Lowassa aibua mapya


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 21 July 2010

Printer-friendly version
Edward Lowassa

MADAI mapya ya Edward Lowassa, yule waziri mkuu aliyejiuzulu, kwamba hata kama angekuwa madarakani angeendelea kushirikiana na kampuni ya Richmond, yameibua mapya.

Akizungumza na kituo cha Televisheni cha TBC1 Ijumaa iliyopita, Lowassa alisema hajutii “uamuzi wa kuipa kazi Richmond.”

Anasema hata kama angerudi leo madarakani, bado angeendelea na mpango huo uliozaa kashfa iliyommomonyoa kisiasa.

Lowassa alijiuzulu wadhifa wake, Februari 2007 baada ya kutuhumiwa kufanya upendeleo wa kuipa kazi kampuni ya Richmond Development Company (LLC) kutoka Marekani.

Kampuni hiyo ambayo ilikuja kuthibitika kuwa haikuwa na sifa wala uwezo wa kifedha na kitaaluma, ilipewa jukumu la kuzalisha megawati 100 za umeme wa dharura. Ilishindwa.

Wakati Lowassa akijitapa kwamba uamuzi wake ulikuwa sahihi, taarifa kutoka ndani ya serikali na Kamati Teule ya Bunge, zinasema Lowassa alitumia madaraka yake vibaya kwa kuagiza kufutwa kwa zabuni ya kufua umeme ambayo tayari ilipewa kampuni ya CDC Glogbeleq kutoka Canada.

Uamuzi wa Lowassa wa kufuta zabuni ya CDC ndio ulisababisha taifa kutumbukia katika giza na hatimaye kuingizwa kwa kampuni isiyokuwa na hadhi, sifa wala uwezo wa kufanya kazi iliyoomba – Richmond.

Uchunguzi unaonyesha kwamba tarehe 11 Januari 2006, serikali iliteua kampuni ya CDC kuingiza nchini mitambo ya kuzalisha umeme yenye uwezo wa kuzalisha megawati 74. Mitambo ya kampuni hiyo ilikuwa na vipengele vifuatavyo:

Kwanza, ikiwa mkataba wa ukodishaji utakuwa wa miaka mitano, serikali itatakiwa kulipa dola za Marekani 3.2 kwa kWh moja ya umeme itakayotumia.

Pili, iwapo mkataba wa ukodishaji utakuwa wa miaka mitatu, serikali italazimika kujikamua na kulipa kiasi cha dola 5.3 kwa kWh moja ya umeme.

Mkataba kati ya serikali na CDC ulikuwa na unafuu mkubwa kwa kuwa kilikuwapo kipengele kinachoelekeza kuwa mara baada ya mkataba wa ukodishaji kumalizika, mitambo iliyokodishwa inakuwa mali ya serikali.

Kwa mujibu wa mawasiliano ambayo gazeti hili linayo, baina ya TANESCO, serikali na kampuni ya CDC, mitambo ya kampuni hiyo ilitarajiwa kuwasili nchini Aprili 2006.

Kampuni ya CDC Glogbeleq ni kampuni tanzu ya kampuni inayofua umeme kwa kutumia gesi ya Songas.

Hadi sasa, hakuna anayefahamu kilichosababisha Lowassa kuingilia mchakato wa zabuni ulioiteua kampuni hiyo ya kimataifa na inayosifika kimaadili, uwezo wa kiuchumi na kiutaalam; na badala yake kuipa kazi hiyo Richmond.

Uchunguzi wa MwanaHALISI unaonyesha kwamba tarehe 20 Februari 2006, Lowassa kupitia kwa aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Dk. Ibrahim Msabaha aliagiza bodi ya zabuni ya Tanesco kuanza mchakato upya.

Mchakato huo ulioibua Richmond kutoka kusikojulikana, ulisimamiwa kwa nguvu zote na Lowassa mwenyewe. Tangazo la serikali la kuitisha zabuni mpya lilitolewa 23 Februari 2006, huku zabuni zikipangwa kufunguliwa 6 Machi 2006 na tathimini kwa wazabuni ikiwa tarehe 7 na 8, Machi 2006.

Hata hivyo, kabla Lowassa hajatekeleza mpango wake wa kuipa kazi Richmond, hapo tarehe 22 Februari 2006, mamlaka ya manunuzi ya umma (PPRA) iliandika barua mbili kwa Tanesco.

Barua zote mbili – ile yenye Kumb. Na. PPRA/Tanesco/41/16 ya tarehe 23 Februari 2006 na nyingine yenye Kumb. Na. PPRA/Tanesco/47/18 – zilikuwa zikitaka kusitishwa kwa zoezi la zabuni zilizozaa Richmond kwa kuwa ilikuwa kinyume cha sheria.

