Kwa jezi ya Ronaldo, roho ya Kikwete kwatu


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 24 March 2010

Printer-friendly version
Michezo

BAADA ya wadau mbalimbali wa soka kuandika makala na chambuzi kupinga gharama kubwa kwa ajili ya ziara ya klabu ya Real Madrid na hatimaye serikali kutangaza kuifuta ilifikiriwa suala hilo limekwisha.

Wadau wa soka walikuwa na shauku ya kuwaona nyota wa klabu hiyo tajiri duniani wakija nchini kukipiga katika uwanja mpya wenye hadhi sawa na viwanja vya Ulaya.

Ilifikiriwa pia ingekuwa njia ya kuutangaza uwanja huo ili baadhi ya timu zinazokwenda Afrika Kusini ziweke kambi nchini. Kilichosababisha wadau wengi kuipinga ziara hiyo ni kutokana na ukweli kwamba gharama za kuwaleta nchini ni kubwa.

Kwanza msafara wao ulitarajiwa kuwa wa watu 80 na pili msafara huo ulipaswa kulipwa posho. Kwa kuangalia gharama zilizopangwa kwa ziara ya Real Madrid bara la Asia, kilitakiwa kiasi kikubwa.

Wadau walipendekeza kiasi hicho cha gharama ambacho kilitarajiwa kutolewa na wadhamini wa ziara hiyo kipelekwe Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa ajili ya maandalizi ya Taifa Stars iliyokuwa inajiandaa kwenda Kombe la Mataifa ya Afrika Ghana mwaka 2008 au Angola na Afrika Kusini mwaka 2010.

Hatimaye ziara ikafutwa na maandalizi ya nguvu ya Taifa Stars yakaanza kuonekana. Kumbe wadau walipigwa mchanga wa macho; mwanzilishi wa mpango wa ziara hiyo, Rais Jakaya Kikwete bado alikuwa na mikakati yake na sasa roho imetulia baada ya hivi karibuni kuzawadiwa jezi ya mshambuliaji wa klabu hiyo, Ronaldo kutoka Ureno.

Rais ambaye ni maarufu kama JK bado alikuwa na mipango nao; ‘ziara’ ikafanyika Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Adam Kimbisa akageuka ghafla kuwa Mkurugenzi mtendaji wa Real Madrid, Hugo Sanchez akazungumza Kihispaniola akamkabidhi jezi ya Ronaldo, Rais Kikwete.

Hafla ikafana, wakapeana mikono ya kupongezana na bila shaka wakazungumzia namna vibopa wa Real Madrid akiwamo Kimbisa wanavyokusudia kuibadili soka ya Tanzania. Mwishowe wakanywa mvinyo kwa furaha.

Wadau wa soka waliona kuwa hicho ni kituko na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) lilisubiri hadi Jumamosi iliyopita kuitangaza habari hiyo katika kipindi chake cha ‘Visa na Vituko’.

Kwa nini? Kwao, tukio zima la kutumwa jezi hiyo na mantiki yake lilikuwa kituko. Anayekabidhiwa ni Rais wa Tanzania na anayekabidhi ni Meya wa Jiji la Dar es Salaam. Vipi?

Waliona hakuna uhusiano wowote wa jezi hiyo na maendeleo ya soka ya Tanzania. Nani aliileta jezi hiyo nchini? Kwa nini mtu aliyeileta hakupewa fursa ya kukabidhi mwenyewe?

Hivi, Real Madrid waliofuta ziara hiyo mwaka 2007 bado walikuwa wanasubiri Cristiano Ronaldo wa Ureno ahamie ndipo watengeneze jezi kwa ajili ya kumzawadia JK? Hata jezi hiyo imesafirishwa kwa shilingi za Kitanzania? Hapo ndipo tumefikia kwamba hatuoni hata mambo yanayotushushia hadhi. Sasa kama nchi tumefaidika vipi na jezi hiyo?

Kwa wasomaji wapya, taarifa za kusudio la serikali kuileta nchini Real Madrid zilitolewa kwa mara ya kwanza na JK Oktoba 2, 2006 alipozungumza na wahariri Ikulu.

Alitoa taarifa hiyo ya kuvutia kwa wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari akisema awali timu hiyo ilitakiwa kuja kufungua uwanja mpya wa michezo mapema mwaka 2007, lakini akasema ziara imeahirishwa kutokana na kubanwa na mashindano ya ligi yao Primera Liga na michuano ya kimataifa.

Mkutano huo na wahariri ulifanyika siku chache baada ya JK kurejea nchini akitokea ziara ndefu ya Marekani. Alisema walipokuwa Madrid wakisubiri kuunganisha ndege alitembelea makao makuu ya Real Madrid ambako alipokewa na Mkurugenzi mtendaji wa klabu hiyo, Sanchez.

Alisema kuwa kusudio lake lilikuwa kuialika Real Madrid kuja nchini katika ufunguzi wa uwanja mpya wa michezo uliokuwa umepangwa kufanyika Februari au Machi 2007.

Alisema licha ya klabu hiyo kuupokea mwaliko huo kwa furaha walijibu wasingeweza kufika kwa kuwa wakati huo watakuwa katika mashindano.

Kwa mujibu wa JK, uongozi wa Real Madrid ulisema kuwa unaweza kuileta timu hiyo Julai au Desemba wakati wakiwa mapumzikoni, wakati hali ya hewa kwao ikiwa ya baridi, hivyo Julai ndio mwezi unaofaa.

JK alisema ili kuhakikisha Real Madrid inakanyaga ardhi ya Tanzania, amekubali sharti la timu hiyo la kutafuta wadhamini wa safari hiyo.

Mpango mzima wa ziara ulifurahiwa na wapenzi wa soka nchini kutokana na shauku ya kutaka kuwaona nyota wa klabu hiyo tajiri duniani. Lakini kauli kwamba wanahitajika wadhamini kugharimia safari yao ilitibua kila kitu; wadau hao hao wakapinga vikali.

Itakumbukwa kwamba, mara baada ya JK kushinda urais kwa kishindo mwaka 2005, alianza safari ya kujitambulisha kwa jamii ya kimataifa, kutangaza vivutio vya nchi na kwa namna ya ajabu kutafuta kocha wa mpira wa miguu. Aliomba marais wenzake wamsaidie.

Halafu, bila maelezo yanayoeleweka bayana akawa anaonekana kwenye klabu nyingi akipokea jezi kama vile za Newcastle England na Los Angeles Lakers ya Marekani. Na hivi karibuni ameonekana akipiga picha na wacheza sinema wa Marekani

Alipokuwa Marekani kupokea tuzo iliyotolewa na shirika moja kutambua mchango wa afya, alipata bahati ya kuonana na mwenyeji wake Rais Barack Obama. Kwa Bernard Membe, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa hiyo ilikuwa sifa kubwa.

Katika mazungumzo yao Ikulu ya White House, Obama aliyekuwa anajiandaa kuzungumza na Ulimwengu wa Kiarabu mwishowe alimpa jezi za mpira wa kikapu na akamtaka auendeleze mchezo huo na awavutie Watanzania kucheza Marekani.

Wakati wanajadili suala la mpira wa kikapu, tayari kulikuwa na Mtanzania, Hasheem Thabeet ambaye anacheza huko. JK hakujua.

Matukio yote hayo yalishutumiwa na wapenzi wa michezo (wanasiasa walishutumu kwa kujificha) nchini kwa madai hazikuwa na uhusiano wa moja kwa moja katika maendeleo ya mpira wa miguu isipokuwa utalii.

Pengine baada ya kuelemewa na shutuma hizo JK alibadili mbinu za kusaka umaarufu kupitia soka. Ilipofanya ziara ya michezo ya kirafiki nchini mwaka huu, timu ya taifa ya Ivory Coast ‘The Elephants’ ikiwa na nyota kadhaa akiwemo nahodha Didier Drogba wa Chelsea ya England akawafanyia dhifa na kumteua Drogba kuwa balozi wa heshima.

Ivory Coast waliodai wangetwaa ubingwa wa Kombe la Mataifa ya Afrika ungekuwa kwa heshima ya Mlima Kilimanjaro. Loo, walitolewa mapema sawa na ‘vidampa’ New Zealand walioweka kambi nchini walipokuwa wanakwenda Afrika Kusini kwa michuano ya Kombe la Mabara mwaka jana.

Turudi nyuma, baada ya JK kushutumiwa kupora majukumu ya TFF, alikaa kimya, serikali ikapanga uwanja huo kufunguliwa na Rais wa China Hu Jintao kimya kimya. Hakukuwa na mechi hata ya Twiga Stars na Dar Combine. Kwa nini? Hasira?

Akasubiri kuwashangaza Watanzania kwa kupewa jezi ya Real Madrid na Kimbisa. Kwa hiyo roho ya JK iko kwatu kwamba lile alilotaka kulitimiza mwaka 2007 kuileta Real Madrid amefanikisha kwa njia nyingine (kupeperushiwa jezi) mwaka 2010?

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: