Kwa staili hii, TFF itamfia Tenga


Alfred Lucas's picture

Na Alfred Lucas - Imechapwa 10 February 2010

Printer-friendly version
Michezo
Rais wa TFF, Leodegar Chilla Tenga

AKILI yangu inanituma kuamini kwamba, TFF (Shirikisho la Soka Tanzania ) chini ya Rais Leodegar Chilla Tenga, inazama.

Nina sababu nyingi za kuamini hivyo, hasa baada ya kuona nguvu, akili na maarifa mengi ya wasaidizi wa Tenga yakielekezwa katika Ligi Kuu na timu ya soka ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’.
Mengi ya msingi tuliyotarajia kuyaona yakikuza soka ya nchi hii ni kama yameachwa yajiendeshe yenyewe.
Kwa mfano, najiuliza kuna sababu gani za msingi za kuipiga danadana Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara ambayo ilitarajiwa kuanza Desemba mwaka 2009, lakini mpaka sasa ni kitendawili?
Timu zilishaingia kambini, mathalani Polisi Dodoma ilishakuwa Dar es Salaam, lakini imekata tamaa na kurejea nyumbani Dodoma, tena baada ya kuingia gharama ambazo hazijulikani nani atazifidia.
Ukiacha Ligi Daraja la Kwanza, kabla ya Tenga kuingia madarakani tulishuhudia uhondo wa Kombe la FAT (sasa pengine lingeitwa Kombe la TFF).
Miaka mingi imepita, Watanzania hawajashuhudia michuano hiyo iliyotoa fursa ya kushirikisha hata timu za mchangani kabisa.
Nakumbuka wakati ule Tanzania Stars iliyoundwa na nyota wengi wa zamani wa Simba na Yanga, ingawa haikuwa katika ligi kubwa nchini, iliweza kutamba mara mbili na kuiwakilisha nchi katika michuano ya kimataifa.
Leo hii michuano hiyo imezikwa rasmi, hakuna anayeijua, na hakuna vipaji vipya vinavyoonekana kutoka mchangani baada ya michuano mingine kumezwa na nyota wa Ligi Kuu.
Ukiachana na michuano, TFF haijaonyesha kabisa juhudi za kufufua au kuendeleza soka ya nchi hii, hasa ile ya vijana.
Mara kadhaa wadhamini kama Coca Cola na Maji ya Uhai imejaribu kuandaa michuano ya vijana, lakini mwisho wa siku michuano na hata vipaji huishia siku ile ile ya mwisho wa mashindano.
Angalau Coca Cola hujaribu kupeleka vijana mpaka Brazil au Afrika Kusini, lakini wakisharudi kila mmoja hulazimika kubeba msalaba wake kujaribu mbinu za kujiendeleza kisoka! Jamani, kwa mtaji huu tunatarajia kuendeleza vipaji au kuua kabisa?
Ni lini tutategemea vipaji vya wachezaji wa Ligi Kuu ambao wengi wamechipukia kwa staili ya uyoga kutokana na kukosa misingi imara ya soka ya kisasa? Kwa staili hii, hakika nguvu za wadhamini waliojitoa mhanga kuipiga jeki Taifa Stars kama vile Benki ya NMB na Bia ya Serengeti zinaweza kupotea bure!
Ndiyo, nguvu zao zinaweza kupotea kwa sababu baada ya akina Shadrack Nsajigwa, hakuna vijana wanaoandaliwa ipasavyo kulitumikia taifa na hatimaye kuirejesha Tanzania katika ramani ya kweli ya soka.
Sana sana tunachokishuhudia sasa ni `madudu’ madogomadogo ambayo kamwe hayana chembe ya kuirudishia heshima nchi hii. Sawa tayari mbinu za kudhibiti mapato zimetangazwa, lakini haitoshi.
Unakuzaje soka kama huna waamuzi waliokomaa, vijana waliolelewa katika misingi halisi ya soka na mambo mengine kadha wa kadha?
Kwa kuyaangalia haya machache, nadhani TFF ya Tenga iliyoanza kwa mbwembwe na kuwajaza watu matumaini si hii tunayoiona sasa kwa sababu imesahau majukumu mengi ya msingi kwa ustawi wa soka ya Tanzania.
Pengine anakosa wasaidizi wenye busara na kiu ya kweli ya kuirudisha soka ya Tanzania katika ramani. Lakini kama ukweli ndio huo, bila shaka juhudi zinapaswa kuelekezwa katika mambo kadhaa, ikiwa pamoja na kuhakikisha anapata Makamu wa Pili wa Rais wa Kweli katika uchaguzi wa mwishoni mwa mwezi huu.
Nadhani mtu kama Ramadhani Nassib akirejea pengine anaweza kukamilisha kazi kwani, licha ya kuwa TFF, atakuwa pia balozi mzuri kwa klabu za ligi kuu na nyingine, akizifikishia ujumbe mzuri jinsi ya kuendesha klabu kisasa na mambo mengine kadha wa kadha.
Nguvu nyingine zinapaswa kuelekezwa katika kuondoa longolongo, kwani katika hili TFF haiwezi kukwepa kutokana na kile kinachodaiwa kuzipiga `panga’ fedha za klabu kutoka kwa wadhamini, mathalani mpaka leo hii Vodacom imeingia doa kwa kushindwa kuzilipa baadhi ya klabu fedha za msimu uliopita.
Inapaswa kuwaimarisha waamuzi ambao leo hii wanaonekana kituko kila wanapoingia uwanjani wakionekana wasiojua chochote au kama wanajua, basi wamenunuliwa.
Imebainika posho ndogo kwa siku ni moja ya sababu ya kuvurunda kwao. Jamani, mwamuzi gani atakwepa kufanya usaliti kwa kuuza mechi kwa kipato kiduchu?
Kuna mengi ya msingi, lakini nisisitize tu kwamba, kwa staili hiii ya sasa, TFF itamfia Tenga na wa kumwokoa makamu wake, Athumani Nyamlani na Nassib kama atapata tena ridhaa. Wa kuchagua “pumba” au “mchele” ni wajumbe.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: