Kwani Muhimbili vipi?


editor's picture

Na editor - Imechapwa 11 March 2009

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

HOSPITALI ya Muhimbili inalumbana na mgonjwa Bernard Ibrahim. Siyo madaktari wote na watawala waliomo katika mzozo, lakini wachache wanaolumbana na mgonjwa wanaleta sura mbaya.

Hii ni hospitali kuu na ya rufaa inayotegemewa kwa aina nyingi kama siyo zote za tiba.

Simulizi kutoka Muhimbili zinatia simanzi na kuogofya. Na hazipaswi kuwa hivyo, kwani pale ni kimbilio la wengi.

Hisia mbaya juu ya Muhimbili haziji kwa bahati mbaya. Zinatokana na aina ya utumishi wa wafanyakazi wake. Mwenendo wa baadhi yao unasononesha.

Watanzania hawajasahau tukio la kufanya upasuaji wa makosa kwa wagonjwa wawili: mmoja akiumwa mguu mwingine uvimbe kichwani.

Aliyepaswa kupasuliwa mguu akafumuliwa kichwani na hatimaye kuwa na ulemavu; huku yule aliyekuwa apasuliwe kichwa, akasababishiwa kifo baada ya kuchanwa goti na kidonda kikakataa kupona.

Leo tunasikia simulizi za Bernard Ibrahim, mgonjwa wa jino aliyeanzia tiba Hospitali ya Manispaa Temeke. Analalamika mitaani. Anadai kuwa amezidishiwa ugonjwa. Anaongeza kuwa watumishi Muhimbili hawamsikilizi; anawaita wakorofi.

Imefikia hatua hata faili la Benard linadaiwa kupotea. Kwa nini lipotee? Katika mazingira yapi? Nani anatunza mafaili? Kitu gani kinafichwa? Nani aliandika humo mara ya mwisho? Aliandika nini? Yote yamo kwenye faili. Lipatikane.

Muhimbili si hospitali ndogo ambako mambo mengi ni mazonge. Nini kimepunguka Muhimbili? Maslahi? Zana? Mazingira? Nini lakini? Wito wa kazi?

Watanzania hawako tayari kuona hadhi ya Muhimbili inapigwa kumbo na wachache waliochoka kazi. Tangu lini hospitali kama Muhimbili ikawa na watu wa kulumbana na mgonjwa badala ya kumsaidia kupona. Lini?

Mgonjwa wa jino alikwenda mbio kwa imani ya kupata msaada; sasa anaeleza kwa uchungu kuwa kazidishiwa machungu kwa majibu ambayo hakuyatarajia na kupotea kwa faili lake.

Ubingwa wa hospitali na daktari unapimwa kwa kiwango cha uwajibikaji kitaaluma na siyo karatasi ziitwazo shahada na mahali ambako muhusika alizipata.

Ubingwa wa daktari usaidie na kulinda uhai wa mgonjwa; uwe kimbilio la wengi na umaarufu wa daktari uwe sehemu ya kukomaa kwa taaluma yake, kutambuliwa na kuheshimika.

Tungependa kusikia faili la Bernard limepatikana. Amepata mtaalam wa kumsikiliza na kumhudumia badala ya bingwa wa kubishana naye.

Muhimbili ibaki kimbilio la wengi. Na wananchi wanakimbilia kule walikowekeza. Ni Muhimbili ambako wamewekeza kodi zao – hospitali kuu ya serikali.

0
No votes yet