Kutokujali kwa watawala ndiko kunaimarisha nguvu ya umma


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 16 November 2011

Printer-friendly version
Uchambuzi

TAKRIBAN watu 400 walitiwa nguvuni jijini Mbeya mwishoni mwa wiki iliyopita baada ya wafanyabiashara ndogondugo maarufu kama wamachinga kupambana na polisi wakipinga uhuni uliozoeleka wa mamlaka za halmashauri za serikali za mitaa kuwafukuza kwenye eneo lao la biashara la Mwanjelwa.

Tukio la Mbeya linafanana kwa kila kitu na tukio jingine kama hilo lililotokea hivi karibuni katiba jiji la Mwanza wakati wamachinga walipopambana na mgambo wa jiji hilo na polisi. Dar es Salaam yamekuwa matukio ya kawaida mno.

Wakati wamachinga wakipambana na vyombo vya dola, umati wa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ulipambana na polisi walipotaka kwenda Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) kudai fedha zao za mikopo.

Matukio yote mawili, ya Dar na Mbeya, yamesababisha watu 83 kushitakiwa kwa makosa yanayofanana, Mbeya watu 33 na Dar es Salaam watu 50.

Aidha mashitaka haya yanafanana na yaliyofunguliwa dhidi ya wafuasi 20 wa CHADEMA Oktoba 28 mwaka huu. Wafuasi hao pamoja na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, walishitakiwa kwa makosa matano ya kukusanyika pasipo kibali, kuhamasisha watu kufanya vurugu, kutokubali amri halali ya polisi, kula njama kutenda kosa na mkusanyiko usio halali.

Ukitazama kwa makini kidogo utagundua kuwa kuna kitu kimoja kinazidi kuota mizizi nchini. Hiki si kingine ila ni nguvu ya mapambano, kukataa kuburuzwa na kukataa majibu mepesi kwa maswali magumu.

Inawezekana hadi sasa watawala wanaamini kwa dhati ya mioyo yao kwamba wanaweza kabisa kudhibiti hali hii kwa kutumia nguvu. Kwa kutumia mabomu ya kutoa machozi, maji ya kuwasha na kila aina ya nyenzo.

Akili ya namna hiyo ni matokeo ya kwenda likizo katika mambo mawili; moja, kuwa likizo kifikra, pili na baya zaidi kuwa likizo ya hali halisi ya yale yanayotokea katika jamii kila uchao.

Kwa sasa harakati hizi zimetawaliwa na kuendeshwa na vijana, aghlabu wenye umri kati ya miaka 15 hadi 35 hivi. Wote hawa wana hasira kuu. Wamechoka na kukataa tamaa kwa sababu kila leo inayokuja kwao ni afadhali ya jana.

Hawana tena tumaini, si wanafunzi walio masomoni, si wachuuzi mitaani, si kwa wasikokuwa na kazi kwa kuwa wote hawaoni mbele kuna matumaini gani, ni kiza kinene kimetanda.

Vijana hawa wana uwezo wa kushiriki maandamano na kila aina ya mapambano dhidi ya dola kwa sababu hawaoni njia nyingine ya kuwasilisha kutokukubaliana na mambo mengi yanayoendelea ndani ya nchi.

Hawana matumaini kuwa sehemu ya jamii inayonufaika na rasilimali au keki ya taifa. Wana hasira kali, wanataka kupambana kama njia ya kubainisha chuki na kutokukunaliana na hali ya mambo ilivyo.

Kundi hili la vijana hata kama serikali ikitumia jeshi la polisi saa 24 siku saba kwa wiki kuwadhibiti, bado wataibuka washindi kwa sababu wana jambo muhimu na la kweli wanalopigania. Haki. Haki yao ya kuwa wadau halali wa kunufaika na keki ya taifa imesiginwa siku nyingi.

Kwa wale ambao walitarajia kuwa wasomi wamejikuta wanasukumwa pembeni mwa mchakato wa kupata elimu hiyo. Kisa, hawana sifa za kukopeshwa. Waliokopeshwa mikopo ni ya kijungu jiko tena inatoka kwa mbinde.

