Kwani TAKUKURU wepi?


editor's picture

Na editor - Imechapwa 04 November 2009

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

TUNAONA Bunge na Serikali, taasisi mhimili katika uendeshaji wa nchi, zinavutana. Kila moja inatunishia mwingine misuli.

Serikali imetuma makachero wake – Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) – wawahoji wabunge kuhusu malipo tata wanayolipwa wanapokagua mashirika ya umma.

TAKUKURU imeanza kuita wabunge na kuwahoji. Lakini, Dk. Harrison Mwakyembe, mbunge wa Kyela, yeye amegoma. Hatua yake hiyo imeamsha hamkani hata kwa wananchi.

Anaona kitendo hicho kinakiuka misingi ya utawala bora na hakikubaliki. Spika Samuel Sitta amemuunga mkono, akisema, “Uchunguzi huo hauna maana kwani sioni tatizo.”

Bunge na TAKUKURU wanategana. Bado bunge linasubiri taarifa ya utekelezaji wa maazimio 23 iliyotaka serikali iyatekeleze; yanahusu ugunduzi wa kuwapo mazingira ya rushwa katika kufikiwa kwa mkataba wa kufua umeme wa dharura uliopewa kampuni ya Richmond.

Azimio mojawapo ni kumwajibisha Mkurugenzi wa TAKUKURU, Edward Hoseah, ambaye alitangulia kusimamia uchunguzi wa mkataba huohuo na kusema “hakuna tatizo lolote.”

Bunge lilimuona Hoseah, kupitia ripoti yake ya uchunguzi wa mkataba huo, alipotosha ukweli aliposema utiaji wake saini haukuwa na tatizo lolote, hakukuwa na rushwa yoyote na wala serikali haikupata hasara yoyote.

Uchunguzi ulioongozwa na Dk. Mwakyembe uliona udhaifu mkubwa na baada ya ripoti kujadiliwa, bunge liliazimia pamoja na mambo mengine, mamlaka iliyomteua Hoseah, ambayo ni rais, imwajibishe. Hajawajibishwa.

Misingi ya utawala bora haikubali Hoseah ambaye hajawajibishwa asimamie uchunguzi unaohusu wabunge. Yeye na TAKUKURU hawajashibana na Bunge. Tuseme Bunge lina tatizo naye. Ni kituko yeye kuongoza uchunguzi dhidi ya wabunge.

Tumemsikia Waziri Mkuu Mizengo Pinda akitetea uchunguzi. Hata Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Sophia Simba, ambaye TAKUKURU iko chini yake, ametetea.

Kwetu busara haikubali. Hatuoni uhalali wowote wa kimaadili katika kuchunguzwa wabunge kwa sasa.

Bali ipo taswira iliyojificha. Huenda serikali inataka kuzima hoja ya Richmond. Hadi sasa inasubiriwa na taarifa ya utekelezaji wa maazimio 23 ya bunge ambayo imeshindwa kuiwasilisha mbele ya kamati ya kudumu ya bunge (Nishati na Madini) wakati wa maandalizi ya mkutano wa 17.

Ni utamaduni mbaya kwamba serikali zisizopenda kusikiliza maoni ya wananchi (public opinion) hutumia mbinu ya kuzua jambo katikati ya mjadala muhimu unaoendelea. Ni ulaghai kwa wananchi eti wageukie hilo na kusahau lile zito zaidi linalowahusu.

Busara ya kawaida inahimiza serikali imalize suala la Richmond ndipo ilete jingine. Watanzania ndivyo wanavyotaka. Tunasimamia hapa, TAKUKURU inayoongozwa na Hoseah, mtuhumiwa na Bunge, haiwezi kuhoji wabunge sasa.

0
No votes yet