Lini serikali itasikia


editor's picture

Na editor - Imechapwa 04 April 2012

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

KIWANGO cha asilimia moja tu cha ukuaji wa uchumi wa maeneo ya vijijini nchini petu, kwa mwaka, kingetosha kubadilisha fikira za viongozi wa serikali kama ni makini.

Labda hawapo makini ndiyo maana hawajali hilo ni tatizo kubwa kimaendeleo. Hawaoni kamwe kunahitajika mapinduzi katika upangaji wa sera na programu ili zilete mvuto kwa wananchi wanaoishi vijijini.

Hawataki kuumiza vichwa japo wanajua kuwa kiwango cha asilimia saba cha ukuaji wa Pato la Taifa (GDP), hakinufaishi uchumi wa mamilioni ya wananchi wa vijijini. Hapa kuna pengo la kipato kwa makundi haya mawili ya wananchi.

Ukweli, pengo la viwango vya mapato ya wananchi wa mijini na wale wa vijijini, ni moja ya vigezo vinavyotumika kupima mafanikio ya nchi katika utekelezaji Malengo ya Milenia (MDGs) yanayosimamiwa na Umoja wa Mataifa.

Upo ukweli mwingine: Matokeo ya hali hiyo ya kuongezeka kwa tofauti ya kipato kwa Mtanzania wa mjini na aliyeko kijijini, ni wale walioko vijijini kuzidi kukimbilia mijini kwa matarajio ya kupata maisha mazuri.

Kawaida, miji inapozidi kuhamiwa na makundi ya wananchi wanaotoka vijijini kwenye maisha duni, huku uimarishaji huduma za kijamii mijini ukikosa msukumo wa kuimarishwa, ni kutengeneza bomu jingine.

Tanzania itakuwa na mabomu mangapi? Tatizo la ajira kwa vijana, ongezeko la kiwango cha umasikini kwa wananchi, uchumi unaochechemea, na ukosefu wa huduma bora za afya, elimu, maji safi na salama na makazi.

Matatizo haya yanaongezeka wakati serikali haijajirekebisha katika namna inavyotumia fedha za umma. Kumekuwa na matumizi mabaya ambayo hata wahisani wanayalalamikia.

Matumizi mabaya ya fedha za walipa kodi na wahisani yanaongeza tatizo kwenye lile la msingi la serikali kushindwa kutumia vizuri raslimali za taifa hivyo kujinyima fursa nzuri ya kuinua uchumi wa taifa.

Sasa wakati viongozi wa serikali wanagoma kutafakari njia za kuondokana na matatizo hayo, wiki iliyopita, wawekezaji wa kimataifa walimpasha Rais Jakaya Kikwete.

Walimwambia ni aibu kwa serikali kulilia misaada ya wahisani wakati ndani ya nchi kuna raslimali nyingi ambazo zingetumika vizuri zingewezesha uchumi kuimarika.

Tumekuwa tukiyaeleza yote haya. Viongozi ambao wanatamba kuwa wanaongoza serikali sikivu, hawajabadilika. Ni lini wataamua kuukubali ukweli na kubadilika, ni vigumu kufahamu. Na huo ndio mtihani kwa serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

0
Your rating: None Average: 5 (1 vote)