Liyumba arudi gerezani


William Kapawaga's picture

Na William Kapawaga - Imechapwa 25 February 2009

Printer-friendly version
Amatus Liyumba

MTUHUMIWA wa kwanza katika kesi ya matumizi mabaya ya madaraka yaliyoisababishia serikali hasa ya zaidi ya Sh. 220 bilioni, Amatus Liyumba, amefutiwa dhamana.

Hakimu Hadija Msongo wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, alitoa uamuzi huo jana baada ya kuridhika na maelezo yaliyotolewa na upande wa mashitaka katika kesi inayomkabili pia aliyekuwa Meneja Mradi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Deogratius Kweka.

Hakimu Msongo alisema huku akisikiliza na umati wa wasikilizaji, kuwa ameridhika mtuhumiwa alitoa hati za uongo katika kujitahidi kutimiza masharti ya dhamana ikiwemo kukabidhi pasi ya kusafiria iliyokwisha muda wake.

Pia alisema uchunguzi wa hati za mali zisizohamishika zilitolewa na wadhamini wa Liyumba, zilibainika kuwa na matatizo mengi.

Baada ya uamuzi wake huo, Hakimu Msongo alitaka upande wa mashitaka kukamilisha upelelezi wa hati hizo ili ifikapo tarehe 6 Machi atoe uamuzi kuhusu dhamana ya mtuhumiwa huyo. Aliahirisha kesi hadi siku hiyo.

Liyumba, ambaye ni mkurugenzi wa utawala na utumishi wa BoT, alifika mahakamani baada ya kutajwa kuwa alikuwa haonekani kiasi cha mahakama kulazimika kuita wadhamini wake kuwahoji.

Hata hivyo, walipoitwa, waliachiwa na kutakiwa kufika tena jana ili kujua hatima ya Liyumba kama atafika mahakamani.

Mahakama ilimtoa rumande Liyumba – ambaye amefunguliwa mashitaka mahakamani na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) – baada ya kuwasilisha hati moja ya mali yenye thamani ya Sh. 882 milioni wakati masharti ya dhamana yake ni pamoja na kuwasilisha hati za mali za thamani ya Sh. 55 bilioni.

Baada ya kugundulika kuwa hati hiyo ilikuwa na kasoro, mahakama ilitoa hati ya kukamatwa Liyumba, ambayo haikuweza kutekelezwa na kuibuka uvumi kuwa alikuwa haonekani.

Mtuhumiwa mwenzake, Kweka, angali rumande baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana hadi jana. Wote kwa pamoja wanatuhumiwa kutumia vibaya madaraka yao wakiwa waajiriwa wa BoT katika mradi wa ujenzi wa majengo pacha ya benki hiyo, jijini Dar es Salaam, na kusababisha hasara ya Sh. 221,197,299,200.95 kwa serikali.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: