Kuteua tu nalo ni tatizo?


Ezekiel Kamwaga's picture

Na Ezekiel Kamwaga - Imechapwa 16 June 2010

Printer-friendly version
Waraka wa Wiki

SEPTEMBA mwaka jana, serikali ilitangaza kuwa nafasi ya Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) iko wazi.

Nilishangaa kusikia wiki iliyopita kwamba Mama Margaret Munyagi, aliyekuwa mkurugenzi mkuu wakati tangazo hilo likitolewa na sasa muda wake umemalizika, anaendelea kukaimu nafasi hiyo hadi leo.

Sasa ni takribani miezi tisa tangu kutolewa kwa tangazo hilo la serikali. Mama Munyagi anakaimu nafasi hiyo kwa miezi tisa!

Huu, pasipo kukwepesha neno, ni uzembe. Kama Mama Munyagi ni mtendaji mzuri, serikali ingeamua tu kumuongezea mkataba tangu wakati huo.

Kama serikali imeona kwamba mama huyo hafai, ingetafuta mtu mwingine wa kuendesha chombo hicho nyeti kwa usalama wa anga letu.

TCAA ndiyo imepewa dhamana ya kuangalia taratibu za usafiri wa anga nchini zinafuatwa. Katika dunia ya sasa ambapo usafiri wa anga umekuwa muhimu kuliko katika kipindi chochote tangu kuumbwa kwa dunia hii, ni ajabu kwamba serikali haijui kuwa kuna nafasi ya wazi inahitaji kujazwa.

Katika hali ya kawaida, mtu hawezi kutekeleza wajibu wake ipasavyo wakati tayari akijua kwamba yeye anakaimu tu nafasi hiyo.

Hawezi kufanya maamuzi yoyote ya mwisho. Hawezi kuadhibu. Hana meno na hawezi kuwa na ushawishi wa kutosha wakati linapokuja suala lolote lenye kuhitaji uamuzi mzito.

Na tatizo hili halipo TCAA pekee. Hata kwenye Shirika la Magazeti ya Serikali (Tanzania Standard Newspapers), wachapishaji wa magazeti ya serikali kama Daily News na HabariLEO, hali iko hivyohivyo.

Kwa zaidi ya nusu mwaka sasa, shirika hilo nyeti kwa serikali halina mtendaji mkuu. Aliyepo sasa, Mkumbwa Ally, anakaimu tu nafasi hiyo.

Aliyekuwa akishikilia nafasi hiyo, Isaac Mruma, amewekwa benchi tangu mkataba wake ulipomalizika. Nafasi haijajazwa na kumbuka hiki ndicho chombo kinachotakiwa kuwa mdomo wa serikali.

Hali ilikuwa hivyohivyo kwa Tanesco kwa zaidi ya nusu mwaka pia. Tangu muda wa Dk. Idris Rashid ulipomalizika, Tanesco ilikaa kwa walau miezi sita bila ya kuwa na mtendaji mkuu.

Ni wiki mbili tu zilizopita ndipo serikali ilipoona umuhimu wa kumteua William Mhando kuchukua nafasi ya Dk. Rashid.

Yaani imeichukua serikali zaidi ya miezi sita kupata mtu wa kuchukua nafasi ya utendaji mkuu wa shirika lake pekee la umeme!

Kuna mifano mingi sana ambayo naweza kuitoa kuhusiana na tatizo hili la kuchelewa kufanya uteuzi katika taasisi za serikali.

Zaidi ya serikalini, nina mifano pia ya balozi mbalimbali za nchi yetu ambazo nyingine zimekaa zaidi ya mwaka mmoja au miwili bila ya balozi.

Matokeo yake maofisa wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wamekuwa wakienda kufanya kazi za muda katika baadhi ya balozi na kulipwa posho nene na serikali.

Hasara hii yote ingeweza tu kuepukwa kwa kufanya uteuzi mapema. Lakini inaonekana hata kufanya uteuzi limekuwa suala gumu kwa serikali yetu.

Katika siku za nyuma, nilikuwa miongoni mwa wale waliokuwa wakihoji ubora wa wale waliokuwa wakiteuliwa kushika nyadhifa fulanifulani.

Nilikuwa nasema sana wakati mtu aliyesomea fani ya ufundi mchundo alipoteuliwa kuongoza hospitali au daktari alipoteuliwa kuongoza shirika la ndege.

Lakini sasa naona kuna tatizo kubwa zaidi; tatizo la kushindwa “hata kukosea” kwa kuteua viongozi wasiofaa. Serikali imeamua sasa kuachia taasisi zake zitembee kama mbuzi waliokata kamba.

Kwa mujibu wa kitabu cha Kenny Orton Kuhn; The Leadership Gap, kuna hasara kwa taasisi kuongozwa na watu ambao wanajua wako mahali hapo kwa muda tu.

Lakini kuna hasara mbili kubwa zaidi ambazo Kuhn alizieleza ndani ya kitabu kile nilichokisoma miaka minne iliyopita.

Kwanza, “makaimu” wanaweza kuamua kutofanya chochote ili mradi wasubiri muda wao upite. Hawa wanaweza wasifanye baya au zuri lolote kwa kampuni au taasisi yoyote husika.

Hawa wako mahali wanapitisha muda tu. Katika taasisi nyeti kama Tanesco na TCAA ambazo zina malengo ya muda mrefu, si rahisi kuelewa ni kwa vipi “kaimu” wa kupitisha muda tu anaweza kupata nafasi.

La pili ni ukweli kwamba kaimu anaweza kuamua kuharibu. Kama ni fisadi, anaweza kufanya ufisadi ambao haujawahi kuonekana.

Ndiyo yale mambo ya kiongozi mpya kuingia madarakani na kukuta akaunti zote zina fedha sifuri. Hili nalo lipo.

Kama ndugu yangu Stephen Mabada aliyekuwa akikaiumu nafasi ya Dk. Rashid angeamua kukamua akiba ya Tanesco, sidhani kama Mhando angekuwa na uwezo wa kuweka mafuta kwa magari yanayotumika kukatia umeme wadaiwa sugu wa shirika hilo hivi sasa.

Jambo moja la wazi ambalo linasemwa katika kitabu hicho ni kuwa kiongozi wa kukaimu hawezi kufanya lolote la maana kwa taasisi husika. Afanye ili sifa ziende kwa mwingine baadaye?

Kama sote tunakubaliana katika hili, maana yake ni kwamba utendaji wa sasa katika TCAA, TSN, Tanesco, kwingineko na katika balozi zetu, utakuwa umeshuka kwa kiwango fulani.

Pengine kinachoiokoa serikali na uzembe huu ni ukweli kuwa wakati mwingine ni vigumu kupima athari za ukaimu.

Pengine akaunti zitaonekana bado zina fedha za kutosha. Pengine wafanyakazi watakuwa wanalipwa mishahara yao kama kawaida pamoja na bili nyingine.

Lililo wazi, na hili ni lazima tuliseme kwa nguvu ni kwamba hakuna taasisi au idara yoyote itakayoendelea kwa kukaimiwa nafasi kubwa za utendaji.

Nakubali kwamba ni vigumu kuona athari za matatizo ya ukaimu katika mwaka husika. Tatizo hili litakuja kutuumiza sana huko mbele ya safari. Tutaona tu.

Lakini, kwa nini tufike huko? Kwani serikali yetu tuliiweka madarakani kwa ajili ya kufanya nini? Kazi yao kubwa si ni kuongoza?

Sasa kama wanashindwa kutupa hata uongozi tu, tunaweza kutegemea nini kingine kutoka kwao?

0
No votes yet