Lipumba: Mimi ndiye rais bora


Ezekiel Kamwaga's picture

Na Ezekiel Kamwaga - Imechapwa 27 October 2010

Printer-friendly version
Profesa Ibrahim Lipumba

MGOMBEA urais wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, amesema Jakaya Kikwete hafai kuwa rais kwa kuwa si mtu makini na hana uwezo wa kuiletea Tanzania maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Prof. Lipumba alisema anamfahamu vizuri na kwa muda mrefu mgombea huyo wa urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwamba si mtu makini wala mtu anayejishughulisha katika kutafuta kiini cha matatizo ya watu na utatuzi wake.

Akizungumza katika viwanja vya Jangwani juzi, Dar es Salaam na baadaye kwenye mdahalo uliofanyika katika Hoteli ya Movenpick, Prof Lipumba alisema mtu pekee bora, kati ya wagombea wote saba wa urais ni yeye.

“Hapa sijambeza wala kumponda mgombea yeyote wa upinzani, lakini ninachosema ninapojiangalia mimi na wenzangu, mimi ni bora na huo ndio ukweli,” alitamba Prof. Lipumba huku akishangiliwa kwa nguvu.

Alisema anashangaa watu kumfikiria Kikwete wakati mgombea huyo wa CCM amekwisha kukiri kwamba hafahamu kiini cha matatizo ya Watanzania pamoja na utajiri ilionao wa maliasili na kwa sababu hiyo hana sifa za kuendelea kuongoza.

“Hii ndiyo tabu ya kuwa na rais Mkwere. Mimi ni Msukuma na Kikwete ni Mkwere na hivyo huyu ni mtani wangu. Lakini katika mambo haya ya kitaifa hakuna utani na ni muhimu Watanzania kufanya maamuzi ifikapo Oktoba 31 kunichagua mimi kuwa rais mpya wa Tanzania,” alisema Prof. Lipumba huku akijinasibu kwa kutaja uzoefu wake wa masuala ya kiuchumi alipokuwa akifundisha nchini Marekani na Finland.

0
Your rating: None Average: 5 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: