Kweli Mkulo ameshiba, sasa anatukejeli


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 23 March 2011

Printer-friendly version
Tafakuri

KUNA usemi maarufu mitaani kwamba wanandoa wakikaa pamoja muda mrefu hufanana. Sijui kufanana huku ni kwa maana ya sura au tabia.

Lakini nafikiri hawa hufanana kwa tabia, kwa kuwa ni vigumu mtu mzima kugeuka sura.

Ndivyo ninavyowaona mawaziri wa fedha wa nchi hii waliowahi kupitia katika wizara hiyo; wanafanana. Hawa kufanana kwao ni kama wale wanandoa walioishi pamoja muda mrefu—tabia.

Wengi tuna kumbukumbu ya mawaziri waliopata kuwa mawaziri wa fedha katika awamu nne tofauti tangu uhuru. Lakini miongoni mwao wapo watatu waliowahi kutoa kauli zenye utata ambazo hazikuwafurahisha wananchi; zinafafana kitabia.

Waziri wa kwanza alikuwa Cleopa David Msuya ambaye aliwaeleza Watanzania kwamba ‘kila mtu atabeba msalaba wake mwenyewe.’

Msuya alitoa kauli hiyo alipokuwa akijibu hoja bungeni juu ya hali ngumu ya maisha ya wananchi.

Hii ilikuwa baada ya Tanzania kupigana vita na Uganda na wakati huo waziri wa kwanza wa fedha, Edwin Mtei akiwa amekwisha kujiuzulu kwa kutofautiana na bosi wake, Mwalimu Nyerere juu sera za uchumi.

Msuya aliandamwa, lakini kadri siku zilivyokwenda serikali ilijivua wajibu wa kuwapa wananchi kila kitu kama walivyokuwa wamezoea chini ya mfumo wa ujamaa.

Mfumo wa maisha ulibadilika baada ya kuingia kwenye sera za marekebisho ya uchumi.

Mambo ya kuchangia gharama katika huduma za kijamii kama kwenye afya, elimu, maji na kwingineko yalianza. Mwishowe serikali ikajitoa kabisa katika mambo mengi ya kimsingi ikajitwika jukumu tata la ‘kuweka mazingira ya uwekezaji’.

Hadi sasa Watanzania wanaendelea kubeba msalaba wao; haijulikana watautua lini.

Awamu ya tatu ilimshuhudia Waziri wa Fedha, Basil Mramba, akitamka wazi kwamba wale wote waliokuwa wanapinga mipango ya serikali ya kununua ndege walikuwa wanapoteza muda kwa kuwa serikali haitabadili mawazo.

Alisema hata kama ni kunyimwa misaada Watanzania walikuwa tayari ‘kula nyasi almradi ndege inunuliwe’.

Huyu alisimamia ndege ya rais hadi ikanunuliwa. Kitu ambacho sina uhakika nacho ni kama kweli Watanzania walikuwa radhi kula nyasi ili ndege hiyo inunuliwe.

Hii ni kwa sababu katika mazingira ya kawaida ni muhali kusema kwamba ndege ilikuwa ya umuhimu sana kwa wananchi wakati huo.

Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo, naye amejiingiza katika kundi la mawaziri wa fedha waliowahi kutoa kauli tata.

Mkulo alisema kwamba ‘Kila Mtanzania atakula kwa jasho lake’. Alitoa kauli hiyo akikataa serikali ya awamu ya nne kubebeshwa lawama za hali ngumu ya maisha huku bei za bidhaa na huduma zikizidi kupaa.

Kwa stahili ya Msuya na Mramba, Mkulo  ameongeza kauli yake ‘kula kwa jasho’.

Kwa uhakika hakuna ubaya kwa viongozi wa serikali kuwaeleza wananchi juu ya kutegemea mafanikio katika maisha yao kwa kufanya kazi kwa bidii.

Ni wajibu wa wananchi kutoka jasho ili wale matunda ya jasho lao, hili linaelezeka katika mazingira ya uwajibikaji kwa pande zote.

Yaani kama viongozi wanaishi kwa mfano; kama nao wanaishi kwa jasho, kama nao wanaogopa kutumia ovyo kodi za wananchi, kama kweli wanaishi kama watumishi wa umma, basi wito wa namna hiyo, ‘kubeba msalaba; kula nyasi ili ndege inunuliwe, na kila Mtanzania kula kwa jasho lake’ unakuwa na maana.

Kwa bahati mbaya, viongozi wetu wanahubiri kile ambacho hawatendi, hawaishi kwa jasho, hawabebi msalaba na wala hawathubutu kunusa harufu ya nyasi achilia mbali kula.

Kauli hizi ni matokeo ya kusikia na kuzoea harufu ya fedha pale Hazina kiasi cha kupumbazika na kukosa hisia kwa umma.

Kwamba Waziri wa Fedha anadhani kwamba fedha za umma ambazo ni kodi ya kila mvuja jasho wa nchi hii ni mali yake, na ana hiari ya kuzifanya atakavyo kwa kuwa tu imetokea kuwa yuko Hazina. Huu ni ulevi mbaya mno wa madaraka, kutokujali.

Watanzania wanakumbuka kuna kiongozi mmoja mstaafu alipata kuwaambia wananchi wake waende kuzimu “go to hell’ kwa sababu tu walikuwa wanalalamikia usafiri wa treni kuwa mgumu wakati huo akiwa waziri wa usafirishaji. Kilichompata waziri huyo ni kipigo kwenye sanduku la kura katika uchaguzi uliofuata.

Hii hata hivyo, hutokea kwa bahati mbaya kwa sababu Watanzania ni wapole. Wanaambiwa wabebe misalaba, wanakubali; wale nyasi wanaitika hewala bwana, na hata wakiambiwa sasa watakula kwa jasho la uso wao ijapokuwa kila siku wanavuja jasho na nafuu hawaioni, watasema tu hewala bwana.

Nani kasema Watanzania hawavuji jasho hadi Mkulo aje kuwakumbusha? Shangingi analoendeshwa Mkulo si matunda ya jasho la wananchi?

Ofisi yenye kiyoyozi anayokaa na kusaini nyaraka za serikali tena kwa mbwembwe bila hata kuonja ‘joto ya jiwe’ ya mgawo wa umeme inalipiwa kodi na nani? Je, nyumba anayoishi imejengwa na kodi za nani?

Je, samani zake au ulinzi wake au safari zake za nje na ndani, nani anazilipia?

Nani asiyejua kuwa Mkulo hajui jasho, tangu NPF hadi ikawa NSSF ambako kote alikuwa mkubwa? Si kuna fedha za wanachama wanakatwa mishahara yao kila mwezi lakini hawana nguvu wala uwezo wowote wa kuamua jinsi akiba yao inavyotumika?

Ni lini hasa Mkulo alitoka jasho? Alitoka jasho akifanya nini na wapi?

Kauli kama hizi zinapotolewa katika kipindi ambacho vongozi wa umma wanapaswa wakose usingizi kwa sababu ya kushindwa kwa serikali kutimiza wajibu wake wa kimsingi kabisa huku maisha yakizidi kuwa magumu, ni kielelezo cha shibe ya ukwasi kwa mtu kama Mkulo.

Hivi, nani asiyejua kwamba kila Mtanzania anajua vilivyo si kazi ya serikali kumjaza fedha mfukoni?

Lakini kila Mtanzania anajua ni wajibu wa serikali kwa mfano kuhakikisha umeme upo, mfumuko wa bei haupandi sana, kodi za wananchi zinatumika kwa ungalifu na kuelekezwa kwenye maeneo ambayo yatapunguza kero na ugumu wa kuzalisha mali na upatikanaji wa masoko kwa wazalishaji wa mashambani na viwandani. 

Mkulo ni lazima ajue kwamba Watanzania wamevuja jasho jingi ndiyo maana yeye anaishi katika ukwasi alionao leo. Anachotaka wafanye sasa ni kutoka damu puani wakifanya kazi kwa bidii ili maendeleo yaje?

0
Your rating: None Average: 5 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: