Lowassa amkatia rufaa Kikwete


Alfred Lucas's picture

Na Alfred Lucas - Imechapwa 15 June 2011

Printer-friendly version
Atinga kwa Nabii Joshua kuombewa
Waziri Membe ateta na Rostam Aziz
Edward Lowassa

EDWARD Lowassa, mwanasiasa anayetajwa “kujipanga kugombea urais mwaka 2015,” ametinga nchini Nigeria kufanya maombi, MwanaHALISI limeelezwa.

Taarifa zilizopatikana jijini Dar es Salaam, mwishoni mwa wiki zilisema, Lowassa aliondoka nchini Ijumaa. Alikutana na Nabii Joshua na kushiriki katika misa ya pamoja iliyofanyika Jumapili iliyopita.

Maombi haya, kwa mujibu wa mmoja wa wabunge wafuasi wake, yanalenga “kukata rufaa kwa nabii, kutafuta utakaso kisiasa, kupata nguvu na ujasiri” kabla ya kuingia katika kinyang’anyiro cha nafasi ya juu ya kisiasa nchini.

Misa ya Nabii ilionyeshwa katika Emmanuel TV ya Nigeria ambayo inaonekana duniani kote. Angalau watu watatu wa jijini Dar es Salaam na mmoja aliyeko Swaziland, wameliambia gazeti hili kuwa wamemwona Lowassa akiwa katika jumba la maombi la Nabii Joshua.

Kupatikana kwa taarifa hizi kumekuja katika kipindi ambamo Lowassa anakabiliwa na kibarua kigumu cha kujisafisha na kujitetea ili asiweze kufukuzwa kutoka ndani ya chama chake.

MwanaHALISI limeshindwa kumpata Lowassa kueleza kwa undani kilichompeleka nchini Nigeria katika kipindi hiki muhimu cha mkutano wa Bunge la Bajeti.

Hata hivyo, wachambuzi wa mambo ya kisiasa wanasema safari ya Lowassa itakuwa imelenga, ama kumshitaki Rais Jakaya Kikwete ambaye taarifa zinasema ameapa kumfukuza yeye na wenzake ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), au kupata tiba ya maombi au kutubu kile kinachoweza kuitwa “makosa ya huko nyuma.”
Mbali na Lowassa, wengine wanaotakiwa kufukuzwa uongozi ndani ya chama na Kikwete, kwa hoja kwamba “wamechafua” sura ya chama hicho mbele ya wanachama na wananchi, ni Rostam Aziz na Andrew Chenge.

Lowassa anatuhumiwa kuipa kazi ya kuzalisha umeme kampuni ya Richmond Development Company (LLC), ambayo ilithibitika kutokuwa na uwezo, sifa wala fedha za kufanya kazi iliyoomba.

Rostam amekuwa akitajwa katika wizi kwenye akaunti ya madeni ya nje (EPA) katika Benki Kuu ya Taifa (BoT) uliofanywa na kampuni ya Kagoda Agriculture Ltd., pamoja na mikataba tata ya kufua umeme ya Richmond/Dowans.

Hata hivyo, gazeti hili linaweza kuthibitisha kuwa Lowassa amekwenda peke yake huko Nigeria, kwani wenzake wako hapa nchini. “Kama ni kitafuta kinga, naona watatafuta hapahapa au nchi nyingine,” amechombeza mmoja wa wafuasi wa karibu wa Rostam.

Miezi mitatu iliyopita, gazeti hili liliripoti mbunge wa Kilindi (CCM), Beatrice Shelukindo akitoa ushuhuda kuwa “Lowassa ndiye rais ajaye wa Tanzania.”
Beatrice ambaye alikuwa akijitambulisha kuwa mmoja wa “wapambanaji dhidi ya ufisadi,” amekuwa mfuasi muhimu wa Lowassa kiasi cha kumtafutia hata wenzake, akiwamo mbunge wa viti maalum, Pindi Chana, kujiunga na kambi yake.

Chana pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu (CC) na Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM, vikao ambavyo vinatarajiwa kuamua hatma ya kisiasa ya Lowassa na pengine mustakbali mzima wa CCM.

Tarehe 14 Februari mwaka huu, Beatrice alieleza Chana jinsi ambavyo “mungu alivyo wa ajabu.” Alisema, “Mungu ni wa ajabu, (Lowassa) ameniombea kura pasipo maelezo. Ameandaa lunch na dinner (vyakula vya mchana na usiku) ambako amekuwa akiniombea kura. Ana njia za ajabu za kufanya mambo. Ahsante kwa kukubali kuhesabu kura,” inasema sehemu ya ujumbe huo.

Katika andishi lake kwa mkono kwa Chana, Beatrice alisema, “Nimezungumza na TB Joshua wa Emmanuel TV Nigeria, aliyenipa unabii kuwa rais ajaye Tanzania ni Edward Lowassa… akaniambia his past is over (maisha yake ya nyuma si kitu).”

Wakati hayo yakiendelea, taarifa ambazo gazeti hili limepata wakati tukienda mitamboni zinasema, Rostam amekutana kwa faragha na waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa, Benard Membe na kuapa kuwa hata iweje, hakuna atakayewang’oa (yeye, Lowassa na Chenge) katika chama hicho.

Membe na Rostam walikutana mjini Dodoma wiki ya kwanza ya mkutano wa Bunge la bajeti.

Mtoa taarifa anasema Rostam alimweleza Membe, hatua zilizochukuliwa kumweka Kikwete madarakani mwaka 2005 na kuapa kwamba njia hiyohiyo iliyotumika kumuingiza ndiyo watakayoitumia katika uchaguzi wa mwaka 2015 na kupata ushindi.

Alipoulizwa Rostam, kwa njia ya ujumbe wa simu (sms) juzi Jumatatu, saa 2 na dakika 34 asubuhi, mbunge huyo wa Igunga hakutuma majibu. Bali Membe alipoulizwa kuhusu mazungumzo yake na Rostam, kwanza alikiri kukutana naye, lakini aligoma kueleza kile walichozungumza.

Hata hivyo, mtoa taarifa ameeleza kuwa katika mazungumzo hayo, Rostam alimuomba Membe kumueleza Rais Kikwete jinsi ya kushunghulikia matatizo yao kwa amani na kwa mustakabali wa chama hicho. Haikufahamika mara moja, njia ambayo Rostam alipendekeza kutumika.

Lakini mtoa taarifa aliyesema kwa sharti la kutotajwa gazetini, amenukuliwa akisema, “Unajua, Rostam alimweleza Membe kuwa wanafanya kazi kubwa ya kuwaangamiza kisiasa, lakini akamuapia kuwa hawatafanikiwa.”

Mtoa taarifa anasema Rostam alimkumbusha Membe kwamba mwaka 2005, Kikwete alikataliwa na sekretarieti nzima ya CCM. Lakini yeye na Lowassa waliunda mtandao mwingine nje ya chama na wakafanikiwa kuubadilisha msimamo wa baadhi ya viongozi wakuu wa chama hicho, akiwamo mwenyekiti wake wa wakati huo, rais mstaafu Benjamin Mkapa.

“Ndani ya sekretarieti nzima ya CCM, Kikwete hakukubalika. Lakini sisi tukatengeneza mtandao wetu mwingine nje ya chama na tukafanikiwa kubadilisha maamuzi ya chama. Sasa kama hayo tuliweza kuyafanya, tutashindwaje kuyafanya mwaka 2015,” anaeleza mtoa taarifa akimnukuu Rostam.

Gazeti hili limeelezwa, hata hivyo, kwamba Lowassa anapanga kukutana na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kabla ya kikao cha NEC kinachotarajiwa kufanya maamuzi juu ya watuhumiwa wa ufisadi.

Hapa ndipo Lowassa anatarajiwa kumwaga kile wanachoita “mchele mbele ya njiwa” ili Tanzania na dunia waweze kupata majibu ya tuhuma dhidi yao.

Maombi nchini Nigeria, maandalizi ya mkutano na waandishi wa habari na mkakati anaosema Rostam, ni kete za mwisho za kujinasua za watuhumiwa watatu wa ufisadi ndani ya CCM.

0
Your rating: None Average: 4.2 (6 votes)
Soma zaidi kuhusu: