Libya yazima Mohammed Enterprises


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 15 June 2011

Printer-friendly version
Mohamed Dewji, Mkurugenzi mtendaji wa MeTL

UBALOZI  wa Libya jijini Dar es Salaam umekana mahusiano yoyote na kampuni ya Mohammed Enterprises (MeTL) na mshirika wao Massoud Mohamed Nassr.

Hatua hii inaziba mwanya wa kampuni hiyo kujipatia sehemu ya dola 121.9 milioni (sawa na kiasi cha Sh. 180 bilioni) ambazo inadaiwa ni deni la Tanzania kwa Libya linalotokana na mkopo wa mafuta.

Fedha hizo zilitarajiwa kuchotwa kwa mtindo wa EPA wa kununua madeni yaliyoshindikana kutoka benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Tayari ubalozi umeiarifu serikali kuhusu suala hilo na nakala ya barua yake kupelekwa mahakama kuu ambako mashauri mawili yamefunguliwa na MeTL.

Taarifa kutoka ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali jijini Dar es Salaam zimeeleza kuwa hata ofisi hiyo tayari imetaarifiwa kuhusu suala hilo.

Nyaraka ambazo MwanaHALISI limepata zinaonyesha kuwa mfanyabiashara maarufu wa chakula nchini, Gulamabbas Hassanali Fazal Dewji anataka kujipatia mabilioni ya shilingi kutokana na kile kilichoitwa kuuziana madeni sugu kati ya serikali za Tanzania na Libya.

Vyanzo madhubuti vya habari vimelieleza gazeti hili kuwa serikali imezuia malipo ya mabilioni ya shilingi ambazo mfanyabiashara huyo amekuwa akijitahidi kuyadai kupitia kesi mbili alizofungua katika Mahakama Kuu ya Tanzania.

Dewji ambaye ni mkurugenzi wa kampuni ya Mohammed Enterprises (T) Limited (MeTL), anadai zaidi ya dola 20 milioni kupitia kesi Na. 127 ya 2009 na kesi Na. 110 ya 2010.

Wakati kesi Na. 127 ambayo MeTL ilimshitaki raia wa Libya aitwaye Massoud Mohamed Nassr au Masoud M. Nasser, iliamuliwa 26 Mei 2011, kesi Na. 110 haijasikilizwa.

Katika uamuzi wa kesi ya awali inayodaiwa kuhusu mkataba wa kuuziana deni, Jaji Augustine Mwarija aliamuru pande husika zigawane mapato pamoja na riba yaliyotokana na uuzaji wa dhamana za serikali zinazoshikiliwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Mapato hayo yanafikia Sh. 6,640,550,960 ambapo uamuzi wa Jaji Mwarija unaelekeza kuwa MeTL itaingiziwa kwenye akaunti yake Sh. 3,320,275,480.

Lakini, kulingana na nyaraka zilizopatikana, hata mapato hayo si halali na serikali imezuia malipo.

Serikali ya Libya, ambayo MeTL imeishitaki kama mdaiwa wa kwanza katika kesi Na. 110, imekataa kutambua mpango wa kuuziana deni la dola 121,900,000 ambalo linadaiwa kutokana na Tanzania kushindwa kulipa mkopo tangu mwaka 1983.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe ameiambia MwanaHALISI kwamba wizara yake haitambui makubaliano ya MeTL na Nasser na haioni uhalali wa madai yao.

Membe ambaye alizungumza na gazeti hili ofisini kwake Dar es Salaam juzi Jumatatu, alisema wizara yake tayari imemjulisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuwa serikali ya kigeni haiwezi kushitakiwa na Mtanzania kwa mikataba ambayo haikuidhinishwa.

“Serikali ya nje haiwezi kushitakiwa bila ya kuwa na nyaraka za serikali zilizosainiwa na watu wenye kutambuliwa katika mikataba. Huyu hajalipa fedha na hana mkataba… (kama ni) deni lazima linunuliwe na serikali na kuna masharti ya kulipa,” alisema.

Akigusia maelezo yaliyotolewa na ubalozi wa Libya nchini, waziri Membe alisema ni maelezo sahihi na kwamba msimamo wa serikali ni kutokuwepo sababu yoyote wala uhalali wa kuishitaki serikali ya Libya katika suala hilo.

Alisema Mlibya anayedaiwa kufunga mikataba ya kuuziana deni na MeTL linalohusu mafuta ambayo serikali ya Libya iliiuzia Tanzania, hakuwa na hata sasa hana mamlaka ya kuiwakilisha serikali ya Libya katika jambo lolote na “hakuwa na mkataba wowote kati ya serikali ya Libya na MeTL.”

MeTL imeishitaki Libya kama mdaiwa wa kwanza katika kesi Na. 110. Ubalozi wa Libya unasema hautambui mpango wa kuuziana deni la dola 121,900,000 uliobuniwa na MeTL kutokana na Tanzania kushindwa kulipa deni lake linalotokana na Libya kuiuzia serikali ya Tanzania mafuta kwa mkopo.

Ubalozi wa Jamhuri ya Kisoshalisti ya Watu wa Libya jijini Dar es Salaam, imeeleza kwamba haitambui makubaliano ya aina yoyote kati ya serikali ya Libya na MeTL au anayejiita mwakilishi wa serikali ya Libya.

Akijibu takwa la kuitwa shaurini mahakama kuu, ofisa wa ubalozi wa Libya anaeleza waziri wa mambo ya nchi za nje Tanzania kuwa serikali yake haijawahi kuipeleka Tanzania mahakamani.

Katika hati yake ya maelezo yenye Kumb. N/REF 7/2/2250 ya tarehe 20 Mei 2011, ambayo nakala yake ilipepekwa mahakamani, ubalozi wa Libya unasema, katika mahusiano yake ya nje ya nchi – yawe ya kisiasa au kiuchumi – huwa inashughulika na serikali wala si mtu au taasisi binafsi hasa suala lenyewe linapohusu deni kwa biashara ya mafuta.

“Libya, katika suala hili (la kuuza mafuta), inazingatia muktadha wa udugu na Tanzania, unaotokana na uhusiano mzuri wa kisiasa tulionao. Tunaamini Libya haistahili kushitakiwa na kampuni hii kutokana na suala hili,” inasema hati hiyo.

Serikali ya Libya, unaeleza ubalozi wake, haijapata kusaini au kuidhinisha mkataba wowote wa kibiashara na kampuni inayodai katika kesi tajwa.

Inasema, “Ni muhimu ukafahamu kuwa mamlaka inayostahili kuiwakilisha serikali ya Libya katika Tanzania ni ubalozi wa Libya na si yeyote mwingine; iwe kwa kusaini mikataba au kuiidhinisha pale inapotokea…”

“Ubalozi wa Libya unaiomba mahakama tukufu kutoendekeza madai haya dhidi ya Libya. Tuna matumaini makubwa ya busara na hekima kutumika katika kutenda haki kuhusu kesi hii,” ameeleza wakala wa serikali ya Libya.

Maelezo ya serikali ya Libya yaliwasilishwa kwa Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania kwa barua ya wizara ya mambo ya nje tarehe 30 Mei 2011 yenye Kumb. Na. GA 226/336/78 iliyosainiwa na Abdallah M. Mtibora kwa niaba ya katibu mkuu wa wizara hiyo.

0
Your rating: None Average: 5 (1 vote)

RSS LISHO

Syndicate content    Jiunge