Kwa mwendo huu kweli Pinda kachoka


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 04 July 2012

Printer-friendly version
Tafakuri

WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda ni mwanasiasa na pia ni mwanasheria, lakini vitu hivyo viwili vimeshindwa kumsaidia kutekeleza wajibu wake. Hawezi kama mwanasiasa na kama mwanasheria.

Kadri siku zinavyopita ndivyo Pinda ama anavyozidi kudhihirisha kuwa amechoka au anakwepa kuwajibika. Ukimtazama usoni unapata jibu, kwamba amechoka kwa maana ya siha ya mwili, lakini pia ukitafakari kwa kina majibu yake bungeni yanadhihirisha ukweli huo. Kachoka.

Jumatano iliyopita Pinda aliliambia Bunge kuwa serikali ingetoa tamko juu ya mgomo wa madaktari. Akiwa ameonyesha kuchoka alisema watachukua maamuzi kama serikali na kama wasemavyo Waswahili ‘liwalo na liwe’.

Kesho yake, Juni 28, wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa papo, alipoulizwa juu ya maana ya kauli yake ‘liwalo na liwe’ baada ya kutokea kadhia ya kutekwa na kupigwa vibaya Mwenyekiti wa Jumuiya Madaktari, Dk. Steven Ulimboka, na kauli ya serikali juu ya mgomo wa madaktari, Pinda alisema kuwa aliposema kuwa liwalo na liwalo, alikuwa anakusudia kuwa alitambua kuwa atalaumiwa kwa kuzungumzia mgomo wa madaktari kwa kuwa suala hilo lilikuwa mahakamani.

Kwa hiyo alijua kuwa angelaumiwa kwa kushindwa kuheshimu mgawanyo wa madaraka katika mihimili mitatu ya dola.

Pia ni katika kujibu swali hilo alilokuwa ameulizwa na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, alisema hata lile tamko la serikali aliloahidi jana yake yaani Juni 27, lisingetolewa tena bungeni kwa sababu ameshauriwa na wasaidizi wake serikalini kwamba suala hilo bado liko mahakamani na ni vema wakaiachia mahakama iendelee na wajibu wake.

Hata hivyo, siku tatu baadaye, yaani Jumapili ya Julai mosi, mwaka huu Rais Jakaya Kikwete, akihutubia taifa katika hotuba yake ya mwisho wa mwezi wa Juni, siyo tu alifanya kile Pinda alikuwa anaogopa kusema bali pia aliingia kwa mapana yake kuuzungumzia mgomo wa madaktari.

Nimepata shida sana kujua Pinda alikuwa anakimbia nini kuzungumzia mgomo huo kama alivyofanya bosi wake kwani kuelezea hali halisi ilivyo na hatua iliyofikiwa sikuelewa na hata sasa sijui inaingilia vipi uhuru wa mahakama.

Kwa hali hii, Pinda siyo tu aliamua kukaa kando na suala la madaktari kwa kisingizio cha kesi kuwa mahakamani, bali pia alionyesha kuwa hapangi majibu yake sawa sawa bungeni.

Pinda ni Waziri Mkuu pekee wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwahi kulia bungeni. Hata kama yalikuwa machozi ya kudhihirisha machungu aliyokuwa nayo kuhusiana na mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino), bado alipaswa kujieleza aliposema wanaoua albino nao wauawe alikuwa na maana gani akiwa ni kiongozi wa serikali inayooamini katika utawala wa sheria. Huenda machozi yalikuwa mbinu mpya.

Kadhalika, Pinda amekuwa waziri mkuu wa kwanza Tanzania kushuhudia wabunge wakijaribu kuanzisha hoja ya kupiga kura ya kutokuwa na imani naye kwa jambo moja tu, kushindwa kuwasimamia mawaziri kiasi cha serikali kujiendea tu kwa kila waziri kufanya atakalo.

Ni kweli jaribio la hoja hiyo ambayo wabunge 72 walijitokeza wakiwamo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), iliishia njiani kwa sababu mbalimbali; kwanza, Spika wa Bunge, Anne Makinda, kuonyesha tangu awali kuwa hakubaliani na mchakato huo; pili, maamuzi ya Rais Kikwete ya kuwaondoa mawaziri sita na naibu wawili katika baraza lake na kuteua wengine nalo lilipunguza hasira za wabunge.

Hata hivyo, bado jaribio hili limemwacha Pinda akiwa ametikishwa, siyo yule wa hapo kabla. Nini maana ya matukio yote haya yanayomzunguka Pinda?

Ni vigumu kuingia ndani ya moyo au kichwani mwa Pinda kujua nini hasa kinamsukuma hadi kuwa ‘mpole’ au ‘mwepesi’ kiasi hili.

Vyanzo mbalimbali vya habari ndani ya Ofisi ya Waziri Mkuu vinasema kuwa Pinda siyo mtu anayefurahia madaraka aliyo nayo kwa sasa kwa sababu anadhani kwamba kila mtumishi wa umma angeliwajibika kwa kadri ya nafasi yake mambo yangekwenda.

Lakini mambo hayaendi hivyo, matokeo yake Pinda anadhani kuna mtu nje ya madaraka yake ambaye anastahili kuja kumsaidia kuwafurumsha watu hao. Hili halimpi raha!

Mbunge wa Ubungo (CHADEMA), John Mnyika, alifukuzwa bungeni kwa kusema kuwa “Rais Kikwete ni dhaifu.” Alishikiwa bango na Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai, baada ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi, kutoa hoja kwamba kauli ya Mnyika ilikuwa ya kumdhalilisha Rais kinyume cha kanuni za Bunge. Mnyika alitakiwa kufuta kauli yake, alikataa na kufukuzwa bungeni siku hiyo.

Mbunge wa Singida Mashariki (CHADEMA), Tundu Lissu, naye alimfikisha Pinda kwenye kona mbaya baada ya kumtaka ajiuzulu kwa sababu ahadi yake kwa taifa hili kwamba mgomo wa madaktari ulikuwa unatafutiwa ufumbuzi na kwamba usingejirudia tena, lakini katika kipindi cha miezi mitatu tu, hali imekuwa ile ile.

Pinda aligoma kujiuzulu. Lissu alimwambia Pinda wazi kuwa amefeli kama Waziri Mkuu.

Kwa nini nimekumbushia haya yote kuhusu Pinda? Ni kwa sababu moja tu, kwamba katika mazingira ambayo umma umekwisha kuamini kwamba Rais Kikwete ni dhaifu, Waziri Mkuu ambaye alitarajiwa afurukute naye amekuwa dhaifu zaidi kuliko hata Rais wake; ni vigumu kuitazama serikali ya awamu ya nne na kushindwa kwake katika mambo mengi bila kumtaja Pinda.

Ni Pinda aliyepata kuaminisha Watanzania kuwa serikali ilikuwa na madaktari wanajeshi ambao wangeliweza kuchukua nafasi ya madaktari raia waliokuwa wamegoma mapema mwaka huu, kwa bahati mbaya madaktari hao kwanza idadi yao ilikuwa ndogo sana, lakini pia hawakufua dafu kwa kazi iliyoko pale Muhimbili. Walishindwa!

Juzi Pinda kasema tena kuwa watawaelekeza madaktari walioko wizarani na wale waliostaafu kurejea Muhimbili kuwahudumia wagonjwa.

Pinda anajua fika kwamba hilo halitawezekana, na muda si mrefu ukweli utajulikana kama ilivyo sasa huduma katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na Taasisi ya Mifupa (MOI) zimesimama kwa kuwa madaktari bingwa wameungana na madaktari wadogo katika mgomo usiokuwa na ukomo.

Ninapomtazama Pinda na kuona amepwaya sikusudii hata kidogo kumwondolea mzigo bosi wake, Rais Kikwete, ila ningependa watu sasa waanze kumtazama Pinda kama sehemu ya matatizo ya serikali ya awamu ya nne.

Unyenyekevu wake na kujipachika jina la mtoto wa mkulima, kama havibadilishi hali ya mambo serikalini na kuwafanya watu wachape kazi, havisaidii kitu.

Kukwepa kuwa mkali na kuamini kwamba muda utapita na kila kitu kitapita, siyo mbinu na mkakati mzuri kwa mwenye nafasi kama ya Pinda.

Tunawajua mawaziri wakuu waliopita katika ofisi ya Pinda na kuacha historia iliyotukuka, kuacha utendaji usiotiliwa shaka. Tunatamani sana Pinda angetumia taaluma yake ya sheria na uanasiasa wake kuleta mabadiliko, kuipeleka mchakamchaka serikali, kuleta tija na uwajibikaji ambao Watanzania wanaulilia kila uchao.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: