Kwa nini Pinda ni kipenzi kwa Kikwete kuliko Dr Shei


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 20 May 2008

Printer-friendly version
Makamu wa Rais, Dk Ali Mohamed  Shein

Tangu ateuliwe kushika wadhifa wa Uwaziri Mkuu takriban miezi mitatu iluiyopita, Mizengo Pinda amemwakilisha Rais Jakaya Kikwete katika shughuli za nje ya nchi mara tatu. Kwa wastani amefanya hivyo mara moja kila mwezi.

Katikati ya mwezi wa nne (tarehe 17 Aprili) Waziri Mkuu Pinda alimwakilisha Rais mjini Nairobi wakati wa kuapishwa kwa baraza jipya la mawaziri wa serikali shirikishi iliyoundwa.

Mapema mwezi huu Pinda alimwakilisha Rais huko Maputo, Mozambique, kwenye mkutano wa Nane wa Muungano wa maendeleo ya Elimu barani Afrika (ADEA). Na mapema wiki hii Pinda alimwakilisha Rais katika mkutano wa siku tatu wa Jukwaa la Uchumi wa Dunia (World Economic Forum) kuhusu Mashariki ya Kati.

Tusisahau pia kwamba wakati Kikwete akiwa ziarani huko China, ni Pinda, na siyo Dr Shein, aliyemwakilisha katika sherehe za Mei Mosi zilizofanyika kitaifa mkoani Iringa. Aidha, kinyume na ilivyotarajiwa, Dr Shein hakuiwakilisha Tanzania katika mkutano wa dharura wa viongozi wa nchi za SADC ulifanyika Lusaka ulioitiswa na Rais Levy Mwanawasa wa Zambia. Dr Shein alibakia nchini kusimamia mapokezi ya mwenge wa Olympic.

Madhumuni ya makala hii ni kuchambua, pamoja na mambo mengine, uamuzi wa Rais, kiuhalali, kiutaratibu, kisheria, au hata kikatiba wa kupendelea kumchagua Waziri Mkuu wake, na si Makamu wa Rais, Dk Ali Mohamed Shein kumwakilisha katika shughuli za nje, na iwapo pia ziko sababu nyingine za kufanya hivyo mbali na masuala niliyotaja.

Ingawa Katiba ya Jamhuri ya Muungano haimpi makamu wa rais haina majukumu makubwa kama vile yale ya Waziri Mkuu ambaye ndiyo kiongozi mkuu wa shughuli za serikali, lakini ndiye mwenye madaraka makubwa, kingazi, au kicheo kuliko Waziri Mkuu.

Na hi inatokana na uhalali wake kidemokrasia -- katika ngazi hiyo kwani amechaguliwa na wananchi. Katika uchaguzi mkuu, Makamu wa Rais alikuwa katika karatasi moja ya kupigia kura (ballot paper) na mgombea wa urais.

Na ndiyo maana anapoondoka rais nchini, kikatiba madaraka yanamuangukia Makamu wa Rais, na si Waziri Mkuu, ambaye anakuja katika ngazi ya tatu. Hali kadhalika, katiba iko wazi kabisa kwamba iwapo lolote litatokea kwa Rais na kumfanya asiweze tena kuendelea na wadhifa wake ? kama vile kuondolewa madarakani kisheria, maradhi au kifo, basi mara moja Makamu wa Rais anaapishwa kuwa rais na kumalizia kipindi cha urais kilichobakia ? na si Waziri Mkuu.

Kwa maneno mengine, katika muhula wote wa utawala wa Rais husika, Makamu wa Rais ni kama ?Rais mtarajiwa? ? kwa lolote linaloweza kutokea kwa Rais. Suali ni kwamba katika kulizingatia hili, kwa nini Makamu wa Rais wa sasa, Dk Ali Mohammed Shein, anaonekana kuwekwa pembeni na Waziri Mkuu ndiyo anaonekana kuwa ndiye mwakilishi zaidi wa Rais hasa katika masuala ya kimahusiano ya kitaifa?

Ni suali gumu katika kupata jibu kiurahisi lakini pengine ni vyema tukaanzia namna Dr Shein alivyokuja kuwa Makamu wa Rais chini ya awamu hii ya Rais Kikwete.

Ikumbukwe kwamba Dr Shein aliteuliwa tu na Rais wa awamu iliyopita, Benjamin Mkapa kushika wadhifa wa Umakamu wa Rais mwanzoni tu mwa muhula wake wa pili, mwaka 2001, baada ya kufariki kwa aliyekuwa anashika wadhifa huo, Dr Omar Ali Juma.

Nasema Dr Shein aliteuliwa na Rais, hakuchaguliwa na wananchi kama ilivyokuwa kwa marehemu Dr Omar Ali Juma katika uchaguzi wa mwaka 1995, au kwa Dr Shein mwenyewe mwaka 2005. Kulikuwa fununu, wakati wa kinyang?nyiro katika chama chama tawala ? CCM ? cha uteuzi wa wagombea wa urais mwaka 2005 kwamba Dr Shein hakuwa chaguo la Kikwete kama mgombea wake mwenza, alishinikizwa tu na Kamati Kuu ya chama hicho chini ya mwenyekiti wake, aliyekuwa Rais wakati huo, Benjamin Mkapa.

Inasadikiwa kwamba baada ya Mkapa kushindwa kumpitisha ?mtu wake? katika kugombea wa urais (kwani Kikwete hakuwa chagua lake) aliona ni bora akakishinikiza chama kumrejesha tena ?mtu wake? ? Dr Shein katika nafasi ya umakamu wa Rais.

Hapo Kikwete alizidiwa kidogo kete kwani Dr Shein kamwe hakuwa mmojawapo wa ?wanamtandao? wake. Inasadikiwa alikuwa anamtaka Zakia Meghji kuwa mgombea mwenza wake.

Na tumekwisha kushuhudia katika kipindi cha zaidi ya miaka miwili ya awamu ya Kikwete, mitikiso yote iliyotokea ? hasa katika masuala ya tuhuma za ufisadi, Dr Shein hajaguswa kamwe. Ni hakika hakuwa ?mwanamtandao?. Na hapa sisemi kwamba ?mtandao? wote ni wa kifisadi, la hasha, lakini ni dhahiri kuona hali halisi.

Hata hivyo katika nchi nyingi zenye mfumo wa kuwapo nafasi ya makamu wa rais ? nafasi hiyo huwa haina majukumu makubwa sana, na mara nyingi huwapo katika kutimiza matashi tu ya kisiasa, kama vile kwa lengo la kuridhia pande fulani.

Hapa Tanzania tuliwahi kuwa na makamu wa rais wawili. Misri haina makamu wa rais kwa muda mrefu tu sasa, na sababu kubwa, inadaiwa, ni kwamba kuna mtu maalum anaandaliwa kumrithi Rais Hosni Mubaraka akimaliza kipindi chake hiki ifikapo mwaka 2011. Na huyo si mwingine bali ni mwanaye ? Gamal Mubarak.

Kutokana na mfumo mpya wa serikali nchini Kenya uliyotokana na serikali shirikishi, makamu wa Rais Kalonzo Musyoka sasa amejikuta hana kazi, hasa baada ya kuanzishwa nafasi ya Waziri Mkuu.

Ni Marekani tu ambako Makamu wa Rais (ambaye namna ya kuchaguliwa wake ndiyo tunaoutumia hapa) ana kazi kubwa aliyopewa kikatiba. Yeye, pamoja na majukumu mengine, ni mwenyekiti wa vikao vya Bunge kuu la nchi hiyo ? Senate.

Na tukirudi hapa kwetu, huenda pia uamuzi wa Kikwete kumpendelea zaidi Waziri Mkuu Pinda, na siyo Makamu wa Rais Dr Shein, amwakilishe katika masuala ya kimataifa katika nchi za nje unatokana na suala la ?utayarishwaji? wa Pinda huko mbeleni.

Kama alivyo Dr Shein, Pinda hana doa lolote kuhusu tuhuma za ufisadi, lakini anamzidi Shein kwa sababu ni mtu wa kutoka Tanzania Bara.

Inasadikiwa pia kwamba Kikwete kadhamiria kumkabidhi Pinda kuyashughulikia masuala yote ya kuhusu vita dhidi ya ufisadi, na tayari tumeanza kuona kuwa yeye ndiye mzungumzaji mkuu wa serikali kuhusu masuala hayo. Na bila shaka hii pia inatokana na yeye kukubalika zaidi kwa wafadhili.

Hakuna haja ya kusema kuwa kuna masuala ya msingi yanayomfanya Kikwete asizungumzie ufisadi ? na kubwa hapa ni kwamba kuna baadhi ya maswahiba wake wakuu aliyowaamini wameanguka kutokana na tuhuma za ufisadi.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: