Kwanini nitampenda Kikwete


M. M. Mwanakijiji's picture

Na M. M. Mwanakijiji - Imechapwa 27 October 2010

Printer-friendly version
Kisima cha Mjadala

RAIS Jakaya Kikwete ataweza kuingia katika historia, iwapo atahakikisha kipindi kilichobaki cha kampeni kinamalizika kwa amani.

Ni kwa sababu, pamoja na majigambo ya serikali kupitia kwa Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Wananchi Luteni Jenerali Abdulrahman Shimbo, kwamba hakuna damu itakayomwagika, tayari wananchi wameshuhudia damu ikimwagika.

Ni kutokana na ukweli huo, siku chache zilizobaki zinaita kwa kelele “inatosha.”

Katika demokrasia inapotokea umwagikaji damu wa aina yoyote ile, katika mazingira ya kisiasa, ni uthibitisho kuwa taasisi za kisiasa na serikali zimeshindwa kulinda demokrasia kufanya kazi yake.

Mara nyingi kampeni zinajaa mbwembwe, kejeli na utani wa kila namna. Lakini hiyo ndiyo demokrasia ilivyo.

Tayari washabiki wa vilabu vya Simba na Yanga wameelewa maana hasa ya ushindani, kwamba timu moja ikifungwa hatuoni tena mashabiki wake wakipigana au kufanyiana vurugu.

Uelewa huu, umekosekana katika siasa, kiasi kwamba tofauti za kisiasa zimeanza kugeuzwa uadui.

Wanasiasa kutoka chama tawala – Chama Cha Mapinduzi (CCM) na upinzani wameanza kupoteza uelewa kuwa tofauti za kisiasa si uadui.

Visiwani Zanzibari wamejifunza ukweli huu, ingawa kwa gharama kubwa. Sasa wameelewa tofauti za kisiasa si uadui. Mahali ambapo kulikuwa na jazba miaka michache iliyopita, leo wanafanya kampeni katika amani. Inaonekana uadui huu unataka kuhamia Bara!

Hili haliwezi kuepukika iwapo viongozi wetu wa kisiasa watashindwa kuonyesha ukomavu kwa kuzuia tofauti za kisiasa kuwa uadui.

Iwapo hilo litawashinda, basi watalazimika kuondoa uadui huo kwa kusimamiwa na jumuiya ya kimataifa kama ilivyokuwa Kenya na Zimbabwe.

Hapa ndipo ninaamini kuwa Kikwete atakapoweza kuingia katika historia.

Mara zilipoanza kelele za umwagikaji damu nilitoa wito kwa wagombea urais hasa Dk. Willibrod Slaa, Profesa Ibrahim Lipumba na Jakaya Kikwete wakutane kwa pamoja na kuonyesha kuwa wao wenyewe wanasisitiza umoja na mshikamano licha ya tofauti za kisiasa. Hilo halikufanyika.

Naamini pasipo na shaka kwamba bila Kikwete ambaye ndiye rais kwa sasa, kutuliza munkari wa vyombo vya usalama na wanachama wake, siku chache zijazo zaweza kuwa za giza kwa taifa.

Vurugu zinazoweza kutokea nchini hazitatokea kwa sababu ya kidini, au kikabila; zitatokea kwa sababu za kisiasa.

Kutokana na ukweli huu, ni hatua za kisiasa tu zitakazozuia vurugu na hasa kuanzia siku ya upigaji kura na kutangaza matokeo.

Ndiyo maana wananchi wengi watampenda Kikwete endapo atashinda katika amani na siyo katika vitisho na vurugu. Ushindi wowote utakaosababisha manung’uniko ya kudumu, utamtia doa yeyote atakayeingia madarakani.

Ni imani yangu kuwa Kikwete atakataa jaribio lolote la kuzuia shamrashamra za ushindi wa Dk. Slaa endapo matokeo ya uchaguzi yataelekea huko.

Hata wananchi wakatae kumwaga damu kwa ajili ya Dk. Slaa kama mwenyewe aklivyosema, badala yake, anataka “ushindi wa heshima.”

Ni lazima wana CCM watambue kwanza kuwa hawana haki zaidi ya kutawala kuliko watu wengine na Kikwete hana haki zaidi ya kutawala kuliko mtu mwingine.

Hili ni hata kwa Dk. Slaa na wana CHADEMA. Haki ya kutawala itakuja katika uchaguzi na kutokana na kura halali zilizopigwa na mazingira mazuri ya uendeshaji wa uchaguzi.

Hadi sasa, siyo Kikwete wala Slaa au Lipumba ambaye ana haki ya kuliongoza taifa.

Hii maana yake ni kuwa wapiga kura ndiyo watakaoamua ni nani wampe kura yao. Uamuzi huu hauwezi kupimwa kwa umati wa watu kwenye mikutano au kwa wingi wa watu waliovaa rangi za chama kwenye kampeni.

Uamuzi huu utapatikana katika mazingira huru ya kupiga, kuhesabu na kutangaza matokeo. Nje ya hapo, demokrasia itajikuta imechakachuliwa.

Rais Kikwete akitaka kushinda, basi na ashinde kwa heshima. Vilevile, awe tayari kushindwa kwa heshima kwani sauti ya kura za wananchi ndiyo sauti pekee ambayo mwanasiasa yoyote anapaswa kuisikia.

Akishindwa hata kwa kura moja, awe tayari kukubali kushindwa huko na kumpatia mshindi mkono wa pongezi na kumsaidia kuweza kulipitisha taifa katika kipindi cha mpito katika mazingira ya amani na utulivu.

Wito huu uwe kweli kwa mashabiki wa CCM ambao yawezekana hawajajiandaa kabisa kuona mgombea wao anapoteza nafasi ya urais na hivyo kuona kana kwamba wanadhulumiwa “haki yao.”

Rais Kikwete akishindwa lakini akasimamia taifa vizuri na kwa amani na kumkabidhi rais mwingine nchi katika amani na utulivu, ataingia katika historia na kukumbukwa na vizazi vijavyo huku vikisamehe makosa au mapungufu yake ambayo watu wanaweza kuwa wameyaona.

Ninafahamu kuwa baadhi ya watu wazo la Dk. Slaa kushinda linawasumbua sana na kuwatisha. Lakini woga wao na hofu yao isiwe sababu ya wao kulitisha taifa kwa vurugu.

Tutakomaa kama taifa endapo tutaweza kubadilishana madaraka katika hali ya amani na utulivu, ingawa machozi yanaruhusiwa!

Naye, Dk. Slaa na timu yake wasipotoshwe na wingi wa watu katika mikutano yao wakatafsiri kuwa ndio kura zenyewe. Kura si wingi wa watu kwenye kampeni.

Vyovyote ilivyo, naami ni historia inapiga hodi mbele zetu. Wananchi wapewe uchaguzi wa wazi kati ya walichozoea na kipya, kilekile na kingine, yale yale na ya tofauti, wale wale na wengine.

Wananchi wapewe fursa ya kuchagua maendelezo yale yale au matumaini mapya. Uchaguzi siyo kati ya Ukristu na Uislamu, ni kati ya miaka mitano inayofanana na miaka mitano iliyopita, au miaka mitano mipya isiyo fanana na miaka 49 iliyopita. Ni uchaguzi wa kiakili siyo vionjo.

Hivyo basi, tuwakatae wanaotaka tupige kura kwa hisia zao na siyo akili, tuwakatae wanaotaka tupige kura katika woga na siyo ujasiri, na ambao wanajaribu kufanya uchaguzi huu hauna maana.

Ninawasihi wapiga kura, kila mmoja atafute kadi yake ya kura, aangalie jina lake kuhakikisha lipo kwenye kituo chake, na siku ya Jumapili pasipo woga wala hofu aende kuonesha uamuzi wake kwenye sanduku la kura, uamuzi ambao yumkini hautamgusa yeye bali watoto wake au watoto wao miaka inayokuja.

Wananchi wasiogope kupiga kura licha ya mavazi ya FFU au ving’ora vya JWTZ.

Historia iko mbele ya rais Kikwete, kwani siku chache zijazo, wananchi watakaopiga hodi katika milango ya miaka 49 ya utawala wa CCM, wanaweza kuyatikisa yakafunguka na kongwa la utawala wake likaondoka kwenye shingo zao kama ilivyoandikwa, “Wamisri mliowaona leo, hamtawaona milele.”

Yawezekana CCM tuliyoiona miaka 49 iliyopita tusiione tena baada ya Jumapili na ule Unabii ambao ukajikuta unatimia. Vyovyote itakavyokuwa chagua kilicho bora!

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: