Lipumba ataweza kuzuia bundi CUF?


Alfred Lucas's picture

Na Alfred Lucas - Imechapwa 14 March 2012

Printer-friendly version

PROFESA Ibrahim Haruna Lipumba ametinga nchini. Safari yake ya Marekani iliyomchukua kwa miezi karibu sita imefika kikomo. Hamu waliyokuwa nayo wanachama wa Chama cha Wananchi (CUF) pamoja na viongozi wenzake imetulia.

Maelfu ya wanachama waliofika uwanja wa ndege wa Mwalimu Nyerere kumpokea, walionyesha kila aina ya furaha na manjonjo. Walitoa majigambo na matamko mepesi na mazito kuhusu tatizo la mgawanyiko uliokikumba chama hicho.

Mgawanyiko huo umejidhihirisha kwa baadhi ya viongozi waliovuliwa uanachama wa CUF kuanzisha chama kipya cha Alliance for Democratic Change (ADC) chini ya mwenyekiti wa muda Said Miraji Abdalla, kijana aliyefikia ngazi ya msaidizi katibu mkuu mwaka 2005.

Msukumo wa kuanzishwa kwa ADC unatajwa na wanachama wa CUF kuwa umetokana na nguvu ya Hamad Rashid Mohamed, mbunge wa Wawi, Pemba, ambaye ndiye aliyeongoza kundi la viongozi walionyang’anywa unachama kwa madai ya kuendesha uasi dhidi ya chama.

Kuonyesha kuwa wana-CUF walikuwa na kiu na Profesa Lipumba, wanachama hao walijitokeza kwa wingi kumlaki wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti wao, Machano Khamis Ali na Katibu Mkuu Maalim Seif Shariff Hamad.

Ni Jumapili, saa 9.30 alasiri, Profesa Lipumba alipotua nchini akitokea Marekani ambako alikuwa akifanya kazi za kusimamia mipango ya urekebishaji uchumi wa dunia pamoja na maprofesa wa uchumi wa mataifa mengine.

Mapokezi yalijenga picha kuwa ilikuwa ni kama “baba anasubiriwa nyumbani kuja kuua nyoka” aliyetinga katika nyumba ya familia kwa takribani miezi mitano sasa kiasi cha vyombo vya habari kuwa na vichwa vya habari kama “CUF yameguka”, “CUF yazidi kugawanyika.”

Ngoma hiyo ilianza hasa 04 Januari, mwaka huu. Baraza Kuu la Uongozi (BKU) lilikutana hoteli ya Mazsons, mjini Zanzibar, na kutoa uamuzi wa kufukuza uanachama viongozi wanne.

Viongozi walioguswa na rungu hilo, wameongozwa na hamad Rashid, mwanasiasa mwanzilishi wa CUF na ambaye amewahi kuwa mkurugenzi wa fedha mwanzoni kabisa mwa uanzishaji chama hicho.

Hamad Rashid aliwahi kuwa waziri katika serikali kabla ya mfumo wa vyama vingi kuanzishwa mwaka 1992. Aliwahi kuwa naibu waziri katika Wizara ya Mambo ya Ndani (1982-87) na Wizara ya Fedha (1987-88).

Wenzake waliofukuzwa pamoja kwa tuhuma hizohizo za uasi kwa chama, ni Doyo Hassan Doyo, Shoka Khamis Juma na Juma Saanani.

Ni hivi, kabla ya uamuzi huo, kulikuwa na mvutano uliochagizwa na kitendo cha Hamad Rashid kutangaza kutaka ukatibu mkuu wa CUF akiwa na maana kuazimia kumpiku Maalim Seif.

Alishikia bango mpango wake huo licha ya kukatazwa na uongozi wa juu. Alieneza kampeni yake katika mikutano ya ndani matawi ya Manzese na Mabibo, jijini Dar es Salaam.

Kishindo kingine kililipuka kwa Miraji, aliyekuwa Meneja wa Kampeni wa Profesa Lipumba alipogombea urais wa Jamhuri ya Muungano 2010, kutangaza kujitoa chama hicho huku akianzisha chama cha ADC.

Miraji anaongoza ADC inayoundwa na wanachama waandamizi waliojitoa CUF. Yeye ni kaimu mwenyekiti wakati Adawi Limbu, aliyekuwa mgombea ubunge wa CUF jimbo la Temeke 2010, akiwa katibu wa muda.

Matokeo haya ya kuanzishwa chama kipya kutokana na waliofukuzwa CUF yalisukuma wanachama wa CUF kugharimika kukodi malori ya aina ya FUSO kwa ajili ya kufika uwanja wa ndege kumshuhudia kiongozi wao ili waondoe kiu ya habari njema, mahali pa habari za kufukuzana.

Mgogoro ulipoibuka, maneno yalianza. Shutuma nyingi zikamuangukia naibu katibu mkuu wa CUF, Bara, Julius Mtatiro na naibu katibu mkuu mwenzake Zanzibar, Ismail Jussa Ladhu.

Hawa wamekuwa wakitajwa kama viongozi matata wanaoeneza chuki dhidi ya kina Hamad Rashid, ikitajwa kuwa chuki hizo ni maelekezo ya Ofisi ya Katibu Mkuu.

Tayari viongozi hao kwa nyakati tofauti wamejibu madai hayo kwamba wanaowapakazia hivyo ndiyo walikuwa wahujumu wa chama kwa muda mrefu licha ya kupewa nafasi nyeti za uongozi kiasi cha kukinyima mvuto chama.

Mfano halisi ambao Miraji analia nao ni kitendo cha CUF kujitoa katika uchaguzi mdogo wa Arumeru Mashariki mkoani Arusha, akisema “kushika namba tatu katika uchaguzi uliopita si kigezo cha kutosimamisha mgombea katika jimbo hilo.”

“Hivi kama Arumeru Mashariki tulishika nafasi ya tatu ndiyo tusisimamishe mgombea kwa kuhofia kupoteza pesa? Mbona katika kiti cha urais mwaka 2010 Profesa Lipumba alishika nafasi ya tatu; je, uchaguzi wa mwaka 2015 hatagombea urais kwa kuogopa gharama?”

“Said Miraji ni mfuasi wa Hamad Rashid kwa muda mrefu sana. Amekuwa akikihujumu chama yeye na Hamad kuondoka kwake siyo tishio kwa CUF,” anasema Mtatiro. Majibu yanayofanana na Ladhu pamoja na bosi wao, Maalim Seif.

Viongozi hao walisema CCM imeshindwa kuiua CUF, hivyo hawadhani kama Hamad Rashid na wenzake wanaojitoa kila uchao, wataweza kutekeleza azma yao.

Profesa Lipumba alizungumza hayo juzi na kusema, “taarifa kuhusu mgongano huo nilikuwa nazipata kupitia vyombo vya habari na kuna wakati nilikuwa nazungumza na viongozi. Lakini nasikia watu walikuwa wanahoji mbona sisemi kitu... haikuwa busara kuacha kazi niliyopewa na kuja kutatua hilo.”

“Nikiwa kule nilikuwa nasema, lakini kule nilikokuwako ni mbali mno, sikuweza kusikika. Ila ukweli ni kwamba ifike hatua wanachama lazima wawe na nidhamu, waheshimu maamuzi ya vikao na kubwa zaidi, katiba.”

Amesema, “Chama imara lazima wanachama na viongozi wake wawe na nidhamu. Kama kuna mtu anataka kuwa kiongozi ni suala la kuwa mvumilivu tu kwani uchaguzi mkuu wa CUF utakuwa 2014. Mwanachama yeyote ana haki ya kuwania nafasi yoyote aitakayo.

“Mathalani mwaka 2009 kwenye uchaguzi mkuu wa chama mimi niligombea na Profesa Safari (sasa yuko CHADEMA) na Meja Masanja kutoka Shinyanga, lakini mwisho wa uchaguzi nikawashinda na wenzangu wakatulia, lakini mmoja akaamua kutoka.

“Kujiunga katika chama na kutoka ni uamuzi wa mwanachama. Hilo halinitii wasiwasi. CUF haiwezi kumfunga mtu kuhama kama wanavyofanya vyama vingine. Ila kuna tatizo ambao ama kweli lazima tuheshimu msemo wa ‘hujafa hujaumbika’ maana mtu kama ni mzima unaweza kuanguka na kuporomoka chini.

“Ni haki yao na ninawatakia kila la kheri. Chama ni nidhamu na humo mtu atapata haki zake zote za kisiasa, kijamii na kiuchumi,” anasema Profesa Lipumba akilenga wanachama waliohama na kuanzisha chama kipya cha ADC.

Aidha, Profesa Lipumba anakiri kwamba matatizo mengi yamesababishwa na kuchelewa kuchapishwa upya kwa katiba iliyorekebishwa mwaka 2009 na mkutano mkuu.

Hata hivyo, ni wanachama wa CUF anayeweza kuona kama ametoshwa hamu yake kwa majibu ya Profesa Lipumba au laa. Alikuwa profesa huyu tu aliyekuwa akitumainiwa kutoa msimamo kuhusu mgawanyiko katika chama hicho.

0
No votes yet