Lowassa amekumbuka vijana uzeeni


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 28 March 2012

Printer-friendly version

HAKUNA ubishi, ajira ni tatizo kubwa nchini. Tena, vijana ndio waathirika wakubwa wa tatizo hili. Wapo wasiokubali hili, wao wanawaangalia vijana kama ndio tatizo.

Edward Lowassa, waziri mkuu aliyejiuzulu kwa shinikizo za Bunge lililomtuhumu kukiuka maadili ya uongozi katika sakata la mkataba wa kifisadi wa Richmond, “ameisimamia vidole” hoja hii. Amefikia hatua ya kulifananisha tatizo na bomu linalosubiri kulipuka.

Lowassa (59) amenukuliwa katika matukio manne tofauti kuanzia mwishoni mwa mwaka, akionya tatizo la ajira kwa vijana linahitaji kupatiwa ufumbuzi wa haraka.

Tarehe 15 Novemba 2011, akiwa katika harambee ya ujenzi wa Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph Makasa, Parokia ya Nyakato, Mwanza, alililitaka kanisa lisaidie kujenga vyuo vya ufundi ili kuajiri vijana.

Akitoa takwimu alizodai zimetokana na utafiti wa mwaka 2006, alisema tatizo hilo kwa sasa limekua na kufikia asilimia 15 huku likigusa zaidi vijana wenye umri wa kati ya miaka 15 na 24. hao ndio nguvukazi kubwa zaidi kwa taifa.

Akiwa katika harambee nyingine kusaidia Kanisa, safari hii la Kiinjili la Kilutheri (KKKT), Usharika wa Amani Sabasaba, Singida, 29 Novemba, 2011, Lowassa aligusia suala hilohilo.

Hata alipokutana na waandishi wa habari mkoani Arusha mwaka jana, Lowassa alizungumzia tatizo hilo la ajira. Ni hapa alilifananisha na bomu.

Inavyoonekana, Lowassa ameamua kulifanya suala hili mtaji mzuri wa kisiasa. Wiki iliyopita, alipokuwa kwenye sherehe za uzinduzi wa Jimbo jipya la Kanisa Katoliki Ifakara, aliwasihi maaskofu watoe kipaumbele kusaidia kutatua tatizo la ajira kwa vijana.

Sasa wenye utawala wameamua kusema. Labda maneno yake ni makali yamemtoa “nyoka pangoni.”

Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, Gaudensia Kabaka anasema tatizo hilo haliwezi kufafanishwa na bomu. Anatuhumu wanaolichukulia hivyo tatizo hilo hawaitendei haki serikali.

Anajenga hoja kwa kutoa takwimu: Tatizo limepungua kutoka asilimia 12.9 mwaka 2000/2001 hadi asilimia 11.7 mwaka 2006. Serikali imeanza kuchukua hatua, imeandaa programu inayotarajiwa kuanza kutekelezwa mwaka wa fedha ujao. Lengo ni kutambua vijana wote wenye taaluma, na aina ya ujuzi walionao katika kila wilaya nchini.

Anasema programu hii imelenga kuwajengea uwezo vijana katika kukuza ari ya kijasiriamali, kuwawezesha kupata ujuzi wa kujiajiri na kukuza soko la bidhaa za ndani.

Kama vile Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye anavyomuuliza Lowassa, waziri Kabaka naye anahoji: “(Yeye Lowassa) alifanya nini kuondoa tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana alipokuwa Waziri Mkuu, naye waziri Kabaka anastahili kuulizwa, “alichelewa wapi kutoka na kueleza mikakati ya serikali katika kutegua bomu la ajira kwa vijana.”

Pia Lowassa angeweza kuulizwa alikuwa wapi katika utumishi wake wa muda mrefu serikalini? Tukumbuke, tatizo hili si la leo wala jana. Mwana-CCM huyo amekuwa katika serikali za awamu zote, hajapata kulieleza namna anavyolieleza sasa.

Au tuseme alishindwa kuwatetea vijana wenzake wakati huo, akasubiri hadi azeeke ndipo awaone vijana wa sasa anaosema ni bomu kwa taifa? Au kwa umri wake huu (wa kustaafu) ndio uwezo wake wa kubaini matatizo yanayowakabili Watanzania umeongezeka?

Lowassa, na rafiki yake, Rais Jakaya Kikwete wamekuwa viongozi katika chama kinachotawala, CCM, tangu ujana wao baada ya kuhitimu Chuo Kikuu, wakiwa ngazi za chini. Wamepanda hadi kuingia vikao vya juu vya maamuzi vya CCM.

Wameshika nafasi za uwaziri hivyo kuwa wajumbe wa Baraza la Mawaziri. Wamepanda hadi ngazi ya uwaziri mkuu na urais, lakini kipindi chote tatizo la ajira limekuwapo na limekua.

Kimsingi, tatizo hili si jipya nchini. Limekuwa ajenda kuu ya upinzani, na hasa katika ilani za uchaguzi za vyama hivi. Wamekuwa wakidharauliwa.

Na serikali imeendelea na mikakati ya kubinafsisha viwanda, kuviua baadhi na kuleta sera za uchumi ambazo utekelezaji wake hauzalishi ajira mpya. Pia serikali zote hazijaonyesha juhudi katika kushughulikia ufisadi, adui mkubwa wa ajira kwa vijana. Nitaeleza.

Wakati tunalijadili suala hili na rafiki yangu mmoja, alihoji, kumbe Lowassa analijua tatizo hili! Nikamuuliza kwa nini? Akasema “huyu ndiye ‘alimbeba’ Rais Kikwete” na kumpigania hadi akawa rais kupitia mtandao wao. Kama ana uchungu na vijana, iweje suala hili halikuwa katika vipaumbele vyao – yeye na rafiki yake?”

Akaendelea kuhoji, “Huyu ametamka mara nyingi Rais Kikwete ni rafiki yake ambaye hawakukutana barabarani, na mwenyewe (Kikwete) hajawahi kukanusha. Sasa ameshindwaje kumshauri jinsi ya kulitegua bomu ili mtandao wao wa kusaka madaraka kwa zamu uonekane wa manufaa kwa taifa? Au anasubiri tatizo hili limsaidie kama ngazi ya kuvuka kwenda ikulu?”

Ukubwa wa tatizo hili uko wazi, lakini halijawahi kuwa katika mjadala. Mjadala wake umeanzishwa sasa na unaelekea kuimarika kwa sababu kadhaa.

Wengine wanasema kwa sababu umeanzishwa na Lowassa, na wengine wanasema kwa kuwa tatizo hili limetumika kama “ngazi pekee” ya kumvusha mtu (huyu) kuingia ikulu.

Ingawa yeye hajatangaza rasmi, mimi sioni tatizo kwa yeye kuibeba hoja hii kwa vyovyote atakavyo, bali asingeifanya ngazi pekee, angeangalia na maeneo mengine ikiwemo kinachosababisha taifa kukabiliwa na bomu hilo na umasikini kuongezeka.

Mathalan, angeanza kwa kueleza umma mbinu gani zitumike katika ujenzi wa viwanda vipya vya umma na vya binafsi, ili kukuza uzalishaji na usindikaji wa bidhaa. Hayo yangeongeza ajira kwa vijana na mapato kwa serikali.

Ili aaminike katika mkakati wa kutegua bomu hili, Lowassa alipaswa kueleza namna alivyopambana kumaliza na aliposhindwa, ili ionekane kama safari hii amekusudia kwa dhati au angali kwenye usanii wa kisiasa.

Angetaja dawa ya tatizo la umeme nchini, unaokatika mara kwa mara, na kusababisha viwanda vingi kufungwa au kupunguza wafanyakazi.

Ndio, tatizo la ubaha wa umeme linaongeza gharama za uendeshaji viwandani, huku serikali na Shirika lake la Umeme (TANESCO), ikilazimika kulipa mabilioni ya shilingi kwa wakodishaji wa mitambo ya umeme, hivyo kunufaisha mafisadi na kuwapa mzigo Watanzania kulipia mikataba mibovu.

Tungesikia mikakati yake katika kupambana na ufisadi hadi serikali kushindwa kuajiri vijana. Ajue ufisadi unadhoofisha uwezo wa serikali kukuza uchumi na kuhudumia wananchi wakiwemo vijana wanaokwama kuingia vyuoni kwa kukosa mikopo ambayo serikali iliahidi kuwapa.

Mbinu za namna hiyo zingeweza kuwa ufunguo mzuri kwa Lowassa kutegua bomu la ajira kwa vijana kuliko kulialia kila siku eti bomu hilo linakaribia kulipuka lenyewe.

0788 346175
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: