Lowassa amchokoza Kikwete


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 29 June 2011

Printer-friendly version
EDWARD Lowassa, waziri mkuu  aliyejiuzulu kwa kashfa ya Richmond

EDWARD Lowassa, waziri mkuu aliyejiuzulu kwa kashfa ya Richmond, “amemtia kidole jichoni” Rais Jakaya Kikwete.

Ijumaa iliyopita, aliishambulia serikali kwa kushindwa kufanya maamuzi mazito, yakiwamo yale yanayohusu maslahi ya taifa.

Alisema, “…hivi sasa kuna ugonjwa umezuka nchini kwa viongozi wa serikali kushindwa kutoa maamuzi magumu. Ni bora ukubali kuhukumiwa kwa kutoa maamuzi magumu, kuliko kuogopa kuyatoa.”

Akizungumza kwa mara ya kwanza bungeni tangu alipojiuzulu wadhifa wa waziri mkuu, Februari 2008, Lowassa alisema, “Hakuna jambo baya kama ugonjwa wa kuogopa kutoa maamuzi magumu.”

Lowassa alikuwa akichangia, bungeni Dodoma, hotuba ya bajeti ya ofisi ya waziri mkuu kwa mwaka wa fedha 2011/2012.

Tayari baadhi ya wachambuzi wa mambo ya siasa nchini wamesema, kauli ya Lowassa itakuwa imetokana na “kufahamu udhaifu wa kiongozi mkuu wa nchi.”

Rais Kikwete amekuwa akilaumiwa na viongozi wastaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali, viongozi wa vyama vya upinzani, asasi za kijamii na watu binafsi, kwa kutochukua hatua mwafaka pale zinapohitajika.

Haijafahamika iwapo Lowassa amejitathmini vya kutosha kabla ya kudandia hoja hiyo, ambayo pia iliwahi kushikiwa bango na Kongamano la Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF) miaka miwili iliyopita.

Bali kuna orodha ya matukio yanayomhusu hata Lowassa ambayo Kikwete hakuyatolea maamuzi – mepesi au magumu.

Kwa mfano, Lowassa alijiuzulu kutokana na shinikizo la bunge baada ya kukamilisha uchunguzi kuwa ama alishiriki au aliwezesha au alishinikiza kutolewa kwa mkataba wa kufua umeme kwa kampuni ya Richmond Development Corporation.

Ilibainika Richmond haikuwa na fedha, utaalam wala uzoefu katika uzalishaji umeme na kwa hiyo ilibebwa. Lowassa alijiuzulu. Hakustaafu.

Lakini Rais Kikwete ameshindwa kufanya maamuzi, mepesi au mazito; kumwambia Lowassa kuwa hakustaafu na hivyo hastahili marupurupu yoyote ya waziri mkuu aliyestaafu.

Bali Lowassa, akihutubia bunge, alisema, “Hakuna jambo baya kama ugonjwa wa kuogopa kutoa maamuzi magumu.”

Rais Kikwete ameshindwa kuwachukulia hatua watendaji wa serikali, akiwamo Lowassa wakati huo, kwa kuidhinisha mkataba tata wa Richmond na Dowans Holdings SA ya Costa Rica na Dowans Tanzania Limited (DHL).

Makampuni hayo ambayo yalikuwa vigumu kujua makazi ya ofisi zao na maofisa wake wanaowasiliana na serikali, yanawakilishwa nchini na mfanyabiashara na mbunge wa Igunga, Rostam Aziz ambaye amekiri mara kadhaa kufahamu wamiliki wake.

Licha ya rais kushindwa kufanya maamuzi, kama mitambo itumike au isitumike; lakini baya zaidi ameshindwa kununua mitambo mipya, hata kwa mkopo; na ameshindwa kuwabana, kuwawajibisha na hata kuwaadabisha waliohusika na maafa ya giza kwa taifa.

Rais ameshindwa kuchukua maamuzi – mepesi au mazito – kuhusu Lowassa. Hata baada ya jina lake kutajwa miongoni mwa watu watatu wanaotuhumiwa “kuchafua” chama kwa tuhuma za ufisadi zinazowakabili, Rais Kikwete ameshindwa kuchukua hatua.

Wengine wanaotuhumiwa na CCM kwa “kuichafua” ni Rostam na mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge. Majina yao yalitajwa na makamu mwenyekiti wa chama hicho, Pius Msekwa mbele ya Halmashauri Kuu ya chama hicho mjini Dodoma.

Rais Kikwete ameshindwa kuchukua hatua ya kuwafukuza kutoka kwenye chama au hata kuwapa barua za onyo. Kutochukua hatua kumefuatia maapizo ya viongozi wenzao kuwa “lazima mafisadi watoswe.”

Rais Kikwete anatuhumiwa pia kushindwa kuwafikisha mahakamani watuhumiwa wa wizi wa fedha za umma kupitia Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ndani ya Benki Kuu ya Taifa (BoT).

Fedha hizo zilizoibwa katika kipindi kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2005, inadaiwa kuwa sehemu yake kubwa ilitumika kuwaingiza madarakani; yeye na wenzake.

Badala ya kuwasweka watuhumiwa mahakamani, Rais Kikwete aliwaingiza katika mkataba usio wa haki wa kukiri kuiba na kurejesha sehemu ya walichoiba ili wasifikishwe mahakamani.

Alishindwa ujasiri wa kutaja wezi hadharani; akawaonea huruma kwa kuwapa upendeleo unaovunja Katiba ya nchi. Alishitaki hawa na kuacha wale.

Rais Kikwete analaumiwa kwa kutochukua hatua kwa waliokwapua zaidi ya Sh. 40 bilioni kutoka BoT kwa jina la Kagoda Agriculture Limited. Miongoni mwa wanaotajwa kuwa na mkono katika mkakati wa kukwapua kiasi hicho ni Rostam ambaye Kikwete amekiri kuwa ni mmoja wa maswahiba wake.

Hata watu wawili wanaotajwa kuwa waanzilishi wa Kagoda, ingawa hali zao za maisha kwa sasa hazionyeshi kuwa waliwahi kushika hata Sh. 500,000 kwa wakati mmoja, hawajafikishwa mahakamani.

Hakuna ushahidi kwamba wakili wa kujitegemea wa jijini Dar es Salaam, Bhyidinka Michael Sanze, ambaye alinukuliwa na gazeti hili, katika andishi maalum kwa Kamati ya Rais kuhusu wizi wa Kagoda, aliishawahi kutumiwa kukama wezi.

Wote ambao wakili alitaja, akiwemo Rostam, ambaye anadai alimwita ofisini mwake, Na. 50 Mirambo jijini Dar es Salaam, ambako alishuhudia hati za Kagoda za kuiba fedha, hawajawahi kukamatwa.

Katika hili la Kagoda, Rais Kikwete hajawahi kuchukua uamuzi mzito au hata mwepesi katika kurejesha fedha za umma.

Hata baada ya Yusuf Manji kukiri kuwa anajua Kagoda; kwamba aliwalipia deni lao serikalini na kwamba anawadai, serikali ya Rais Kikwete haijachukua hata uamuzi mwepesi wa kukabiliana na Manji ili kupata fununu juu ya Kagoda.

Lakini ni Kamati ya rais ya kuchunguzi wizi iliyoamua kiasi gani Kagoda walipe iwapo hawataki kupelekwa mahakamani. Hivyo Rais Kikwete anajua Kagoda ni nani, alichukua kiasi gani na walimtaka alipe kiasi gani.

Katika hili, rais amebaki amenyamaza kama mlinzi mkuu wa mafisadi hao, badala ya kuwa tishio kwao. Ameshindwa kuchukua maamuzi; hata mepesi.

Aidha, Rais Kikwete ameshindwa kufanyia kazi tuhuma zinazoikabili kampuni ya Deep Green Finance Ltd., ambayo ilikwapua Sh. 8 bilioni kutoka BoT. Kampuni ya mawakili ya IMMA Advocates and Co. ya Dar es Salaam ndiyo ilisadia usajili wa Deep Green na ndiyo iliyowafilisi (!)

Deep Green Finance Limited ilichota fedha hizo kati ya Septemba na Desemba 2005 wakati wa mchakato kuelekea uchaguzi mkuu wa 2005.

Rais ameshindwa kuchukua maamuzi kuhusu tuhuma za ukwapuaji wa mabilioni ya shilingi kutoka Hazina na BoT. Makampuni hayo ni pamoja na Tangold Limited na Meremeta.

Kampuni ya Meremeta pekee ilichota zaidi ya Sh. 155 bilioni kutoka BoT. Kwa miaka mitano sasa, serikali imekuwa ikijibaraguza kwa kusema Meremeta ni kampuni ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) iliyokuwa na kazi ya kuchimba dhahabu katika mgodi wa Buhemba, mkoani Mara.

Hata hivyo, MwanaHALISI lilithibitishia ulimwengu, kwamba kampuni hiyo  ilianzishwa kwa kazi ya ununuzi na uchimbaji dhahabu nchini; iliandikishwa nchini Uingereza mwaka 1997 na baadaye kufilisiwa nchini humo mwaka 2006.

Katika hatua ya kujinasua, waziri mkuu Mizengo Pinda aliwahi kusema Meremeta ni mali ya serikali kwa asilimia 100, jambo ambalo halikuwa sahihi. Mali za Meremeta, kwa mujibu wa katiba yake, zinaweza kurithiwa na wazazi, ndugu na wengine kama binamu. Iko wapi serikali yenye baba, watoto, binamu na wajukuu?

Mpaka sasa, serikali ya Kikwete imeshindwa kuifanyia kazi au kuitoa hadharani ripoti ya wakaguzi waliokagua BoT, Juni 2006. Taarifa zinasema ndani ya ripoti hiyo ndimo sakata la Meremeta liliibuliwa.

Kwa yote haya, Rais Kikwete alikaa kimya na anaendelea kukaa kimya. Ngao yake kuu imekuwa kukaa kimya na bila kuchukua hatua yoyote – ngumu au nyepesi.

Kuna hili la gavana wa BoT Daudi Balali. Pamoja na kwamba wakati anaondoka nchini kwa kile kilichoitwa “kwenda kutibiwa Marekani,” kashfa nyingi za ufisadi zilikuwa zimeibuliwa, serikali ya Kikwete ilimnyang’anya ugavana peke yake, bila hata kumshitati akiwa hayupo.

Juu ya hilo, serikali haikutoa maelezo ya wazi kabisa kuhusu ilichoita “kifo cha Balali nchini Marekani.” Ukungu uliotanda juu ya kimya cha Balali ulihitaji kauli ya rais. Hakusema. Hakuchukua hatua ya kuondoa wananchi gizani.

Hata waandishi wa habari walipotaka kujua aliko Balali, wakati fulani waliambiwa na ofisi ya mkurugenzi wa mawasiliano ikulu kwamba “Serikali ina mkono mrefu. Balali akihitajika ataletwa…” Hakuletwa na haijulikani kama bado serikali ina uwezo wa kumleta.

Uuzaji holela wa mgodi wa mkaa wa mawe Kiwira na uuzaji wa nyumba za serikali ambazo Kikwete aliapa kuzirejesha, ni miongoni mwa mambo ambayo rais ameshindwa kufanyia maamuzi.

Rais Kikwete ameshindwa kushughulikia wizi uliofanywa katika ununuzi wa rada ya kijeshi. Rais anafahamu watuhumiwa, lakini amekataa kuwapeleka mahakamani.

Hata baada ya msaada wa Uingereza, hadi mbunge machachari mwanamke Clare Short kujiuzulu akipinga uuzaji rada hiyo kwa “nchi masikini” na kwa bei iliyopitiliza, bado serikali ya Kikwete ilikaa kimya.

Leo ndio serikali inajikakamua kupinga masharti ya kurejeshewa fedha zilizokuwa zimeibwa na kampuni ya BAE. Lakini haijaonyesha kuwajibika kwa kuchunguza, kukamata na kupeleka mahakamani wale wote waliokula mlungula katika ununuzi huo.

Miongoni mwa yaliyotajwa ambayo Rais Kikwete ameshindwa kuchukulia maamuzi mepesi au mazito, kuna ambayo yalitendeka Lowassa akiwa waziri au waziri mkuu.

Hili ndilo linafanya wachunguzi wa mambo ya kisasa wajiulize zaidi juu ya hatua ya Lowassa kumtia kidole jichoni. Ameamua kuingia “siasa za kuumbuana” au anatafuta upenyo wa kurejea kileleni kwa kutamka yale ambayo yaweza kumpa umashuhuri?

Kusema ni jambo moja. Kuaminika ni jambo jingine. Lakini ni siku sita tangu Lowassa ajiunge na wale ambao wamekuwa wakisema Kikwete na serikali yake wanashindwa kuchukua uamuzi mgumu juu ya masuala muhimu ya kitaifa.

Bado taifa halijasikia sauti ya Rais Kikwete kupinga au kukubaliana na tuhuma dhidi yake. Inawezekana hata kwa hili atashindwa kuchukua uamuzi mgumu au mwepesi wa kujibu tuhuma dhidi yake binafsi na serikali yake?

0
Your rating: None Average: 3.8 (4 votes)
Soma zaidi kuhusu: