Lipumba amvaa Mkapa


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 12 August 2008

Printer-friendly version
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba

CHAMA cha Wananchi (CUF) kimesema hakina imani na juhudi za Rais Jakaya Kikwete za kupambana na rushwa kwa kuwa uongozi wake ulipatikana kwenye misingi ya rushwa.

Kampeni za Chama Cha Mapinduzi (CCM) na mgombea wake Kikwete za mwaka 2005 zililipiwa na uporaji wa fedha za umma kupitia akaunti ya EPA ya Benki Kuu, amesema Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba katika taarifa kwa vyombo vya habari.

Taarifa ya Lipumba aliyotarajia kusoma jana kwenye mkutano wa waandishi wa habari, inafafanua mkondo wa ufisadi nchini ambapo pia analaumu wafadhili kwa kuendelea kuisifia serikali wakati hakuna kikubwa kinachofanyika kuhusu mapambano dhidi ya rushwa.

?Kwa hakika mtandao wa Kikwete ni mtandao wa mafisadi. Wameyasaka madaraka siyo kwa nia ya kuleta ?Maisha bora kwa kila Mtanzania,? bali kuzitafuta na kuzitumia fursa zozote za kuipora nchi kwa ari mpya, nguvu mpya na kasi mpya,? ameeleza Lipumba katika andishi maalum.

Amependekeza viongozi na watendaji serikalini waliojilimbikizia mali isiyoelezeka kwa vipato vyao halali, wafikishwe mahakamani kwa mujibu wa sheria.

Aidha, ameshauri Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) ?ipewe uongozi mpya ulio makini na jasiri wa kupambana na rushwa.?

Profesa Lipumba ametoa mlolongo wa mapendekezao katika kukabiliana na rushwa. Kwa mfano ameshauri kazi za Tume ya Rais iliyoshughulikia ubinafsishaji mashirika ya umma zifanyiwe tathmini na uhakiki wa utendaji wa kina.

Amesema mashirika yaliyobinafsishwa katika misingi ya rushwa yarejeshwe serikalini na kubinafsishwa kwa mujibu wa sheria; wakati makampuni ambayo hayakutimiza mikataba ya ubinafsishaji, yachukuliwe hatua za kisheria.

Kuhusu ubinafsishaji nyumba za serikali, amependekeza kuwa nyumba zote zilizouzwa kwa viongozi wa serikali bila kufuata utaratibu wa kisheria wa kuuza kwa mnada wa wazi mali ya umma, zirudishwe serikalini.

Katika andishi hilo Lipumba anasema msimamo wa chama chake ni kupambana na rushwa za aina zote.

Amesema msimamo wa chama chake ni kupambana na rushwa kwa kuhakikisha kuwa ?Sangara na Mapapa" wa rushwa, wanaoshiriki katika rushwa kubwa, wanashughulikiwa kwanza sambamba kuwashughulikia ?dagaa? wa rushwa.

Akiwageukia wafadhili, Lipumba amesema anashangazwa na kauli zao za kumpamba rais mstaafu Benjamin William Mkapa kuwa aliweka misingi ya utawala bora.

Lipumba amesema matukio mkubwa ya rushwa na ufisadi ?katika nchi yetu yalitokea katika kipindi cha uongozi wa Rais Mkapa.

?Mkapa alivunja sheria na kanuni za maadili ya uongozi kwa kutumia ikulu kuanzisha kampuni na kukopa benki dola 500,000 (fedha kidogo kwa nchi tajiri, lakini fedha nyingi sana kwa nchi maskini kama Tanzania). Mkopo huu ulilipwa ndani ya mwaka mmoja,? amelalama Lipumba.

Pamoja na mambo mengine, Lipumba amesema katika andishi hilo kuwa ?Mkapa alibinafsisha mgodi wa makaa ya mawe ya Kiwira kwa kampuni ya familia na rafiki zake kwa bei poa ya shilingi milioni 700 lakini wakalipa shilingi milioni 70 tu.? Bei ya soko ya mgodi huu inakadiriwa kufikia Sh. 4 bilioni.

Amemtuhumu Mkapa kwa kushindwa kutangaza mali zake baada ya kumaliza muda wa utawala wake na kuruhusu kuendelea kwa mradi wa kufua umeme wa kampuni ya IPTL.

Lipumba amesema Mkapa alikaidi hata baada ya kujulishwa na wataalamu wa ndani (Wizara ya Nishati na Madini, na TANESCO) na wataalamu wa Benki ya Dunia, kuwa mradi huo ni ghali sana, una harufu kali ya rushwa na utaifilisi TANESCO.

Uanzishaji wa mradi wa dhahabu wa Meremeta, mikataba ya makampuni ya madini, ununuzi wa rada kwa bei ya juu sana (Sh. 40) ?kwa sababu ya wakubwa kupokea rushwa,? ni baadhi ya mambo Lipumba anamlaumu Mkapa kwa kusimamia na kutekeleza.

Hayo ni pamoja na uuzaji kwa ?bei ya kutupa? baadhi ya mashirika ya umma kama vile Kampuni ya Sigara, Shirika la Simu Tanzania (TTCL) na Benki ya Biashara ya Taifa (NBC).

Hata hivyo, Lipumba anasisitiza kuwa ukwapuaji wa mabilioni ya shilingi kwenye akaunti ya EPA uliandaliwa na kutekelezwa wakati wa utawala wa Mkapa na kwamba huo hauwezi kuwa msingi wa kumsifia Mkapa.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: