Kwanini serikali inatetea waovu?


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 27 January 2010

Printer-friendly version
Tafakuri

Turejee kauli ya Serikali kwenye Kamati ya Nishati na Madini juu ya utekelezwaji wa maazimio ya Bunge kwa watumishi wa serikali waliozembea, baada ya kuvuta muda tangu azimio la Bunge litolewe Februari 2008 kwamba waliozembea hadi kusababisha mkataba tata wa kufua umeme wa megawati 100 kufungwa kati ya Tanesco na Richmond waadhibiwa. Serikali sasa imejitokeza katika rangi yake halisi na kulitisha Bunge.

Kwa mujibu wa taarifa zilizovuja kutoka Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, Serikali si tu imethubutu kusema hakuna mtumishi wake atakayeadhibiwa kwa uzembe kama azimio la Bunge linavyodai, bali pia imelitisha Bunge.

Serikali imeliambia Bunge kwamba kazi yake ni kuishauri serikali! Kwa maana hiyo, mwenye kupewa ushauri ana hiari kuuchukua au kuuacha. Kwa hiyo, serikali imeamua kuuacha ushauri wa Bunge kuhusu kuadhibiwa kwa watumishi wake waliozembea hadi taifa likashindwa kupata umeme wa dharura kwa wakati. Viwanda vikashindwa kuzalisha, wafanyakazi wakakosa kazi, biashara mbalimbali zikasimama, lakini kubwa ya yote kodi za serikali zikapungua kwa sababu hakuna uzalishaji wa bidhaa na huduma nyingine.

Kwa hiyo, Serikali ni kama inaliambia Bunge lifunge mdomo kwa sababu si kazi yake kuadhibu, wala halina haki ya kushurutisha hatua zozote zichukuliwe na serikali. Huu ni ujasiri ambao unastahili tafakuri ya kina.

Mbali na suala la Richmond, Serikali imethubutu bila chembe ya soni kuua kashfa ya Kagoda. Kwa muda wa zaidi ya miaka miwili sasa, suala hili limeachwa likining’inia kama si la muhimu. Kwa ujasiri ule ule unaofanana na kuacha wazembe wa Richmond waendelea kuitumbukiza nchi katika matatizo ya mikataba ambayo ni jadi ya serikali yetu, kashfa ya Kagoda imeachwa ili ife!

Na kweli si Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), wala Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) mwenye ubavu wa kusimama hadharani na kusema kuhusu Kagoda ukweli ni huu.

Kwa mifano hii miwili, inawezekana kabisa ikaelezwa kwamba serikali yetu ina sura mbili au ina makengeza makali katika kutekeleza majukumu yake, hasa katika kusimamia sheria na kuwachukuliwa hatua watuhumiwa wa uhalifu.

Kama ni mwenzao, hata ukitenda kosa gani hakuna wa kukugusa. Ikibidi, visingizo na ubabe vitatumika kulindana. Hii ndiyo serikali inayoheshimu sheria kwa kutazama rangi, jinsia na itikadi.

Wakati haya yakitendwa na serikali, jambo moja la kustaajabisha linasumbua akili na fahamu za wengi.

Hivi katika wabunge wote 300 na ushei hakuna hata mmoja mwenye ubavu wa kuibuka na kuwasilisha hoja binafsi kuionyesha serikali kwamba katika utekelezaji wa majukumu yake imeshindwa kusimamia sheria bila upendeleo?

Idadi kubwa ya wabunge wanamjua mwenye Kagoda ni nani, wanajua ni fedha kiasi gani zilichotwa na kampuni hii. Labda pia wanajua nani alinufaika na fedha hizo ambazo ni takribani theluthi moja ya Sh. bilioni 133 zilizoibwa kwenye Akaunti ya Madini ya Nje (EPA).

Wanajua kwa sababu kuna ushahidi wa kibenki jinsi fedha zilivyochotwa. Waweka saini wa kuchukua fedha wapo. Picha za watu waliofungua akaunti zilizotumika kuchota fedha zipo. Kuna ushahidi mzito, lakini serikali imejitia kiburi na kupuuza kilio cha wananchi. Imekataa kuchukua hatua.

Ni kiburi hicho hicho kimedhihirika juzi kwenye Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini. Ni ubabe huo huo wa kuwatisha wabunge kwamba hawana haki wala mamlaka ya kuishurutisha serikali kuchukua hatua.

Sasa katika mazingira kama haya, nani ana ujasiri wa kuitetea serikali kwamba inapambana na ufisadi na kila aina ya uchafu? Ni kwa nini umma usisadiki kwamba mtindo wa utendaji wa serikali ni uleule unaoakisi makundi yanayoparurana ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)?

Ni kwa jinsi gani serikali ya namna hii inaweza kujipiga kifua kwamba inapambana na maovu wakati kila mwananchi mwenye kuona mbali akitambua wazi kwamba kinachofanyika ni mosi, kukomoana; mbili, kuhadaa umma ukubali kwamba kuna kazi inafanyika wakati si kweli?

Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alipata kusema katika moja ya hotuba zake kwamba “ni lazima serikali itishe wala rushwa.” Kwa maneno mengine, watenda maovu katika jamii ni lazima wawe na hofu wanaposikia serikali ipo.

Serikali inayowalinda waovu, inakula nao. Inawajengea mazingira ya kukwepa mkono wa sheria. Hii ni serikali inayojiaibisha na kuweka ridhaa yake rehani. Ni jambo la kusikitisha kwamba serikali inaonekana kila uchao ikisinyaa na kutetemeka inaposikia harufu ya mafisadi waliotenda makosa makubwa ya kuumiza taifa.

Serikali iliyojaa woga tu ndiyo inaweza kupata ujasiri wa kutetea waovu na kujenga mazingira kwamba waovu hao hawakamatiki, hawashitakiki, hawawezekani kwa kuwa eti wana fedha. Serikali yenye maslahi ndani ya mtandao wa waovu ndiyo tu inayoweza kuthubutu kuwalinda; kwa sababu serikali yoyote iliyoingia madarakani kwa njia ya kura, kazi yake ni kulinda na kutetea maslahi ya wananchi kwa mapana yake.

Serikali isiyoweza kusimamia sheria zake bila kuyumbishwa, bila kuzua visingizio vya ugumu wa sheria, ni serikali iyoamua kuwalinda wahalifu; ni serikali yenye makengeza katika kutimiza wajibu wake.

Hii ni serikali inayoweza kutikiswa na wabunge makini wasiojali rangi, sura, jinsia wala haiba ya mtu, bali wanaosimama katika kutetea sheria na katiba ya nchi.

0
No votes yet