Aidha, PPRA ilitaka Tanesco kutafuta moja kwa moja mitambo kutoka kwa watengezaji kwa maelezo kuwa, katika mazingira yaliyopo nchini na kutokana na zabuni kwenda kinyume cha taratibu, zoezi hilo likiendelea litaingiza wazabuni feki.

Lakini katika hali isiyotarajiwa, serikali iligoma kutekeleza maagizo ya PPRA na badala yake ilijibu kwa kile kinachoitwa, “Tumepokea ushauri wenu, lakini uamuzi wa mwisho ni wetu.”

Ni katika mkakati huo, serikali iliagiza Tanesco kufungua tenda iliyowekewa masharti ya vigezo 29. Kati ya makampuni tisa yaliyoomba, hakuna hata moja iliyofanikiwa kupenya. Kampuni ya Richmond ilionekana kuwa na mapungufu 17.

Baada ya vigezo hivyo kuonekana vimeshindwa kuibeba “kampuni ya Lowassa,” ofisi ya waziri mkuu, kupitia katibu mkuu wizara ya nishati na madini, Arthur Mwakapugi, ilipunguza vigezo hivyo kutoka 29 hadi 16.

Katika mchujo huo, kampuni tano ziliteuliwa ikiwamo Richmond ambayo, hata hivyo, tayari ilikuwa ya mwisho katika mchujo wa awali.

Katika eneo hilo, wazabuni ambao angalau walionekana afadhali walikuwa wanne, yakiwemo makampuni kutoka Italia, Ujerumani, Gapco ya Tanzania na Richmond “ya Marekani.”

“Hata pale Tanesco ilipofanya tathimini ya kina, bado Richmond ilikutwa na mapungufu13 katika vigezo vilivyowekwa,” taarifa zinaeleza.

Kama hiyo haitoshi, nyaraka zinaonyesha tarehe 1 Aprili 2006, serikali kupitia waziri Msabaha ilikataa mapenedekezo ya Bodi ya Zabuni ya Tanesco iliyosisitiza kwamba “hakuna mzabuni mwenye sifa miongoni mwa wazabuni walioomba.”

Msabaha alifika mbali zaidi. Huku akijua kuwa ni kinyume cha sheria ya manunuzi ya umma kuingilia mchakato wa zabuni, barua yake inayodaiwa kuandikwa kwa maelekezo ya Lowassa, yenye Kumb. Na. CBD/88/286/01, iliagiza kuvunjwa kwa Bodi ya Zabuni ya Tanesco.

Barua hiyo ilitumwa kwa mwenyekiti wa Bodi ya Zabuni ya Tanesco.

Vilevile, Dk. Msabaha alindika barua nyingine tarehe 12 Aprili 2006 ambayo ilimtaja moja kwa moja Lowassa.

Barua hiyo yenye Kumb. Na. CBD/88/286/01, inasema “…suala hili limeshughulikiwa na waziri mkuu baada ya kuunda kamati ya wataalamu ya watu watatu, katibu mkuu wa hazina, katibu mkuu wa wizara ya nishati na madini na mwanasheria mkuu wa serikali.”

Barua hiyo ilieleza pia, “Nia ni kuliondoa suala hili mikononi mwa Tanesco na isije tena picha ya kuendelea na suala hilo, maana huko ni kukiuka maagizo ya waziri mkuu.”

Kujitumbukiza kwa Lowassa katika mchakato wa zabuni ulianza kuonekena tarehe 10 Februari 2006, mara baada ya kumalizika kwa mkutano wa Baraza la Mawaziri ulioongozwa na Rais Jakaya Kikwete, Ikulu Dar es Salaam.

Katika mkutano huo, serikali iliamuru wizara ya nishati na madini kuwasiliana na CDC kwa mambo mawili.

Kwanza, kuiomba kampuni hiyo kuuza mitambo yake moja kwa moja badala ya kuikodisha.

Pili, kama ombi la kutaka serikali kuinunua litakataliwa na CDC, basi mitambo itakayoagizwa ikodishwe katika kipindi kile tu cha ukame na kwamba baada ya ukame kumalizika mitambo hiyo irejeshwe kwa CDC.

Hata hivyo, kinyume na maagizo ya Baraza la Mawaziri, taarifa zinaonyesha mara baada ya mkutano huo, Lowassa alimuagiza aliyekuwa katibu mkuu wa wizara ya nishati, Mwakapugi kuvunja mkataba.

Katika kile kilichoelezwa kuwa ni kutekeleza maelekezo ya Lowassa, tarehe 10 Februari 2006, mara baada ya kikao cha baraza la mawaziri kumalizika, Mwakapugi aliandikia barua Kumb. Na. CBD286/297/01 kwenda CDC.

Barua ya Mwakapugi inasema, “Licha ya maendeleo mazuri mliyoyafanya katika mradi huu, serikali imeamua kufuta ukodishaji wa mitambo, badala yake itaipatia Tanesco fedha za kununua, kufunga na kuzindua mitambo yake na ya aina hiyohiyo.”

Inaarifiwa kwamba Mwakapugi alieleza Kamati za Nidhamu zilizokuwa zinasikiliza utetezi wa watuhumiwa wakuu wa Richmond, jinsi alivyokuwa tarishi wa Lowassa katika kuipa kazi Richmond.

Inaelezwa kwamba katika vikao hivyo, Mwakapugi alitoa hadi vimemo vya Lowassa vilivyokuwa vikimtaka kuvunja mkataba na kuipa kazi kampuni aliyotaka Lowassa, pamoja na kwamba alijua haikuwa na sifa kwa kila hali.

“Mle ndani ya Kamati za Nidhamu kulifumuka mambo mengi. Kuna wakati watu waliumbua wakubwa. Kwa mfano, Mwakapugi alitoa hadi vimemo vilivyokuwa vinaonyesha jinsi Lowassa alivyomshinikiza kuipa kazi Richmond, pamoja na kwamba alijua kuwa haikuwa na sifa ya kupewa kazi iliyoomba,” zinaeleza taarifa zisizopingika.

Hoja ya kupindisha maamuzi ya Baraza la Mawaziri ambapo Lowassa aliagiza kuvunjwa kwa mkataba, ilitawala mjadala wakati wa mahojiano yaliyodumu kwa siku nne kati ya Kamati Teule ya Bunge na Dk. Msabaha aliyekuwa waziri wa nishati na katibu wake Mwakapugi.

Kwa mujibu wa Hansard ya Bunge, Kamati ilitaka maelezo katika maeneo yafuatayo kutoka kwa Dk. Msahaba na Mwakapugi:

Kwanza, iwapo kulikuwa na kikao kingine cha Baraza la mawaziri kilichofanyika tarehe 10 Februari 2010 na kubatilisha maamuzi ya kwanza.

Pili, kama hakukuwa na kikao kingine cha baraza la mawaziri, kwa nini wizara ya nishati na madini ilipeleka ujumbe tofauti CDC kinyume cha maagizo ya baraza la mawaziri?

Tatu, kwa nini barua ya wizara kwenda CDC ilipelekwa hata kabla ya kampuni hiyo kujibu maombi ya serikali ya kutaka kubadilisha mkataba?

Nne, Kamati ya Bunge iliuliza: Je, maamuzi kama haya yaliyochukuliwa siku nne baada ya mgawo wa umeme kuanza, huku serikali ikiwa haina kampuni mabadala, yalikuwa sahihi au yalilenga kunufaisha kikundi fulani cha watu ndani ya serikali?

Si Msabaha wala Mwakapungi aliyeweza kujibu kwa ufasaha maswali yaliyoulizwa na Kamati.

Wakati hayo yakiwa ndani ya serikali, Kamati Teule ya Bunge iling’amua kuwa kumwita na kumhoji Lowassa kungevuruga ushahidi na kukwamisha kazi za Kamati. Aidha, ilihofia mamlaka ya rais kuingilia kati.

“Unajua, Kamati Ndogo ya Bunge, haikuwa na mamlaka ya kuhukumu waziri mkuu. Kazi ya kuhukumu au kumwajibisha, ilibaki mikononi mwa Bunge. Hilo ndilo lililomuidhinisha na ambalo linaweza kumfukuza kazi,” ameeleza mjumbe mmoja wa Kamati Teule.

Kwa mujibu wa mamlaka za Bunge, kuita na kuhoji waziri mkuu kungehitaji kibali cha Spika ambaye naye angelazimika kupata ridhaa ya rais wa Jamhuri.

“Wengi wanakiri kuwa hekima iliongoza Kamati Teule. Badala ya kumhoji Lowassa ilipendekeza kwake kujitetea mbele ya Bunge na juu ya masuala yaliyomgusa na Bunge lingeamua baada ya kusikiliza maelezo yake,” kimeeleza chanzo kingine cha habari.

Kwa kuzingatia utendaji wa Rais Kikwete na majukumu aliyonayo, kulikuwa na uwezekano mkubwa wa kuchelewa kutoa idhini ya kumhoji Lowassa.

Vilevile huenda rais angenyamaza ili asionekane mbaya na kazi mzima ya kamati ingekwama, ameeleza mmoja wa wajumbe wa Kamati alipoulizwa juu ya kiini cha Lowassa kudai kuwa bado anashikilia Richmond.

Majigambo ya Lowassa yameonekana kwa wachunguzi wa siasa za CCM kuwa njia ya kujikosha kwa kuendelea kung’ang’ania kuwa alikuwa sahihi kutoa mkataba kwa kampuni iliyofeli kutenda wajibu wake.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: