Lipumba aulizwe alipojikwaa


Stanislaus Kirobo's picture

Na Stanislaus Kirobo - Imechapwa 31 March 2009

Printer-friendly version
Profesa Ibrahim Lipumba

MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF) Profesa Ibrahim Lipumba, amejitosa katika sakata la ununuzi wa mitambo ya Dowans.

Katika kauli yake wiki mbili zilizopita, wakati akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari kupitia Jukwa la Wahariri, Prof. Lipumba alijenga hoja yake kwa kutoa sababu za kiuchumi – kikubwa ni kwamba nchi zote zilizo nyuma katika maendeleo ya viwanda hutumia mashine na mitambo iliyotumika sehemu nyingine.

Alisema, “Hatuwezi kukwepa kununua mitambo chakavu. Makampuni huhamisha mitambo iliyotumiwa nchi moja na kutumiwa nchi nyingine, na huu ni uzoefu wa kawaida.”

Prof. Lipumba alisema katika kuendesha mashirika ya umma ya kibiashara ni muhimu kuzingatia “faida inayopimwa kwa uwiano wa gharama kwa mwekezaji.”

Katika hoja yake, Lipumba amezingatia zaidi suala la mitambo ya Dowans “kibiashara” na “kifaida” kuliko suala lingine lolote.

Kwa maneno mengine, anatazama mitambo ya Dowans kama mitambo iliyopo sasa Ubungo; hataki kabisa kuangalia historia nzima na hasa ujio wa kampuni hiyo na utata wa miliki yake.

Kwa maneno mengine, hataki kuliangalia suala hilo kama linahusika na “ufisadi,” “kashfa” au “uovu” mwingine wowote uliotendeka huko nyuma hadi kusababisha kuwepo kwa kampuni ya Dowans.

Pamoja na kulitizama suala la ununuzi wa mitambo ya Dowans kibiashara, bila shaka Lipumba anatambua kuwa kauli yake ya kuunga mkono imewafurahisha wale watakaonufaika na ununuzi wa mitambo hiyo – yaani mafisadi.

Inashangaza kuona profesa huyo aliyebobea katika mambo ya uchumi hataki kuliangalia suala hilo kama sehemu ya mgogoro ,kubwa na hata vita dhidi ya ufisadi nchini.

Hana habari, au hataki kuzingatia kwamba kampuni hiyo ni mtoto wa kampuni ya kifisadi ya Richmond iliyopigiwa kelele nyingi, kutikisa nchi na kusababisha kujiuzulu mawaziri watatu akiwemo waziri mkuu.

Isitoshe kuna maafisa wakuu wawili wa serikali wengine ambao walidhihirika kuhusika na sakata lenyewe na ambao serikali iliagizwa na Bunge kuwachukulia hatua lakini hadi sasa serikali haijafanya hivyo. Anayejua sababu za kutotenda ni serikali yenyewe.

Ilikuwa mara ya kwanza katika historia ya nchi hii kwa waziri mkuu kujiuzulu kutokana na kashfa; tukio ambalo lilionyesha uzito wa ufisadi ulivyofanyika.

Hili pia Lipumba hakutaka kulitia maanani wakati anatoa kauli yake hiyo ambayo bila shaka imewavunja moyo baadhi ya watu katika mapambano haya dhidi ya ufisadi.

Mtazamo wa Lipumba ni kwamba Dowans ichukuliwe kama Dowans tu, mengine yote hayo ni siasa. Nadhani Profesa amesahau kitu kimoja: Vita vyovyote vya dhati dhidi ya ufisadi lazima viendeshwe kimaadili na vizingatie miiko. Bila hivyo, itaonekana ni dhihaka na havitafika popote.

Hakuna maadili yoyote kwa serikali kuamua ghafla kutathmini kitu ambacho tayari ilishaamua kuwa ni uchafu.

Ni kama vile lori lililokamatwa kwa kusheheni pembe za ndovu au nyara nyingine za serikali na mwenyewe kuhukumiwa kufungwa – halafu serikali inakuwa tayari kununua lori lake ili kumsaidia.

Au jambazi aliyethibitika kunyan’ganya na kuua na baadaye kufungwa, halafu serikali ikawa tayari kununua nyumba yake ili kumsaidia. Tungekubali iwapo serikali ingetafuta namna au vipengele vya kutaifisha mitambo hiyo yenye harufu mbaya ya rushwa kuliko kuinunua.

Aidha, hata kama haiwezekani kukwepa kununua mitambo chakavu, lakini siyo lazima kununua hii ya Dowans ambayo hata utaratibu wake wa kuingizwa nchini ulighubikwa na udanganyifu.

Si vyema inunuliwe mitambo mingine basi, chakavu kama sheria/kanuni ya serikali ya ununuzi itapindishwa au kurekebishwa? Inunue mitambo isiyokuwa imetia dosari na kuitikisa serikali na nchi nzima.

Serikali lazime ionyeshe angalau kaujeuri ka-kuzingatia maadili na heshima katika kuendesha vita hii ya ufisadi na masuala yanayotokana nayo. Hakuna haja ya serikali kuonekana kuwapa ahueni mafisadi.

Kwani leo hii, serikali ikiwaambia Dowans waondoe mitambo yao ndani ya miezi miwili ama sivyo itakokotwa na kuwekwa nje, itakuwa na kosa gani? Kwa nini serikali inakuwa na woga mkubwa katika masuala ya msingi?

Na hapa bado sijazungumzia suala la umiliki wa mitambo – yaani nani mmiliki. Kwa muda mrefu mmiliki alikuwa hajulikani. Lakini ajabu ni kwamba lilipozuka tu suala la ununuzi, ikabidi mmiliki aundwe au atangazwe ili apatikane wa kufanya biashara na serikali.

Wiki iliyopita gazeti hili liliandika kuwa mtu mmoja, raia wa Oman, anayedai kuwa mmiliki wa mitambo hiyo, hapo awali aliwahi kuikana kampuni hiyo, kwamba wala haiijui. Ushahidi upo. Na hadi sasa hajasema chochote kuhusu kusutwa huko.

Hili suala nalo limeongezea dosari hoja hiyo ya Lipumba na kuipa nguvu ile kambi inayopinga ununuzi, kwani inaonekana kwamba suala zima ni mwendelezo wa ulaghai wa awali kupitia Richmond.

Inavyoonekana, masuala ya ufisadi siyo anga za Lipumba na ndiyo maana CUF haishupalii sana suala hili kama vile Chadema. Inawezekana ni kwa sababu Lipumba amebanwa sana na suala la muafaka kiasi kwamba hana muda kushughulikia masuala ya aina hii.

Tayari baadhi ya wadadisi wanaona kauli ya Prof. Lipumba inaweza kupunguza mvuto na guvu ya chama chake. Kuna haja ya kutafiti alikojikwaa na kwa nini.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: