Kwaheri kipa Syllersaid Mziray


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 03 November 2010

Printer-friendly version
Hayati Syllersaid Mziray ‘Super Coach’

BAADHI ya watu waliokuja kuwa makocha maarufu duniani ni wale ambao awali walipata kuwa wachezaji mahiri.

Kwa hiyo, wakishastaafu kucheza soka ya kiwango cha juu, huchukua mafunzo na kuwa makocha. Lakini pia wapo watu ambao hawajapata kuwa wachezaji wa hali ya juu ila wameibuka kuwa makocha maarufu baada ya huchukua mafunzo ya ukocha.

Katika kundi hili la pili yumo hayati Syllersaid Mziray ‘Super Coach’ ambaye, kama ilivyo kwa wanaume wengi, alicheza soka hadi ngazi ya shuleni tu. Aliishia hapo.

Wakati anasoma katika Shule ya Sekondari Malangali, Iringa, Mziray alikuwa kipa wa kutumainiwa katika bweni lake la Shaaban Robert na darasa lake.

Mbali ya soka, Mziray alikuwa mchezaji mahiri wa timu za mpira wa wavu na mpira wa kikapu iliyokuwa inafundishwa na mkuu wa shule mwenyewe, Sylvester Mkoba.

Mziray akishirikiana na mwanafunzi mwingine mrefu Nsaji Moses walikuwa na uwezo wa kupokea mipira (boost), kutoa pasi (set) na kupiga (spike) katika mpira wa wavu.

Mziray ameshiriki michezo hiyo kama kipa, mchezaji wa mpira wa kikapu na wavu hata alipokuwa Shule ya Sekondari Milambo, Tabora.

Vilevile Mziray alikuwa mwenyekiti wa utamaduni na alikuwa mshiriki wa vikundi vya mijadala ya Kiingereza na Kifaransa. Alishiriki kila mchezo shuleni kwa lengo la ama kuwakilisha darasa lake au bweni.

Tangu aliponiacha Malangali mwaka 1977 nikiwa kidato cha II, nilikuja kuonana naye mwaka 1990 alipokuja na timu ya soka ya Simba kuweka kambi ya mazoezi Lushoto mkoani Tanga. Timu ilikuwa ikifanya mazoezi katika uwanja wa Shule ya Sekondari ya Magamba niliyokuwa nafundisha ingawa kambi yao ilikuwa katika Chuo cha Maendeleo ya Jamii, Mabughai.

Simba iliweka kambi huko, ambako ni nyumbani kwa aliyekuwa mwenyekiti wa klabu hiyo, Yussuf Hazali. Hapo ndipo nilipojua alivyojitosa rasmi katika soka na kuwa kocha maarufu.

UWAZI

Mziray katika maisha yake kuanzia alipokuwa shuleni hadi anafanya kazi hakuwa mtu wa kuficha hisia zake. Kama hakuridhishwa na kitu alisema bila kificho na ikiwa alifurahishwa alisifia pia.

Hiyo ndiyo sababu kocha huyo amekuwa akionekana kama kukorofishana na baadhi ya viongozi wa soka au kutoeleweka na maofisa wengine.

Hivi karibuni, Mziray alikuwa mkosoaji wa mfumo wa ufundishaji wa Kocha mkuu wa Stars, Mbrazil Marcio Maximo kiasi cha watu kumwona ‘mzushi’.

Mathalani, wakati akiwa bado na mkataba na Simba mwaka 1990 alijitolea kuifundisha Yanga katika mechi yake dhidi ya Taifa Stars. Tukio hilo liliwaudhi viongozi wa Simba, wakamtimua.

Mwaka 1998 baada ya Taifa Stars kufungwa bao 1-0 na Burundi mjini Dar es Salaam, kocha mkuu wa timu hiyo Hafidh Badru alijiuzulu. Mziray alijitolea kuinoa timu hiyo kwa mechi ya marudiano mjini Bujumbura iliyopangwa wiki mbili baadaye, lakini bado Stars ilifungwa pia 1-0 na ikatolewa katika michuano hiyo ya Kombe la Mataifa Afrika.

Vilevile alikuwa mmoja wa wadau wa soka waliojitolea kufanya ushawishi yafanyike mabadiliko ya katiba ya kilichokuwa Chama cha Soka Tanzania (FAT) mwaka 2004. Vuguvugu hilo ndilo ilimwingiza madarakani Leodegar Tenga katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2004.

Mafanikio
Mziray atakumbukwa kwa mengi lakini zaidi mafanikio makubwa ya heshima aliyoipatia Tanzania.

Mwaka 1994 akisaidiana na Sunday Kayuni, aliiwezesha timu ya soka ya Tanzania Bara kutwaa Kombe la Challenge katika fainali zilizofanyika mjini Nairobi, Kenya. Hiyo ilikuwa mara ya pili tangu mwaka 1974 Bara ilipotwaa kombe hilo chini ya Paul West Gwivaha akisaidiana na Joel Bendera.

Vilevile mwaka 2001, Mziray akishirikiana na Charles Boniface Mkwassa alitwaa Kombe la Castle baada ya kuifunga Uganda kwa mabao 3-0.

Kwa mafanikio hayo, pamoja na kuzipa ubingwa Yanga na Simba, Mziray alipewa jina la Super Coach na kwa baadhi walimwita Mwanangu.

HISTORIA

Mziray alizaliwa Novemba 11, 1957 na alipata elimu ya msingi katika shule saba tofauti zikiwemo za Ifunda ya Iringa alikoanzia na Wami ya Morogoro alikomalizia.

Masomo ya sekondari alipata Malangali na Milambo na baadaye alisomea michezo Chuo Kikuu cha Vuebamaki, Finland na baadaye Bulgaria alikohitimu shahada ya pili ya viungo na utamaduni.

Aliajiriwa na Wizara ya Elimu, Utamaduni na Michezo kama afisa lugha na sanaa, lakini baadaye aliamua kuzama rasmi katika ukocha.

Alianzia Simba ya Dar es Salaam, akahamia African Sports ya Tanga na baadaye akatua Pilsner iliyokuwa inamilikiwa na Kampuni ya Bia Tanzania.

Timu nyingine alizofundisha ni Yanga, Mzizima United, Tanzania Stars iliyokuja kuzaa Twiga FC, Pan Africa na Pallsons ya Mererani ya Arusha.

Kazi ya taaluma. Mwaka 1990 Mziray alikuwa mmoja wa walimu na waanzilishi wa Kitivo cha Michezo katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam akiwa mtumishi kutoka serikalini.

Baadaye Mziray alihamia Chuo Kikuu Huria (OUT) ambako amefanya kazi hadi mauti yanamkuta.

0
No votes yet