Labda wewe, wenzako Shamsi wanauza ardhi


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 07 April 2009

Printer-friendly version
Kalamu ya Jabir

MAGAZETI mawili yanamnukuu Waziri Kiongozi wa Zanzibar, Shamsi Vuai Nahodha akisema ndani ya Baraza la Wawakilishi: ardhi ni mali ya serikali; serikali yetu haitakubali kuona wananchi wanakosa ardhi, wakati watu wasiostahiki wanamilikishwa ardhi.

“Bado serikali itabaki kuwa mlinzi wa ardhi ya Zanzibar na kuhakikisha inawafaidisha raia wake badala ya kumilikisha watu ambao watakifanya kizazi kijacho kisiwe na haki za kutumia ardhi.”

Akamalizia, “kama ulinzi wa ardhi utaachwa mikononi mwa wananchi kuna hatari ya raslimali hiyo kuhodhiwa na raia wageni.”

Kwa kauli, aliyoyasema ni matamu kuyasikia. Ndivyo inavyotakiwa. Ardhi ndio raslimali muhimu zaidi na ya msingi kwa taifa inayochochea ukuaji wa uchumi. Hata kwa mtu mmoja mmoja, akiwa na ardhi amejitengenezea njia nzuri ya kuimarika kiuchumi.

Serikali ina nafasi nzuri zaidi ya kulinda ardhi. Pamoja ya hiyo, ni kweli imeruhusu wananchi kumiliki sehemu ya ardhi ikiwemo kwa njia ya kuirithi kutoka kwa wazazi. Huu ni umilikaji wa asili wa ardhi.

Sehemu ya ardhi ambayo ilitaifishwa na serikali baada ya mapinduzi ya 12 Januari 1964, iligaiwa kwa wananchi waliotajwa kama waliokosa ardhi kwa mpango wa eka tatu-tatu.

Hadi leo mpango huu unatambuliwa, ingawa kwa muda sasa kumekuwa na kauli za viongozi wa serikali kuitwaa ardhi ambayo aliyepewa ameshindwa kuitumia.

Lakini wakati Shamsi akitoa kauli inayosisitiza umuhimu wa ardhi kumilikiwa na serikali, kuna matukio ambayo siyo tu yanaonyesha uvunjaji mkubwa wa sheria, bali pia yanathibitisha namna uroho wa viongozi wa kiserikali unavyochochea migogoro ya ardhi.

Viongozi wengi wanamiliki maeneo makubwa ya ardhi, mengine wakiyachukua kwa nguvu. Wananchi wanalalamika kudhulumiwa ardhi waliyokuwa wakiitumia kwa kilimo lakini hakuna anayejali.

Na kutojali huku kwa viongozi, hakukuja kwa bahati mbaya; ukweli ni kwamba baadhi yao, tena waandamizi wanatwaa maeneo ya ardhi na kuyafanyia biashara kwa kuyauza kwa wageni.

Nimesema yapo matukio ya wananchi kulalamika kuhusu kudhulumiwa ardhi na viongozi. Tunayasikia haya Nungwi, Tumbatu, Matemwe, Kidoti, Tazari, Kilombero, Selem, Mwakaje, Kijichi na Kizimbani.

Haya yapo Dunga, Bambi, Pongwe, Uroa, Chwaka, Tunguu, Fuoni, Kibele, Kikungwi, Ungujaukuu, Paje, Bwejuu, Jambiani, Makunduchi, Kizimkazi, Muyuni na Kisauni.

Ni sehemu chache sana hazina malalamiko dhidi ya uporaji wa ardhi unaofanywa na viongozi. Wengi wanauza ardhi kibiashara kwa wanaoitwa wawekezaji wageni.

Hayo yanatokea Pemba. Kuanzia Konde na Micheweni kaskazini, hadi Makongeni na Mkoani upande wa kusini. Viongozi wamejimegea hata maeneo ya hifadhi.

Nilipoitwa mwaka 2007 kushuhudia utwaaji haramu wa ardhi ambayo kwa asili imekuwa ikitumiwa kwa kilimo cha juu na wananchi wa Nungwi, sikuamini nilichokiona. Wana Nungwi walitoa maelezo na vielelezo vilivyoonyesha uharamia uliofanywa na viongozi akiwemo Waziri aliyetumikia serikali ya Dk. Salmin Amour Juma.

Kwanini nisishangae kukuta kiongozi mwakilishi wa wananchi anajiundia kampuni na makada wenzake wa CCM wakiitambulisha kama kampuni iliyoanzishwa na Kamati ya Maendeleo ya Nungwi lakini manufaa ya mauzo ya ardhi waliyonyang’anya wanakijiji yakibaki kwa watu wachache?

Kupitia kinachoitwa Kamati ya Maendeleo Nungwi, makada wa CCM wametwaa eneo kubwa la ardhi hata kufika ekari 200 na kuanza kujengea uzio. Baada ya muda mfupi, unasikia sehemu ya eneo ameuziwa mwekezaji kwa Sh. 150 milioni.

Wana Nungwi ambao asili yao ni uvuvi, wanahitaji ardhi hii kwa ajili ya kilimo cha mazao ya chakula. Wanapoporwa ardhi waliyoitumia kwa miaka yote huko nyuma, maana yake wamedhulumiwa.

Hakuna anayejali kwa sababu pamoja na kuchapisha gazetini taarifa za uporaji huo wa ardhi inayonufaisha makumi ya wananchi, hakuna kiongozi wa serikali aliyechukua hatua ambayo ingewezesha wananchi kurudishiwa ardhi hiyo.

Viongozi wa SMZ wamekuwa wakitajwa kujiingiza na biashara ya kuuza ardhi waliyoitwaa kiharamu, hakuna anayewakemea. Hawakemewi kwa kuwa wanajua hata viongozi walio juu yao wamepora ardhi sehemu moja au nyingine ya nchi.

Kwa sababu viongozi hawajali sheria, hawana thubutu ya kukemea wageni wanaotwaa ardhi kwa njia haramu. Wageni wangapi wamenyang’anywa ardhi waliyoitwaa kilaghai vijiji vya Michamvi, Bwejuu, Paje na Jambiani kwa msaada wa maofisa kutoka idara za serikali?

Uporaji ardhi za asili za wananchi ndio uliosukuma wanakijiji wa Uroa kupiga kelele mpaka uongozi wa juu kulazimika kuingilia kati. Jinsi uporaji ardhi ulivyokithiri, sasa maofisa wa serikali wanauza hata maeneo ya makaburi. Laana tupu!

Ipo ardhi kubwa ambayo haijatumika ipasavyo kwa manufaa ya nchi. Hii ungetarajia ikatolewa kwa utaratibu ulio wazi na unaohusisha viongozi wa kijiji ilipo ardhi husika. Hakuna kitu kama hicho. Viongozi wanatumia mamlaka kutwaa maeneo kama haya bila kushirikisha wananchi.

Imefanyika hivyo Muyuni na Micheweni karibu na maeneo ya Hifadhi ya Msitu wa Ngezi. Bila ya kujua kinachoendelea, wananchi wanashtukia vijana wa kazi wanajenga uzio kuzunguka eneo ambalo wanakijiji wamekuwa wakilima mazao ya chakula.

Wakijaribu kutaka kujua, anatokea kiongozi anasema “hili eneo linatumika kwa manufaa ya nchi.” Akibanwa kidogo, anamtaja kiongozi aliye juu ambaye anajua hakuna mwananchi atakayethubutu kumfikia.

Uporaji haramu unafanyika kwa ardhi inayokusudiwa kwa ujenzi wa nyumba. Maofisa husika wanajulikana walivyo waroho pale wanapotumwa kupima maeneo kwa jili ya ujenzi wa makazi ya watu.

Baadhi yao walibainika kutwaa viwanja hadi vitatu eneo la Tunguu. Kukimbia kesi, wakauza harakaharaka. Hadi leo Waziri mhusika hajatoa ripoti ya uchunguzi alioagiza ufanywe kuhusu tuhuma hizi.

Kama ugawaji wa nyumba za mkopo nafuu Kwa Mchina na Michenzani ni mtihani kwa serikali, itakuwa ardhi? Sasa Shamsi inawezekana hajagaiwa, lakini ajue wenzake ni mafundi wa uporaji ardhi.

Hofu kubwa niliyonayo, ni kwamba mlinzi wa ardhi Zanzibar ni mfano wa komba aliyefungwa kwenye mpukusa wenye ndizi iliyoiva; atakula tu.

0
No votes yet