Libya ya Gaddafi imeteketea, imeisha


Fred Okoth's picture

Na Fred Okoth - Imechapwa 24 August 2011

Printer-friendly version
Muammar Gaddafi

MTIHANI mkubwa unaoikabili Libya kwa sasa, mbali ya mapambano makali ya kufyeka majeshi tiifu kwa Rais Muammar Gaddafi, ni jinsi ya kuzuia umwagikaji zaidi wa damu katika mitaa mbalimbali ya jiji la Tripoli.

Wakazi wa maeneo mbalimbali katika jiji hilo walikuwa wakisherehekea kufuatia shemu kubwa ya jiji kuangukia mikononi mwa wapinzani hivyo kuelekea kuhitimisha utawala wa miaka 42 wa Gaddafi.

Mpaka juzi haikuwa bayana kama wangeweza kuutwaa mji huo, lakini hatua ya majeshi ya waasi kuingia katika jiji hilo, bila umwagaji damu inaonesha kwamba fikra za wakazi wapatao milioni mbili ni upatanisho zaidi kuliko kulipiza kisasi.

Kuingia kwa kishindo kwa majeshi ya waasi katika jiji la Tripoli ni mafanikio ya kushangaza. Katika maeneo mengi majeshi ya waasi yalikuwa yakitembea kwa miguu bila kupiga risasi. Hiyo inatokana na mipango ya muda mrefu ya kuwaandaa wananchi kuasi kuanzia Jumamosi iliyopita.

Hofu iliyopo ni namna gani Baraza la Mpito la Kitaifa (NTC) lenye makao yake makuu mjini Benghazi, kwa uhakika, litakavyoweza kulinda usalama wa raia.

Imeelezwa kwamba kuna silaha nyingi ndogondogo mikononi mwa wapiganaji wa kujitolea nchini Libya, na kama ilivyo katika nchi nyingi zenye migogoro, ni vigumu kutabiri nini kitatokea katika siku zijazo kupitia silaha hizo.

Wakati hadi juzi bado ilikuwa haifahamiki alikojificha Gaddafi, jamii ya kimataifa imetoa ombi kwa kiongozi huyo wa muda mrefu akubali kun’gatuka madarakani.

Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron amemtaka Gaddafi kujisalimisha kwa majeshi ya waasi bila masharti yoyote.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia, Franco Frattini alisema kwamba Gaddafi hakuwa anadhibiti zaidi ya asilimia 15 ya jiji. Hakueleza namna alivyopata takwimu hizo.

Rais wa Merakani Barack Obama amesema kuwa Libya "imeteleza kutoka katika mikono ya kimabavu na kuwa katika mikono ya umma" na akamtaka Gaddafi kuachia madaraka haraka ili usiwepo umwagiliaji zaidi wa damu.

"Hatima ya Libya sasa imo katika mikono ya watu wa Libya," anasema Obama na kuahidi kufanya kazi kwa karibu na waasi.

Kauli hiyo ya Obama inafafana na ahadi iliyotolewa na maofisa wa Majeshi ya Kujihami ya Nchi za Magharibi (NATO) kuwa ndege za kivita kutoka katika muungano huo zitaendelea kulinda usalama wa anga la Libya.

Iliripotiwa juzi kuwa Afrika Kusini, ambayo iliongoza jitihada za mwafaka za Umoja wa Afrika kati ya waasi na serikali ilikuwa imetuma ndege kumwokoa kiongozi huyo.

Lakini Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini, Maite Nkoana-Mashabane alikanusha habari hizo kuwa nchi yake haijatuma ndege yoyote nchini Libya.

Nkoana-Mashabane alithibitishia waandishi wa habari akisema, "Hatujui Gaddafi alipo na tunadhani bado yupo Libya."
Katika hatua nyingine, kituo cha televisheni cha Libya kilitangaza sauti ya Gaddafi ikiwasihi Walibya, kwa maneno makali, kuwa wasimame na kusaidia kulinda utawala wake. Gaddafi mwenyewe hakuoneshwa.

Msaidizi wa karibu wa zamani wa  Gadhafi ambaye wiki iliyopita alikimbilia Italia, alisema kuwa kiongozi huyo hatokubali kuondoka madarakani kirahisi.

"Nadhani haitawezekana kabisa kumwona Gaddafi akijisalimisha," alisema Abdel-Salam Jalloud alipohojiwa na kituo cha redio ya taifa RAI iliyopo Italia. "Gaddafi hana ujasiri kama ya Hitler ya kujiua mwenyewe."

Jalloud, ambaye alikuwa msaidizi wa karibu wa Gaddafi mpaka mnamo miaka ya 1990 walipokosana alitoroka Tripoli siku ya Ijumaa na kwenda Italia.

Hadi juzi waasi walikuwa wamewakamata watoto watatu wa Gaddafi akiwemo mtoto kipenzi aitwaye Seif al-Islam aliyekuwa anaandaliwa kurithi utawala wa baba yake. Seif al-Islam na baba yake wanatuhumiwa na mahakama ya kimataifa ya ICC iliyopo The Hague, Uholanzi kwa makosa ya ukiukwaji ya haki za binadamu.

Mtoto mwingine aliyekamatwa, kwa mujibu wa msemaji wa Baraza la Taifa la Mpito (NTC), lenye makao yake Benghazi, Mustafa Abdel-Jalil ni Al-Saadi Gadhafi huku mwingine akiwekwa chini ya ulinzi. Al-Saadi pamoja na kaka zake Mutassim na Khamis wote walikuwa wakuu wa brigedi.

Umati mkubwa wa watu wenye furaha ulifurika eneo la Green Square Jumapili jioni wakiimba nyimbo kumsema Gaddafi aliyejaliwa nyele zilizojisokota.

Wapiganaji walifyatua risasi heweni huku wananchi wakishangilia kwa kupiga makofi ya kuwapongeza huku wakipepea bendera yao yenye rangi tatu. Baadhi walitia moto bendera za rangi kijani kibichi zilizotumika enzi za utawala cha Gaddafi na wengine walikanyaga picha za kiongozi huyo.

Msemaji wa serikali, Moussa Ibrahim amewapa imani wafuasi wao kwamba kulikuwa na maelfu ya wapiganaji wenye ari na walioapa kuendelea na mapambano makali dhidi ya waasi.

"Tutapigana. Wakazi wa nchi nzima wako upande wetu. Wanakuja kwa wingi kulinda Tripoli kupambana dhidi ya waasi," alisema Ibrahim.

Taarifa nyingine zinasema kwamba majeshi ya waasi yalipofika katika milango ya Tripoli, wanajeshi maalum wa Gaddafi wanaopewa jukumu la kulinda jiji la Tripoli walijisalimisha wenyewe.

Imeelezwa sababu ya kujisalimisha ni kwamba kamanda wa kikosi hicho maalumu alikuwa mfuasi  wa waasi kwa siri baada ya kuishi na chuki ya muda mrefu dhidi ya Gaddafi.

Kisa cha kamanda huyo ‘kumuasi’ kisiri Gaddafi ni kwa vile alimnyoga kaka yake miaka kadhaa baada ya Gaddafi kugundua kuwa alikuwa mfuasi wa waasi. Taarifa hizo ni kwa mujibu wa Fathi al-Baja ambaye ni kiogozi mwenye nyadhifa kubwa katika kambi ka waasi.

Vita dhidi ya Gaddafi vyenye lengo la kumn’goa katika utawala wake wa miongo minne vilianza Februari mwaka huu, katika kile kilichoelezwa ni mageuzi ya tawala za nchi za Kiarabu.

Mapinduzi ya wananchi dhidi ya tawala za Kiarabu kwa mtindo wa nguvu ya umma yalianza Tunisia, yakaingia Misri na yakaenea Yemen na Syria lakini watawala wa Jordan, Algeria na Iran waliwahi mapema kuzima.

0
No votes yet