Wazazi wao hawana uwezo wa kuwalipia chochote cha maana, wamekunja migongo hadi sasa basi. Hali ni mbaya kuliko inavyoweza kuelezwa.

Kwa hiyo, wasomi hawa hasira yao ya kuwekwa kando haina tofauti kubwa na wamachinga wanaoshinda juani kutwa wakisaka wateja, ambao hawaendi na hata wakienda hawako tayari kununua kwa bei ya kuwahakikishia faida, ni mwendo wa kukatishana tamaa, matokeo yake wanaishia tu kuambulia vijisenti vya kulinda uhai usiachane na mwili kwa sababu ya njaa. Hakuna nafuu.

Ndiyo maana tunapotafakari na kujiona kama taifa, kwamba sisi si sehemu ya mataifa ya Kiarabu ambako sasa moto unawake, tunafikiri tuko salama. Tunasahau kukumbuka kuwa kilichowaunganisha wale vijana wa Tunisia ambao walianzisha mageuzi makubwa yaliyokuja kupewa jina la mapinduzi ya jasmine, nguvu yao ni hiki kinachowaunganisha wamachinga wa Mbeya, Arusha, Mwanza na hata wanafunzi walio tayari kupambana na askari kwa kuwa hasira yao imefika juu.

Ni kiongozi gani nchini kwa sasa anaelewa hasira ya vijana hawa? Hayupo. Ndiyo maana akili zao ambazo zimeachwa kwenda likizo wanatazama hali hii na uhusiano wa harakati za CHADEMA.

Lakini hawajiulizi kwa nini CHADEMA waungwe mkono kiasi hicho na vijana hawa? Je, wanawahonga? Je, wanagawa chakula kwenye maandamano yao? Je, vijana wanalazimishwa kushiriki katika harakati hizo? Jibu ni jepesi tu, hapana. Wanajiunga kwa ridhaa yao kwa kuwa wanakubaliana na kile wanachohubiriwa. Haki zao kuporwa na kikundi kidogo cha watawala.

Katika nchi ambayo imeendesha mgawo wa umeme kwa zaidi ya miezi tisa sasa kudhani kwamba hasira ya vijana ni ya kuchochewa na mtu ni upofu mkubwa wa kutazama hali ndani ya jamii ilivyo.

Mgawo wa umeme ukiunganishwa na mfumo wa ovyo kabisa wa kuifikia keki ya taifa unawafanya wamachinga wote; vinyozi, wauza maji baridi, soda, wachomea vyuma, wachonga magrili, waendesha saluni zote, waendesha vijiwe vya kupiga chapa na foto kopi na hata waliokuwa wanaendesha vibanda vya kuonyesha sinema uswahilini, kujikuta hawana kazi kwa kiwango na tija ile ya kuwako kwa umeme. Hali hii majibu yake ni kujengeka kwa hasira.

Kujengeka kwa hasira ni jambo moja, lakini jambo la pili ni utayari, umakini na ubunifu wa watawala kutambua kwamba hali kama hiyo imezidi kuota mizizi ndani ya nchi, na kwa maana hiyo kuchukua hatua za kuishughulikia hasira hiyo kwa kuondoa vitu vinavyoileta.

Kwa bahati mbaya hakuna anayeona. Hasira inaachwa iwe utamaduni na iwe mfumo wa kukabiliana na kila kitu.

Tunisia yule kijana aliyejilipua kwa moto, aliwakumbusha wenzake kwamba njia iliyobakia ni hiyo tu, kama hawaitaki basi wawaondoe wote waliowafikisha hapo.

Mbeya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimenyooshea kidole mgambo wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya, na wametaka wadhibitiwe, wamegundua kuwa kuwasambaratisha wamachinga, kupora bidhaa zao, kuwakimbiza kama wanyama waharibifu wa mazao shambani, hakika hakutibu machungu na njaa za wamachinga, sana sana ni kuzidi kuwajengea hasira. Hali hii bila shaka ndiyo inazaa moyo wa kukataa kuburuzwa, moyo wa kuamua kupambana na polisi. Huku ndiko tunakoelekea kujenga, kuimarisha na kurasimisha nguvu ya umma kuleta ukombozi wa pili.

0
No votes yet