Kwa mabango haya, hofu au JK hajulikani?


mashinda's picture

Na mashinda - Imechapwa 22 September 2010

Printer-friendly version
Tafakuri

Kama ilivyo ada, wananchi kwa ujumla wao wametumbukia kwenye jadi yao , wanacheza ngoma waijuayo vizuri. Ni msimu wa kucheza ngoma ya kuongopewa, ahadi nyingi, kuvalishwa fulana, khanga na kofia, zilizosheheni majina ya wagombea.

Kadri siku zinavyokaribia uchaguzi mkuu ndivyo mitaa inazidi kupambwa kwa mabango ya picha za wagombea, harakati za mabango ni kubwa, ipo mitaa na barabara nyingine mtu ukipita unajiuliza maswali magumu kidogo; kwamba nguvu kubwa namna hii ya kusaka kura ni ya nini? Na je, nani analipia mabango na picha zilizozagaa kila kona?

Huko nyuma tulizoea kuona ushindani wa mabango ukiwa miongoni mwa makampuni ya simu za mkononi kwa nia ya kutawala soko la biashara; lakini inapokuwa ni kwa watu wanaosaka ofisi ya umma, utumishi, mtu anashindwa kupata majibu kwamba nguvu kubwa kiasi hicho ni ya nini?

Pengine inaweza kueleweka kwa wagombea wapya ambao hawajulikani kwamba wanajitahidi kufahamika kwa wananchi. Kwa maana hiyo hutumia nguvu nyingi ya mabango ni mbinu ya kujitambulisha kwa wepesi zaidi.

Lakini sasa inapokuwa rais aliyeko madarakani ndiye anayeongoza kwa juhudi za mabango, picha, mtaa baada ya mtaa, barabara baada ya barabara inakuwa vigumu kuwa na majibu kama nia ni kujitambulisha kwa wananchi tu.

Miongoni mwa vijisababu vilivyotolewa na makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kukwepa mdahalo wa wagombea urais, hususan kauli ya Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba na Mwenyekiti wa Timu ya Kampeni ya Rais Kikwete, Abdulrahman Kinana, ni kwamba mgombea wao anajulikana, hana sababu ya kuingia katika mdahalo.

Sasa swali linakuwa kama mgombea wa CCM anajulikana, jambo ambalo halina ubishi kwa sababu amekuwa rais tangu mwaka 2005-2010, sasa mabango yote haya ni ya nini?

Lakini si hilo tu, juhudi hizi za kuwa na rundo la watu wanaopita huko na huko kusaka kura kwa niaba yake ni za nini, je, Kikwete mwenyewe hatoshi?

Kuna msafara wa Mgombea Mwenza, Dk. Mohamed Gharib Bilal ambao unachanja mbuga kama wa mgombea urais mwenyewe; lakini kuna msafara mwingine wa mke wa Rais, Mama Salma, ambao nao unachanja mbuga kukutana na wanawake nchini kote; zote hizi ni gharama.

Pia, Rais Kikwete ni wa ghali sana. Kwa mfano akiwa mkoani Kilimanjaro mgombea huyo msafara wake ulikuwa na helikopta tatu. Ile maana ya kumpunguzia uchovu sasa inageuka kuwa mbwembwe za kuwakoga wananchi.

Kwa nini CCM inashindwa kuonyesha hisia za huruma kwa wale wanaowaomba ridhaa ya kutawala huku wakionekana fika kwamba wamegubikwa na lindi la umasikini?

Nilisikiliza uzinduzi wa kampeni za chama cha NCCR-Mageuzi viwanja wa Tanganyika Parkers, Kawe jijini Dar es Salaam . Kiongozi mmoja katika mkutano ule aliwakumbusha wananchi waliokuwa wamejitokeza kusikiliza kampeni zile kwamba tangu serikali ya awamu ya nne iingine madarakani Desemba 2005, hakuna bidhaa ambayo haijapanda bei zaidi ya mara dufu.

Alitaja sukari kutoka kilo moja Sh. 450 hadi sasa 1,200, kibiriti kutoka Sh 20 hadi sasa Sh. 50, unga wa sembe kutoka Sh. 200 hadi sasa zaidi ya Sh. 550, alitaja mlolongo mrefu, lakini la msingi ni kuonyesha kwamba maisha ya watu wetu yamekuwa ya dhiki zaidi kuliko ilivyokuwa mwaka 2005. Haya yote yanasema jambo moja tu, gharama za maisha hazishikiki. Watu wetu wamepigika.

Katika hali hii umma kwa kweli ulitarajia kuona kwamba harakati za kampeni zinafanana na hali halisi ya watu wetu. Ukweli huu ndio umekuwa unazungumzwa mara nyingi juu ya vipaumbele vyetu, swali kuu limekuwa ni kweli kama taifa hatuna uwezo, hatuna fedha hatuna namna au shida ni kwamba ni kwa jinsi gani tunatumia kile kilichopo?

Ni kawaida kabisa kwa viongozi wetu kuishi maisha ya ukwasi wa juu hata kama kuna mbadala ambao hakika hauvunji uheshimiwa wake.

Wakati vyama vya siasa vinajadili kanuni za sheria ya gharama za uchaguzi kulikuwa na tatizo kubwa la kutokuelewana juu ya gharama halisi ambazo vyama vitatumia kusaka kura, wapo waliotaka bilioni 40, lakini wapo waliopendekeza kiwango cha mwisho kwa mgombea urais kisizidi Sh. bilioni tano.

Kama nia ya matumizi haya ni kuwafikia wananchi, je, katika zama za sasa ambazo mawasiliano yamerahisishwa zaidi kupitia njia kama za simu za mikononi, ikikisiwa kwamba Tanzania ina watumiaji wa simu hizo milioni 15, huku waliojiandikisha kupiga kura wakiwa ni takribani milioni 19 tu, je, njia hiyo si ingekuwa rahisi na gharama nyepesi kuwafikia walengwa?

Lakini la muhimu zaidi, mtandao wa televisheni nao umekuwa mkubwa nchini; je, njia za mijadala ya wazi, ambayo ingeruhusu wananchi kuuliza maswali moja kwa moja kwa wagombea si ingepunguza zaidi gharama hizi pia na kuwafikiwa wananchi kwa wingi zaidi?

Kila ninapotafakari napata ganzi kama kweli taifa hili litafika kokote kwa taratibu hizi za matumizi ya kufuru, hata kama mbinu mbadala zingesaidia kuokoa fedha nyingi.

Ikumbukwe kwamba katika taifa ambalo bado mambo yake hayako wazi sana , nyingi ya fedha za kampeni zinaweza kuwa zinachotwa kwa mlango wa nyuma kutoka Hazina. Tujiulize kama kwa mwendo huu umasikini na uduni wa watu wetu vinawapasua roho za watawala wetu.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: