu sana kuzungumza na Dk. Ulimboka katika masuala ya msingi.

Ni kwa sababu hiyo, sikushangazwa na taarifa za usiku wa manane kuwa ametekwa na “watu wasiojulikana” na kupelekwa “mahali pasipojulikana.”

Kutekwa na kuteswa kwa mtu mwenye msimamo mkali dhidi ya utawala wowote, huwa ya kawaida kwa tawala nyingi zisizojiamini; lakini pia ni hatua ya mwisho ya utawala unaodai kujiamini lakini ukiigiza kujiamini.

Kuteka raia au mpinzani wa mfumo, ni silaha ya kawaida itumiwayo na tawala dhalimu zisizopenda kukosolewa.

Sasa limekuwa jambo la kawaida kwa serikali yetu kuwawinda wanaoitwa wapinzani wa mfumo kwa njia mbalimbali zikiwamo za kuwahonga, kuwagawa, kuwafukuza kazi.

Msitu wa Mabwepande ulianza kupata sifa mbaya mwaka 2006. Huko ndiko haki za watu zinakanyangwa kwa kutumia mtutu wa bunduki na vitendo vingine vya kinyama.

Mwaka huo, miili ya wafanyabiashara watatu wa madini kutoka wilaya ya Ulanga waliochinjwa kwa risasi ya polisi ilitupwa. Huko pia ndiko Dk. Ulimboka alitupwa baada ya kupigwa karibu ya kufa.

Katika sakata hili la kutekwa na kuteswa kwa Dk. Ulimboka mmoja wa watuhumiwa ni serikali yetu. Hii ni kwa mujibu wa viwango vya kawaida vya upelelezi, ambavyo hata serikali yenyewe kupitia jeshi la polisi huwa inavitumia.

Mathalani, ukitokea ugomvi wa muda mfupi au mrefu kati ya wanandoa, majirani na hata ndugu, na kwa bahati mbaya mmoja wa hao akafa katika mazingira ya kutatanisha, mtuhumiwa wa awali huwa ni yule mgomvi mwenzake.

Mara nyingi utasikia polisi wakitangaza kuwa fulani “anaisaidia polisi” wakiwa na maana kuwa yuko mikononi mwa polisi, akihojiwa ili kubaini chanzo cha kifo cha mgomvi mwenzake.

Dk. Ulimboka, akiwa kiongozi wa madaktari amekuwa na ugomvi na serikali. Ugomvi huu umedumu kwa muda mrefu.  Sasa Dk. Ulimboka ametekwa na kuteswa karibua kufa. Ni wazi watesaji wake walilenga kumuua.

Kwa msingi wa mazoea ya kiuchunguzi katika kesi za namna hii, ilitarajiwa kuwa serikali iwe mikononi mwa polisi “ili kuisaidia polisi,” sawa tu na kesi nyingine zote zinavyoendeshwa.

Tumesikia serikali, kupitia jeshi la polisi, wanaunda tume ya kuchunguza suala hili. Serikali na jeshi la polisi ni watuhumiwa wa kujaribu kumuua Dk. Ulimboka, watawezaje kuchunguza sakata hili?

Sina maana kuwa hakuna watuhumiwa wengine, ila  kwa uzoefu wetu wa siku zote katika masuala haya, watuhumiwa wengine wangefuata baadaye au  pamoja na serikali.

Wanaharakati wamedai hawana imani na tume ya polisi kwa sababu haiko huru. Serikali au jeshi la polisi wanadai tume hiyo ni ya wataalamu na ni huru.

Uhuru huo kwa jeshi la polisi mbele ya serikali umetoka wapi na umeanza lini? Ikiwa vyombo vinavyotamkwa kuwa huru na katiba haviko huru, jeshi la polisi ambalo ni sehemu ya serikali litapaje uhuru wa kuichunguza serikali?

Si muda mrefu tumesikia kilio cha jaji mkuu kilichodai uhuru wa mahakama haupo kwa sababu watendaji wa serikali wamo ndani ya tume za utumishi wa mahakimu.

Aidha, jaji mkuu aliyepita, Augustino Ramadhani, aliwahi kusema uhuru wa mahakama unakuwa mashakani endapo fedha za kuendesha mahakama hiyo zimo mikononi mwa serikali.

Tumekuwa tukishuhudia ziara za ghafla za wakuu wa dola katika vyombo hivyo na kuashiria kuingilia mhimili huo wa utoaji haki.

Hata katika sakata hili la mgomo wa madaktari, tumeshuhudia Spika wa Bunge, Anne Makinda akizima mjadala wa sakata hili kwa madai kuwa suala hilo liko mahakamani. Lakini muda haukupita mrefu, tukamsikia Rais, Jakaya Kikwete akilijadili suala hili na kupitisha hukumu kuwa madaktari kama hawataki kurudi kazini waondoke na hakuna malipo kwa madai yao.

Uhuru wa mahakama uko wapi ikiwa rais anatoa hukumu wakati suala liko mahakamani? Narudia tena, ikiwa uhuru huo umekosekana mahakamani, polisi watapata wapi uhuru huo ili wachunguze suala la kutekwa kwa Dk. Ulimboka?

Serikali hii yenye kasoro nyingi katika masuala ya utoaji haki, inawezaje kushughulikia suala hili kwa uwazi na ukweli? Kisingizio cha usalama wa taifa mara zote hujitokeza yanapofika masuala tete kama hili.

Tumeshuhudia serikali ikikubali kushindwa mahakamani na kulipa fidia kwa wafiwa wa watu fulani waliokufa katika mazingira ya kutatanisha kama hili la Dk. Ulimboka.

Serikali inaweza kuwa tayari kulipa fidia kwa familia ya Dk. Ulimboka kuliko kuendelea kulumbana naye katika mgomo wa madaktari.

Na kwa maoni yangu, ningedhani ingekuwa bora kwa serikali kukubali uchunguzi huru juu ya suala hili, ili hata ukweli ukipatikana kuwa ni serikali ilihusika, basi ilipe fidia kuliko “kituko” hiki cha serikali kuwa mtuhumiwa halafu ikajichunguza yenyewe.

Ukweli ni kwamba serikali haina miundombinu wala utashi wa kujikamata yenyewe ikiwa mtuhumiwa namba wani.

Na kama kuna mtu ndani ya serikali aliyeidhinisha tendo hili lakini bila ridhaa ya wakuu wa serikali, basi imchukulie hatua za wazi ili kujiosha na kashfa hii mbaya.

Haitakuwa mara ya kwanza katika taifa letu kufanya hivyo. Kashfa ya kuuawa wafungwa mkoani Shinyanga iliwagharimu waziri wa mambo ya ndani na wakuu wengine wa vyombo vya usalama.

Hapa tunazumgumzia utekwaji wa Dk. Ulimboka kwa mtutu wa bunduki za serikali! Kama hili halifanyiki, ni bora wana harakati wote na wenye maoni tofauti na mfumo wa serikali ya sasa, waanze kutafuta hifadhi za ukimbizi katika nchi nyingine maana yaelekea kilichomtokea Dk. Ulimboka ni tangazo la awali.  Makubwa yaja siku chache zijazo.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: