Kwa nini tunaendesha nchi kama Zimamoto?


editor's picture

Na editor - Imechapwa 12 May 2010

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

KWA muda wa siku tatu kuanzia tarehe 5 Mei hadi 7 Mei mwaka huu, nchi yetu ilishuhudia ugeni mkubwa wa viongozi wakuu wa nchi mbalimbali na wataalamu wa uchumi waliokuja kuhudhuria mkutano wa kimataifa wa Jukwaa la Uchumi (WEF) uliofanyika jijini Dar es Salaam.

Pamoja na mambo mengine yaliyojadiliwa, mkutano huo ulizungumzia namna ya kuikwamua Afrika kutoka katika mkwamo wa uchumi unaolikabili.

Sisi ni kati ya Watanzania waliojisikia fahari sana kwa mkutano huo uliofanyika baada ya mkutano mwingine kama huo wa Leon H. Sullivan uliofanyika Arusha mwaka jana.

Hata hivyo, kuna mambo ya kusikitisha yaliyojitokeza kabla, wakati na baada ya mkutano wa WEF ambayo hayapaswi kuachwa hivi hivi bila kukemewa.

Jambo la kubwa ambalo halikufurahisha ni maandalizi ya zimamoto. Japokuwa serikali ilikuwa inajua mkutano huo utafanyika wapi, idadi na aina ya wageni waalikwa na kazi ya upambaji uliofanywa katika barabara na eneo la Mlimani City ulikofanyika mkutano ulikuwa aibu.

Kazi ya upandaji miti jamii ya mitende ilifanyika hadi Jumanne yaani siku moja kabla ya kufanyika mkutano huo kwa lengo la kuwafurahisha wageni. Tunasema hivyo, tukiamini kama ingekuwa kwa ajili ya kuimarisha mandhari ya eneo husika, kazi isingefanyika kwa kasi ile tena usiku na mchana.

Tunaamini upandaji wa miti pembezoni mwa barabara na jirani na Mlimani City si kitu ambacho kingetakiwa kusubiri hadi WEF ifanyike.

Tunaamini mpango mzima wa ujenzi wa barabara ya Sam Nujoma pamoja na eneo la Mlimani City ulipaswa ujumuishe upandaji wa miti.

Hii si mara ya kwanza. Viongozi wa mkoa wa Mbeya waliwahi kupanda migomba ya ndizi usiku kwa lengo la kumpendesha Mwalimu Julius Nyerere, lakini alipojaribu kung’oa mmoja na ukang’oka aliwalaumu viongozi hao.

Miaka michache iliyopita, nchi yetu ilishuhudia barabara za mkoani Arusha zikipigwa deki kwa vile aliyekuwa Rais wa Marekani, Bill Clinton, alikuwa akitembelea nchi yetu.

Tumeshuhudia mara nyingi magreda yakifukia mashimo rais au mgeni fulani anapotembelea mambo ambayo yangeweza kufanyika bila ya presha, gharama wala usumbufu kwa wananchi wetu iwapo ingekuwapo mipango ya mapema.

Mambo haya ya kukurupuka yamekuwa miongoni mwa vyanzo vikubwa vya ufisadi ndani ya nchi yetu. Kila linapotokea tukio kubwa, inaonekana wako watu ambao wako tayari kulitumia kwa ajili ya kujinufaisha.

Ni kweli kwamba ni utamaduni wetu kwamba wakati mgeni anapokuja, hata majumbani mwetu, familia huingia gharama kidogo kumfanya ajisikie yuko nyumbani.

Lakini hatuwezi kuendesha nchi kama nyumba zetu. Nchi inaendeshwa kwa mipango endelevu na ya muda mrefu.

Nchi haiwezi kuendeshwa kama kikosi cha Zimamoto. Wakati umefika sasa kwa viongozi kuweka mipango ya kuhakikisha aibu hii ya WEF haijitokezi tena.

0
No votes yet