Kwa maridhiano, Amani Karume moto


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 06 October 2010

Printer-friendly version

KWA kuangalia hali halisi ya mwenendo wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka huu, nathubutu kusifia utekelezaji wa dhamira ya maridhiano katika siasa za Zanzibar.

Lakini hata kabla sijapiga hatua kuendelea na makala yangu leo, namtaja Rais Amani Abeid Karume kuwa ndiye mhimili mkuu wa usimamizi wa utekelezaji wa maridhiano hayo.

Rais Karume, kiongozi wa Zanzibar anayemaliza muda wake kikatiba wa kuiongoza nchi yetu, sehemu muhimu ya Jamhuri ya Muungano, anaongoza vizuri maridhiano yaliyofikiwa pamoja na kiongozi mkuu wa upinzani Zanzibar, Maalim Seif Shariff Hamad.

Viongozi hawa wawili walianza kurudisha nyoyo zao kufikiria zaidi maslahi ya nchi badala ya vyama vyao, pale walipokutana kwa mara ya kwanza kwa faragha tarehe 5 Novemba mwaka 2009.

Mkutano wao uliofanyika Ikulu ya mjini Zanzibar ukawa ufunguo wa kufuta siasa za chuki na hasama na zilizojaa fitna na hasadi, na kukaribisha siasa safi, zinazolazimisha maridhiano ya pande zote.

Kwa jicho la kawaida, viongozi hawa utasema wako katika kiwango sawa cha mamlaka. Ni kweli wote ni wanasiasa wazoefu, wenye ushawishi mkubwa kwa watu wanaowasikiliza na kuwaamini. Hili halina ubishi.

Ila kipo kitu kimoja Rais Karume amemzidi Maalim Seif. Rais Karume ana mamlaka ya kikatiba kuongoza maridhiano waliyoyafikia baada ya kukutana mara kadhaa na kujadiliana, maridhiano ambayo hatimaye yaliidhinishwa kisheria na kikatiba na viongozi wawakilishi wa wananchi kupitia Baraza la Wawakilishi.

Karume ni rais wa Zanzibar, amiri kwa vikosi maalum vya ulinzi vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, mteuzi mkuu wa viongozi wa kisiasa na watendaji katika serikali, na kadhalika yeye ndiye mlinzi mkuu wa amani kwa watu wa Unguja na Pemba.

Kwa mantiki ya mada hii, Rais Karume ana kitu kingine cha ziada: Utashi wa kisiasa wa kuthibitisha imani aliyopewa na wananchi mara tu baada ya kufikiwa kwa maridhiano.

Rais Karume ameamua na katika kuamua kwake, hataki mchezo. Ingekuwa kitu cha kulinganishwa katika kupima kiwango cha msimamo, basi anafanana na bahari juu ya uchafu.

Kimaumbile, bahari haipendi uchafu wowote. Baharini kukiingia mafuta yanabaki juu, hayawezi kuruhusiwa kupenya chini; baharini kukiingia taka, za aina yoyote ile, zinabaki juu ya maji.

Bali hatimaye, uchafu wote unaofanikiwa kubaki juu, unasukumwa ili ufike kule ambako utadhibitiwa vizuri na kupunguzwa ukali wake ambao ukiachwa utaathiri mazingira ya bahari yenyewe na viumbe wanaoitumia.

Uchafu wa baharini unapelekwa ufukweni. Ule ulio mzito kama vile vyombo vya baharini vinavyopotea njia, basi hupelekwa chini ambako akili za binadamu zinawatuma kuzamia na zana za kisasa kuvitoa juu ili kukinga uharibifu.

Sasa kwa maridhiano ya kisiasa aliyoyafikia na Maalim Seif, Rais Karume yu bahari ambayo haipendi uchafu na inaushughulikia uchafu unapotokea kwa kuutupa kunakostahiki.

Tangu maridhiano yafikiwe, Rais Karume ameonyesha dhamira ya kweli kuyatekeleza. Kwa kutambua wajibu alionao kikatiba na kiutu, amesimama kidete kusimamia utekelezaji wa maridhiano haya.

Nimesema Rais Karume ana mamlaka ya kidola ya kuongoza usimamizi na utekelezaji wa maridhiano. Kama kiongozi mkuu wa Zanzibar, anajua akiyumba tu, maridhiano yamepigwa kumbo. Dhamira ya kutandika siasa safi na kuzitumia kuijenga upya Zanzibar, itafutika.

Hataki kufikia hapo. Anaonyesha dira kwa kuyaongoza maridhiano. Ni haki yake, ni wajibu wake. Lazima aonyeshe utiifu kwa ahadi aliyoiweka mbele ya wananchi, mbele ya viongozi wenzake wa kila namna, na mbele ya Mwenyezi Mungu aliyemuumba.

Ndivyo wanafalsafa wanavyoamini kwamba kiongozi mwenye mamlaka ndiye mwenye wajibu zaidi wa kusimamia utekelezaji wa jambo lolote ambalo amelikubali na walio nje ya mamlaka. Yeye ana kila kitu cha kuelekeza na kuongoza utekelezaji.

Aliye nje ya mamlaka, hata kama ana umma unamtii – kama ambavyo Maalim Seif anao – atasema tu maana kwa siasa chafu za ki Afrika, mtu kama huyu na umuhimu wake katika kusukuma demokrasia istawi na neema ienee, watendaji serikalini, humpuuza. Si wanasikiliza tu bwana wao!

Ukiangalia hali unagundua kwamba bado ameshika hatamu za uongozi. Kile anachoamini kinasaidia kutekeleza vema maridhiano anakitamka na kuagiza watu wake wakifanye. Na naona kinafanyika.

Mengi tunayasikia mitaani na katika midomo ya watu walio karibu naye, lakini pia kutoka kwa watu wanaodhani Rais Karume amepotea njia.

Tunayachukua yote. Tunachukua yale mazuri na kuyahimiza yaendelee; lakini tunayachukua hata mabaya ya kuyarudisha kwa mamlaka yashughulikiwe kwa sababu isipokuwa hivyo, dhamira ya maridhiano itapigwa kumbo.

Inafurahisha kampeni zinakwenda vizuri. Hakuna aliyeguswa. Ilipotokea mtu ameguswa, hatua za kisheria za kurekebisha zinachukuliwa. Zaidi kinachotia moyo ni kukuta katika kuchukua hatua, hakuna muhali unaozingatia itikadi za kisiasa, hali iliyokuwa imeota mizizi.

Kwa mfano, walipotokea watu wachache na kuchana picha za mgombea urais kwa tiketi ya CUF, Maalim Seif, mhusika alishughulikiwa na kwa uharaka. Tukio kama hilo lilipotokea kwa picha ya mgombea urais wa CCM, Dk. Ali Mohamed Shein, hatua ilichukuliwa. Zipo kesi chache mahakamani kuhusu uhalifu huu.

Hata pale mtu alipotamani picha ya Dk. Shein iondolewe kwenye nyumba yake kwa sababu hakutoa idhini ibandikwe hapo, ilifuatiliwa na ikaondolewa. Ni haki yake na Kituo cha Polisi walipoelezwa kuhusu haki ya mtu huyu, walielewa na kuondoa nia ya kumshitaki.

Hizi ndio siasa Wazanzibari wanazihitaji. Ukweli, uwazi, uungwana, uadilifu na maelewano. Wanaamini ndizo zinajenga nchi, zinajenga uchumi wa nchi na zinawaweka katika nafasi nzuri wao wananchi kujenga uchumi wa familia zao na kuchangia katika uchumi wa nchi.

Haya ni mambo ya maana sana kwa hatua iliyofikia Zanzibar kwa sasa. Kulinda kwa nguvu zote halali mafanikio yaliyopatikana. Hii ndio maana ya kuendesha siasa kwa kutambua haki na wajibu.

Hakuna vijana wahuni waliopachikwa jina la Janjaweed ambao wamehilikisha wananchi wengi katika uchaguzi uliofanyika 2000 na 2005 Zanzibar. Jitihada za kufufua kambi za vijana hawa zinapingwa na inafurahisha kusikia hata Dk. Shein ana msimamo kwa hili. Hataki uhuni katika siasa. Swadakta.

Tunakwenda vizuri hakika. Na hii ndiyo njia ya kushika. Unaotakiwa ni uchaguzi huru na wa haki na ambao utakuwa umemridhisha kila mtu wakiwemo wagombea ili siku ya matokeo pasitokee hitilafu.

Ni muhimu Rais Karume na mgombea wake wa CCM, Dk. Shein wakaendelea hivyo kwani wakiruhusu mipango ya kuhujumu maridhiano, watakuja kusutwa na wananchi, watasutwa na ulimwengu, watasutwa na muumba. Watapotea.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: