Kwa nini Kikwete hataki kura 350,000?


Ndimara Tegambwage's picture

Na Ndimara Tegambwage - Imechapwa 12 May 2010

Printer-friendly version
Uchambuzi

WANAOJALI watakumbuka kwamba katika historia ya siasa za ushindani, hakuna anayedharau kura moja.

Ni hivi: Katika ushindani ulio kwenye uwanja linganifu – kama mteremko basi mteremko kwa wote; kama mwinuko basi mwinuko kwa wote; na kama makorongo basi makorongo kwa wote – hakuna awezaye kupuuza kura moja.

Mtu hawezi kupuuza kura moja kwa kuwa kila anayepiga kura anapaswa, kwa mujibu wa sheria, kupiga kura moja tu kwa mtu mmoja.

Katika mazingira haya, ukiona anayetaka kugombea urais anasema hajali hata kama watu 350,000 watamnyima kura, basi ujue kuna jambo.

Lakini hivyo ndivyo alivyosema Rais Jakaya Kikwete wiki iliyopita; na Kikwete ni mgombea mtarajiwa wa Chama Cha Mapinduzi, kwa jina jingine, CCM.

Aliwaambia waliotambulishwa kuwa ni “wazee wa Dar es Salaam” kuwa kama madai ya wafanyakazi ya kutaka kima cha chini cha mshahara kiwe Sh. 315,000 ni shinikizo ili wampe kura, basi hataki kura zao.

Historia ya mfumo wa vyama vingi haikumbuki lini mwanasiasa aliuambia umati kuwa hataki kura zao. Haikumbuki kwa kuwa hizo siyo kauli za wanasiasa.

Hata katika mfumo wa chama kimoja cha siasa – pale wananchi walipotakiwa kusema “Ndiyo” na “Hapana,” ikiwa na maana ya ndiye huyuhuyu na hapana mwingine; hapakujitokeza jeuri ya kiwango hicho.

Na jeuri ya aina hiyo haiwezi kujitokeza katika mwaka wa uchaguzi. Haiwezi kuonekana pale ambako kuna “utaratibu wa kweli na wa haki” unaotambua uamuzi wa wapigakura.

Haiwezekani ubabe wa aina hiyo ujitokeze katika kipindi ambamo kila mmoja anapaswa kuwa “ombaomba” hata mbele ya yule ambaye alimtimulia vumbi jana na hata mnyonge aliyemwacha bila msaada.

Badala yake, jeuri ya aina hiyo huweza kukutwa kwenye mazingira yaliyoandaliwa tayari ya “kushinda kwa njia yoyote ile,” hata kama siyo kwa kura; au kwa kura zilizopatikana kwa njia yoyote ile.

Hiyo yaweza kutokea pia katika mazingira ya kidikiteta ambamo watawala hawaombi ridhaa za wananchi au ambamo kauli zinaimba demokrasi lakini vitendo ni udikiteta mtupu.

Sasa fanya kama una uwezo wa kumtuma kazi “Mwenyezi Mungu.” Mwambie akuchotee kilichokuwa rohoni mwa Jakaya Kikwete, Jumatatu, tarehe 3 Mei pale alipoona kura za watu 350,000 kuwa si lolote si chochote.

Naye Mkuu wa Wakuu na Mfalme wa Wafalme ataripoti kwa ukweli usiotiliwa shaka kuwa, asiyetaka kura huku anashindana kwa njia ya kura, tayari ana kura za kutosha.

Utashangaa. Utauliza Mkuu wa Wakuu, ilikuwaje mtu akashiba kura hata kabla ya kupiga kura; naye atakwambia: “Na tazama, nje ya ufalme wangu, wametenda kinyume cha haki na utashi wenu.”

Mungu hawezi kubadilisha hili kwa muujiza wake. Analirudisha kwa watu. Anasema wametenda “kinyume cha haki na utashi wenu.”

Kwa maana hiyo Mungu anawaambia watu wachukue hatua na kuhakikisha haki yao inapatikana na utashi wao unatimia na kuheshimika.

Hapo ndipo watu wataanza kujiuliza msingi wa Kikwete “kutotaka” kura laki tatu na nusu katika mfumo unaosema mtu akikuzidi kwa kura moja, basi tayari ameshinda.

Ni utawala wa CCM wa awamu ya tatu uliobadili Katiba ili iseme kuwa mshindi ni aliyekupita na siyo lazima yule aliyepata nusu au zaidi ya nusu ya kura zote.

Haya yalikuwa mabadiliko legelege na zoazoa. Yalilenga kutumia umaarufu wa chama kikongwe huku yakifunga pingu uwezekano wowote ule wa vyama vingine kukusanya kura zao na kuunda serikali ya pamoja.

Katika mazingira ya Katiba kutoruhusu vyama kuunganisha kura na kuunda serikali, ulizaliwa uwezekano wa chama kuingia ikulu kikiwa na hata asilimia 30 ya kura zote alimradi ndicho kinaongoza.

Utaratibu huu, unaoweka uwezekano wa asilimia 30 kukoromea asilimia 70 za wapigakura, siyo tu ni wa kizembe, bali pia ni hatari. Huu ni mgodi wa migogoro na kaburi la utawala bora.

Kwa hiyo katika mfumo ambamo kila mmoja anapiga kura moja, inatia wazimu kufikiri jinsi gani anayetaka kura anaweza kupuuza kura za watu laki tatu na nusu.

Rais alisema hawezi kushinikizwa na wawakilishi wa idadi hiyo ya wafanyakazi. Lakini kundi hili ni mwakilishi tu. Ni moja ya makundi ambayo hayaridhishwi na mwenendo wa serikali katika suala la ajira na malipo.

Kwa msingi huo, kwa rais kukana wanaolia njaa na wanaotaka mabadiliko kupitia kundi moja, tayari amekana mamilioni ya wananchi waliomo katika mazingira kama hayo. Sasa kura za ushindi atazipataje?

Chukua hata hao laki tatu na nusu. Wana waume au wake zao. Wana wazazi. Wana watoto wa umri wa kupiga kura. Wana mababu. Kwa jumla, wana ndugu na hata marafiki wanaowategemea.

Ni maelfu. Mamilioni. Wengi sana wanaotaka mabadiliko katika maisha yao ya kila siku. Kukana huyu ni kukana yule; na mgombea mtarajiwa wa CCM anasema hataki kura zao.

Nani asiyejua kuwa jasho la mfanyakazi, kwa njia ya ujira, linakwenda hadi mpakani Msumbiji, Uganda, Burundi, Zambia, Kenya na Rwanda kuokoa maisha ya wahitaji?

Kiduchu kama ulivyo, mshahara wa mfanyakazi unategemewa na wengi mitaani – mamantilie, mwenye genge, fundi cherehani, mwenye duka – makundi mengine mengi ambayo yanajua hata tarehe ya wafanyakazi kupokea ujira.

Kwa hiyo, kama mgombea urais mtarajiwa wa CCM anakana wafanyakazi, basi anakana sehemu kubwa ya wananchi wapigakura katika unyonge wao. Sasa atapata wapi kura? Atashindaje?

Kikwete amedharau umuhimu wa kura moja inayoleta ushindi. Amekataa kuona kuwa kila mpigakura anapiga kura moja.

Kwa wanaochunguza mambo, sharti waone kuwa Jakaya Mrisho Kikwete ana njia nyingine za kupata kura za kuziba pengo. Ni njia zipi hizo?

Tujiridhishe basi kuwa, kwa kauli ya rais, kwamba hataki kura za wanaomshinikiza, basi ametangaza kuwa ana kura za kutosha.

Je, kwa hili hawezi kuwa amejitangaza mshindi wa uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu? Je, bado kuna uchaguzi wa kweli mwaka huu?

Imeandikwa, “Na tazama, nje ya ufalme wangu, wametenda kinyume cha haki na utashi wenu.” Nani atawarudi? Wako wapi walinzi wa haki na utashi wa umma?

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: