Kwa nini ajali za majini zitaendelea


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 28 March 2012

Printer-friendly version

INGAWA ajali za meli kama m.v. Spice Islander I husababisha maafa makubwa baharini, vyombo vidogo huchangia asilimia 78.6 ya ajali zote.

Taarifa ya Mamlaka ya Usimamizi wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra) inasema hili linatokana na meli kuwa chache, wakati vyombo vidogo na ambavyo havitambuliwi na mamlaka hayo, ni vingi na hubeba abiria na mizigo mingi.

Ajali nyingi zimehusishwa na vyombo kutokidhi ubora unaohitajika, hali mbaya ya hewa; upakiaji abiria na mizigo kuzidi kiwango; na vyombo kuendeshwa na wafanyakazi wasio na sifa au uzoefu unaostahili.

Taarifa ya Sumatra iliyotiwa saini na Meneja Mawasiliano, David Mziray, inataja sababu nyingine kuwa ni kusafiri usiku na bila vifaa vya kuongozea chombo na kukwepa kutumia bandari na mialo rasmi.

Sumatra imesajili jumla ya meli 90; kati ya hizo 50 ziko Bahari ya Hindi, 34 Ziwa Victoria, nne Ziwa Tanganyika na mbili Ziwa Nyasa. Mamlaka inakadiria kuwa vyombo vingine vipatavyo 50,000 vinafanya safari majini nchi nzima.

Maelfu mengine ya vyombo vya usafiri kwenye mialo na bandari ndogo na ambavyo vinabeba abiria maelfu kwa maelfu viko nje ya orodha na mamlaka ya Sumatra.

Kwa msingi huu, Sumatra hawana takwimu za kuthibitisha vyombo vilivyopo; wala hakuna mpango mkakati wa kudhibiti ajali nje ya duara lao dogo. Takwimu zilizopo ni za ajali za meli katika rejesta yao tu tangu mwaka 2006.

Katika mahojiano na wadau wa tasnia ya usafiri majini, MwanaHALISI limeambiwa kuwa miongoni mwa sababu kubwa za ajali ni uzembe wa mabaharia, kutotii sheria, ukosefu wa elimu ya usalama kwa abiria, ”rushwa na kujali fedha zaidi” kuliko huduma na uhai wa abiria.

Sumatra hata hivyo, inataja vyanzo vya ajali za meli kuwa ni ubovu wa meli unaochangiwa na umri mkubwa na matengenezo yasiyokidhi viwango. Haitoi orodha ya aina ya matengenezo wala viwango vyake.

Mamlaka hayo yanasema, katika kipindi cha Januari 2006 hadi Desemba 2010, kulikuwa na matukio 54 ya ajali zilizosababisha vifo vya watu 237 na 662 kuokolewa.

Takwimu zinaonyesha kuwa mwaka 2006 kulikuwa na jumla ya ajali tano zilizoua watu 57; mwaka 2007 kulikuwa na ajali 11 zilizoua watu 20 na mwaka 2008 watu 71 walikufa katika ajali 12.

Mwaka 2009 kulikuwa na ajali 13 zilizoua watu 35 na mwaka uliofuata, watu 54 walikufa katika ajali 13. Hivyo, kwa wastani, kila ajali moja iliyosababisha kifo (2006 – 2010), ilipoteza maisha ya watu wanne.

Ajali 21 zilitokea Ziwa Viktoria, mbili katika Ziwa Tanganyika, moja katika Ziwa Rukwa na 28 katika Bahari ya Hindi. Ajali mbili zilitokea katika mito ya Ruvuma na Rufiji.

Kwa upande wa vifo vilivyotokana na ajali hizo, 126 vilitokea katika Ziwa Viktoria, 44 katika Ziwa Tanganyika, 40 katika Bahari ya Hindi na 8 katika Ziwa Rukwa.  Vifo 10 vilitokea Mto Ruvuma na vingine tisa katika Mto Rufiji.

Kwa jumla, Ziwa Viktoria ndiko kumekuwa na matukio mengi ya vifo ambapo katika kipindi cha tathimini ni asilimia 53 ya vifo vyote.

Mikakati ya Sumatra iko katika kushughulikia ajali za meli na siyo vyombo vidogo ambavyo ni vingi; visivyo na magati maalumu na visivyofuata taratibu zake za kujikinga na ajali.

0
No votes yet